Mahakama
ya Hakimu Mkazi Arusha imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya
udiwani katika kata ya Musa wilayani Arumeru Magharibi iliyofunguliwa na
mgombea wa CCM, Flora Zelote dhidi ya diwani wa Chadema, Loth Laizer.
Akitoa
uamuzi wa hukumu hiyo iliyosomwa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo,
Mwamkuga Gunta, alisema haoni kama kuna kasoro yoyote katika uchaguzi
huo uliompa ushindi Laizer.
Akitoa
uamuzi, Gunta alisema licha ya Zelote kudai kudhalilishwa pamoja na
kuibiwa kura lakini ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi
mbalimbali hautoshi kudai kuwa alipokwa ushindi wa kuwa diwani wa kata
hiyo.
“Natupilia
mbali kesi hii sababu ushahidi uliotolewa mahakamani hapa hautoshi
kumvua udiwani diwani wa Chadema, pia mashahidi waliotoa ushahidi
mahakamani hapa ushahidi wao umejichanganya hivyo natupilia mbali kesi
hii,” alisema Gunta.
Awali
kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo wiki iliyopita, Hakimu Gunta aliomba
radhi kwa kutokamilisha hukumu hiyo kwa sababu alikuwa akiuguliwa hivyo
aliahidi kutoa hukumu jana, Machi 29.
Kesi
hiyo ambayo awali ilisikilizwa kwa siku mbili mfululizo kwa zaidi ya
saa nane kila siku, mashahidi wote walikamilisha ushahidi wao akiwamo
Laizer aliyekiri mahakamani hapo kuwa aliongozana na kundi kubwa la
wafuasi wa chama chake kwenda katika kituo kikuu cha kujumlishia matokeo
ya udiwani katika kata hiyo kilichokuwa katika shule ya sekondari ya
Musa.
Hata
hivyo, akiongozwa na wakili wake Adiel Charles, diwani huyo alishindwa
kukanusha lugha ya matusi iliyotolewa na wafuasi wake aliyokuwa
ameongozana nao Oktoba 25 mwaka jana, wakiwa na silaha za jadi ambazo ni
sime na fimbo pamoja na kutishia usalama wa maisha ya mgombea wa CCM,
Zelote.
Wengine waliotoa ushahidi wa upande wa mlalamikiwa ni pamoja na msimamizi msaidizi wa uchaguzi kata ya Musa, Tuwati Leondoya.
Wengine
ni Lomito Robert na Ally Mollel. Kwa upande wa mlalamikaji, mashahidi
watano walitoa ushahidi akiwamo Zelote, Meimoite Kivuyo, Lekisongo
Singa, Edson Lesikari na Alex Lukumay.
Kesi
hiyo ya uchaguzi namba sita ya mwaka 2015 ilifunguliwa mahakamani hapo
na Zelote aliyekuwa mgombea wa udiwani katika kata hiyo kwa tiketi ya
CCM dhidi ya Laizer wa Chadema.
Zelote
alifungua kesi hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa
taratibu za kampeni pamoja na uchaguzi zilizotolewa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC). Laizer alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo.
0 comments:
Post a Comment