Saturday, 12 March 2016

Updating>>> Dr Vicent Mashinji Atangazwa Rasmi Kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA Kuchukua Mikoba ya Dr Slaa.

Dr. Vicent Machinji ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kupitishwa na Baraza Kuu la Chadema, katika kikao chake kilichokaa jijini Mwanza.

Katika Kikao hicho cha Baraza Kuu kilichodumu hadi saa  nne usiku, Freeman Mbowe alitangaza jina la Dk. Machinji na kuungwa mkono na wajumbe wa baraza hilo, hivyo anajaza nafasi iliyoachwa na Dk. Willibrod Slaa, aliyejienguwa ukatibu mkuu wa chama hicho.

Jina la Dk. Machinji halikuwa miongoni mwa wanachama wa Chadema ambao walikuwa wanatarajiwa kumrithi Dk. Slaa kwani waliokuwa wanatabiriwa kukatia kiti hicho ni Salum Ally Mwalimu, Frederick Sumaye, Benson Kigaila, John Mnyika, Dk. Marcus Albanie na Prof. Mwesiga Baregu.

Nafasi ya Katibu wa Chadema ilikuwa wazi tangu Dk. Slaa alipoondoka Chadema muda mfupi baada ya chama hicho kumpitisha Edward Lowassa aliyetokea CCM kuwa mgombea urais wa chama hicho na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Dr. Mashinji  ni  nani?
Dk Mashinji aliyezaliwa katika Wilaya ya Sengerema, alianza elimu ya msingi katika Shule ya Iligamba Januari 1981 hadi Oktoba 1987 na kisha kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari ya Makoko Seminari kuanzia Januari 1988 mpaka Oktoba 1991 alipohitimu na kufaulu kujiunga na Shule ya Sekondari Mzumbe kuanzia Julai 1992 hadi Juni 1994 alipohitimu kidato cha sita.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere Uganda mwaka 1995 hadi alipohitimu mwaka 2001 na kutunukiwa shahada ya udaktari. 


Mwaka 2003 hadi 2005 alisomea Shahada ya Uzamili ya Anaesthesiology katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) na mwaka 2007-2010 alijiunga na Taasisi ya Teknolojia ya Blekinge ya Sweden ambako alisomea Shahada nyingine ya Uzamili, safari hii katika Utawala na Biashara (MBA).

Hivi sasa ni mwanafunzi wa Shahada nyingine ya Uzamili katika Afya ya Jamii anayosomea Chuo Kikuu cha Roehampton, Uingereza na pia Shahada ya Uzamivu ya Uongozi katika Chuo Kikuu Huria

0 comments:

Post a Comment