MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa hati ya kukamatwa kwa Hamis Tale
‘Babu Tale,’ ambaye ni meneja wa mwanamuziki wa bongo fleva,Diamond Platnumz.
Mahakama imetoa hati hiyo kutokana na Babu Tale kutotii amri ya mahakama iliyomtaka amlipe Shekhe Hamis Mbonde Sh. 250 milioni.
Babu
Tale anatakiwa alipe fedha hizo kutokana na kuvunja mkataba kati yake
na Shekhe Mbonde, kwa kuuza na kusambaza nakala za mawaidha (DVDs) bila
ridhaa ya shekhe huyo, jambo ambalo ni kinyume na haki miliki.
Kutokana
na Babu Tale na mwenzake Iddi Tale kushindwa kulipa fedha hizo kama
ilivyoamriwa tarehe 18, Februari mwaka huu, mahakama ilitoa hati ya
kukamatwa kwa wadaiwa hao tarehe 8 Julai mwaka huu.
Katika
hati hiyo, mahakama ilimuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda ya Ilala kuwa,
hadi jana tarehe 19 Julai mwaka huu awe amewakamata wadaiwa hao ili
wafike mahakamani kueleza kwanini wasipewe adhabu kwa kukiuka amri ya
mahakama.
Shauri
hilo limetajwa tena jana mbele ya Juma Hassan, Kaimu Msajili wa Wilaya
wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo alitoa hati nyingine
kumuelekeza Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni kuwakamata wadaiwa hao.
Msajili
Juma alitoa hati hiyo baada ya Mwesigwa Muhingo, Wakili wa Shekhe
Mbonde, kuomba hati hiyo ipelekwe Kinondoni kwa kuwa Babu Tale anaishi
huko na si Wilaya ya Ilala kama hati ya kwanza ilivyoeleza.
Tarehe
18 Februari mwaka huu, Jaji Augustine Shangwa, aliwaamuru wadaiwa
kulipa Sh. 200 milioni kama fidia ya kuvunja haki miliki ya Shekhe
Mbonde na Sh. 50 milioni kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na
kuvunja makubaliano.
Katika
uamuzi wake Jaji Shangwa alisema, Juni 16, 2013, Mbonde aliingia
makubaliano na wadaiwa hao na wenzake ya kufanya biashara ya kurekodi
mawaidha na kutengeneza nakala DVDs kwa ajili ya kuziuza nchini.
Wadaiwa
hao waliahidi kumjengea nyumba, kumnunulia gari na kuitangaza kazi yake
pia walimpa Sh milioni mbili na kumnunulia kanzu na kofia (baraghashia)
na kurekodi DVDs zenye ujumbe Uzito wa Kifo, Fitina Juu ya Wanawake,
Umuhimu wa Swala, Mwanadamu Yumo Ndani ya Hasara na Maadui wa Uislam.
Alisema,
makubaliano ya awali yalikuwa kurekodi halafu baadaye wakubaliane
kuhusu bei na jinsi ya kuziuza, badala yake waliziuza na kuzisambaza
nakala hizo na kujipatia faida bila kumshirikisha Mbonde ambaye alitumia
ujuzi wake.
Mbonde
kupitia wakili wake Muhingo, Gwamaka Mwaikugile na Clement Kihoko,
alifungua kesi ya madai namba 185/2013 akiiomba mahakama iamuru wadaiwa
wamlipe Sh. 700 milioni kama fidia ya kuvunja makubaliano na Sh. 50
milioni kama fidia ya hasara aliyoipata kutokana na kuvunjwa kwa
makubaliano.
0 comments:
Post a Comment