KIONGOZI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, amefunguka kwa kuelezea safari yake aliyoifanya nje ya nchi hivi karibuni, baada ya taarifa mbalimbali kudai kuwa alilikimbia Jeshi la Polisi.
Akiongoza
ibada kanisani kwake, Ubungo, jijini Dar es Salaam jana, Askofu Gwajima
alisema aliondoka nchini kwenda Japan Juni 15, mwaka huu, kwa ndege ya
Emirates.
Akitoa
mahubiri katika ibada jana, Gwajima alisema alifika mjini Osaka Juni 16
na kuanza mkutano wa kuhubiri injili na siku zilizofuata alikwenda
katika miji mbalimbali.
Askofu
Gwajima ambaye aliingia kanisani hapo saa 5:00 asubuhi na kuanza
kuhubiri dakika 15 baadaye, asubuhi alitumia muda wa saa tatu hadi saa
8:20 kumaliza mahubiri yake.
Baada
ya kuanza kuhubiri, alielezea safari hiyo kwa kutaja miji aliyekwenda
ikiwamo Nagoya alikohubiri kwa siku mbili, Karuizawa, Ibaraki, Hiloshima
na Yanakochi.
“Safari yangu ilikuwa ya mafanikio sana. Tulisafiri salama na kuzunguka miji mbalimbali na tulirudi Jumatatu ya wiki iliyopita,” alisema Askofu Gwajima.
Kadhalika,
katika mahubiri hayo, Gwajima aliwakumbusha waumini wa kanisa hilo
kuhusu kuhama kwa kanisa hilo, kwa kuwatajia siku ya mwisho ya kumalizia
michango kwa ajili ya ujenzi wa kanisa jipya kuwa ni Julai 30, bila ya
kutaja sehemu ambayo kanisa hilo litahamia.
Hata hivyo, Askofu Gwajima wakati wote wa mahubiri, hakuzungumzia suala la kuhojiwa kwake na Jeshi la Polisi.
Wakati huo huo, mwandishi alizungumza
na Msaidizi wa Askofu Gwajima, Yekonia Bihagaze, kuhusu tetesi za
kufungiwa kwa kanisa hilo na kusema taarifa hizo si za kweli bali ni
maneno ya mitaani.
“Hayo maneno si ya kweli. Si umeona ibada imeendelea kama kawaida na Askofu amehubiri? Maneno ya mtaani usiyalete kanisani,” alisema Bihagaze.
Julai
12, mwaka huu, Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere
(JNIA) kilimkamata Askofu Gwajima wakati akitokea Japan kwa kutumia
ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.
Baada
ya kukamatwa, alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili
ya kuhojiwa, akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi uliopita.
Jeshi
la Polisi lilikuwa likimtafuta Askofu Gwajima baada ya kusambazwa
mkanda kwenye mitandao ya kijamii unaodhaniwa una sauti yake.
Katika
mkanda huo, Gwajima anapendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete afikishwe
mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake, ambayo kwa
sasa Rais Magufuli anayashughulika kwa staili ya utumbuaji majipu.
Pia
Gwajima alisikika akimshauri Rais John Magufuli, kuhama Chama Cha
Mapinduzi (CCM) iwapo watakataa kumkabidhi uenyekiti na kwamba apeleke
muswada bungeni, kuondoa kinga ili rais ashtakiwe kwa makosa
aliyoyafanya akiwa madarakani.
Tangu
kusambaa kwa mkanda huo, Jeshi la Polisi lilikuwa likipiga kambi katika
moja ya nyumba za Askofu Gwajima, iliyoko Mbezi Salasala jijini Dar es
Salaam.
Pamoja na kupiga kambi, jeshi hilo halikufanikiwa kumkamata na baadaye ilielezwa kuwa amekwenda nje ya nchi kuhubiri.
0 comments:
Post a Comment