WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameikaribisha kampuni ya ujenzi ya Moladi Tanzania
ielekeze nguvu zake Dodoma ambako kuna mahitaji makubwa ya nyumba za
watumishi.
“Natambua
kuwa mnatumia teknolojia ya kisasa na ujenzi wa nyumba zenu unachukua
siku chache sana. Ninawaencourage mje Dodoma ambako kuanzia Machi
mwakani, watumishi wengi wataanza kuhamia huko,” amesema.
Waziri
Mkuu ametoa wito huo jana mchana (Jumatano, Oktoba 12, 2016) wakati
akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Abeid Abdallah
ambaye alifika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam na
kumuonyesha ramani ya nyumba za watumishi ambazo wanazitumia.
Waziri
Mkuu alisema Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina maeneo
ambayo imeyatenga rasmi kwa ajili ya viwanja vya makazi na anaamini
katika muda wa miezi miwili wanaweza kujenga nyumba za kutosha watumishi
wanaotarajiwa kuhamia katika awamu ya pili.
“Nimeangalia
michoro yenu, nyumba za vyumba vitatu vya kulala zina hadhi ya kukaa
hata wakurugenzi; na watumishi wa kawaida wanaweza kumudu zile za vyumba
viwili vya kulala… ninawatia moyo mwende haraka Dodoma na wale ambao
wako serious wataleta maombi yao mara moja,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema amefarijika kuona kuwa size ya ramani zao inatosha kwenye
kiwanja cha ukubwa wa mita za mraba 550 ambacho ni high density na
watumishi wengi wanaweza kumudu kuvinunua.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi huyo, Bw. Abdalla alimweleza Waziri Mkuu kwamba
nyumba ya ukubwa wa vyumba vitatu vya kulala, yenye sebule, jiko, stoo
na choo inatosha eneo la mita za mraba 94 tu.
“Kati
ya vyumba hivyo vitatu, kimoja ni master, pia kuna sebule, chumba cha
kulia na kibaraza. Hii inaanzia shilingi milioni 35 hadi milioni 41
kutegemea na aina ya vifaa unavyoweka kwenye umaliziaji. Lakini
tukiongeza na servant quarter utalazimika kulipia shilingi milioni 7
ambapo unapata vyumba viwili na choo na bafu ndani,” alisema.
“Kimsingi,
ni lazima tutaweka madirisha, milango, vyoo, masinki ya bafuni na
jikoni, tiles (na mtu anaruhusiwa kuchagua za China, Italy au Spain),” aliongeza.
Akifafanua
kuhusu nyumba yenye vyumba viwili vya kulala, Bw. Abdalla alisema nayo
pia ina sebule, jiko, stoo na choo kimoja na inatosha eneo la mita za
mraba 54. Alisema nyumba hizo zinaanzia sh. milioni 20 hadi 25
kutegemeana na aina ya vifaa vinavyowekwa kwenye umaliziaji.
Alisema
ujenzi wa nyumba moja unachukua wiki sita na kama viwanja viko eneo
moja au jirani, wanaokoa muda wa siku tatu hadi tano kwa kila nyumba.
“Tunajenga
ukuta kwa kumwaga theluji isiyochanganywa na kokoto ambayo ni
mchanganyiko wa saruji, mchanga na kemikali. Inakauka baada ya saa saba
na ukuta wetu ni imara mara nne zaidi ya ukuta uliojengwa na tofali la
zege.”
Teknolojia
yetu inawezesha ukuta wa nyumba nzima kukamilika ndani ya siku sita,
nyumba zetu zinastahimili matetemeko, vimbunga na ujenzi wake unapunguza
gharama za ujenzi kwa asilimia 40.
Akizungumzia
kuhusu upatikanaji wa nyumba hizo, Bw. Abdalla alisema wana mikataba na
mabenki kwa hiyo wanaweza kujenga nyumba na kuziuza mara moja lakini
pia wananchi wanaweza kuingia mikataba na mabenki na kulipia kidogo
kidogo katika muda maalum (mortgage).
0 comments:
Post a Comment