WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali kuhamia siyo siasa kama
watu wanavyodhani bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili na kwamba
Serikali inakamilisha eneo la kisheria juu ya uamuzi huo.
“Hapa
tulipofika ni hatua ya utekelezaji wa pamoja na hakuna namna nyingine
kwa sababu uamuzi umeshatolewa. Nataka niwahakikishie kwamba hii siyo
siasa, tunachokamilisha ni eneo dogo tu la kisheria juu ya uhamishaji wa
makao makuu kuja Dodoma na katika Bunge la Septemba sheria hii
itapitishwa,” amesema.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Julai 26, 2016) wakati akizungumza na
viongozi wa mkoa, Serikali za mitaa, viongozi wa dini, wajasiriamali,
wazee wa mji huo, wasafirishaji, wafanyabiashara, wakuu wa taasisi za
elimu, za kifedha na watoa huduma mbalimbali katika mkutano uliofanyika
kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Waziri
mkuu ambaye aliitisha kikao cha kazi na wadau hao mjini Dodoma,
ameutaka uongozi wa mkoa huo pamoja na wadau wake wakae na kuandaa
mpango kazi wa jinsi ya kupokea na kutekeleza uamuzi wa Serikali kuhamia
Dodoma.
Pia
ametoa siku 14 kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma kukamilisha mpango kazi
wao na kumkabidhi mapendekezo yao ili yaweze kuingizwa kwenye mpango
mkubwa wa Serikali kuu.
“Uongozi
wa Mkoa, ukishirikiana na Ofisi yangu kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais TAMISEMI usimamie na kuyaratibu majukumu
haya. Ndani ya siku 14 nipate proposal ya kwanza namna
mtakavyoyatekeleza. Naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu
kitakachowajumuisha makundi yote niliyoyataja,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu amesema chimbuko la uamuzi wa kuhamia Dodoma kuifanya makao makuu
ya Serikali lilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage
Nyerere ambayo imeendelea kudumu katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 chini ya Ibara ya 151.
“Napenda
kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,
na viongozi wengine wote wa Chama kwa kusimamia ndoto ya Baba wa Taifa
ya kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma. Ni imani yangu kuwa wananchi
wote mtaunga mkono uamuzi huu muhimu kwa Serikali yetu na wananchi kwa
ujumla, amesema.
Akiweka
msisitizo juu ya kazi kubwa inayowakabili viongozi hao, Waziri Mkuu
amesema masuala yanayotakiwa kufanyika kuanzia sasa ni pamoja na Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhakikisha eneo la makazi ya Serikali
Kuu litakalotumika kwa ofisi za wizara na taasisi zake, makazi ya
watumishi na huduma za biashara elimu na taratibu zote za kisheria za
kulitwaa zinakamilika kwa haraka na linakuwa tayari kwa matumizi.
“Natambua
kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa na inahitaji jitihada za pamoja. Hivyo
kila taasisi na mtu mmoja mmoja ana jukumu la kuhakikisha kuwa
tunajipanga vizuri na kuweka mazingira ya ujio wa Serikali katika maeneo
yote muhimu,” amesema.
Amezitaka
Mamlaka za Mipango Miji na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo mmoja wa
upatikanaji wa viwanja ambao utajulikana na kila mmoja, utakuwa wazi
usio na urasimu. “Mfumo huu wa viwanja uwekwe kwenye mfumo wa kompyuta
na uuzaji wa viwanja hivyo uwe wa kieletroniki kuepusha udanganyifu
kutoka kwa madalali,” amesisitiza.
Waziri
Mkuu ameonya CDA na Manispaa zisibadili ramani ya mipango miji
iliyokwishawekwa awali kama vile maeneo ya wazi kutumika tofauti na
makusudio yaliyokusudiwa na akaagiza maeneo hayo yote yarejeshwe na
kufufuliwa.
“Natambua
katika makazi hapa Dodoma kulitengwa maeneo ya vituo maalum
vijulikanavyo kama D Centers kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali. Cha
ajabu sasa kuna magenge, groceries na sasa naagiza kwa hadhi ya Makao
Makuu haya maeneo sasa yatumike kuwekeza maduka makubwa (shopping malls)
ambamo huduma zote mbalimbali hupatikana,” amesema.
Ameitaka
Manispaa iboresha usafi wa mazingira na bustani zake kwa kushirikiana
na taasisi mbalimbali kuzitunza. Pia ameitaka manispaa ya mji huo
ishirikiane na TANROADS kuboresha barabara zote za mitaa na taa za
barabarani mji ukae kisasa, na usalama uwe bora zaidi.
“Eneo
jingine muhimu ni Manispaa na CDA kuhamisha makundi mbalimbali ya
wafanyabiasahra na huduma za masoko yasiyo rasmi na kuyapa maeneo yaliyo
rasmi na bora zaidi. Hii ni pamoja na maeneo ya maegesho ya bajaji,
bodaboda, taxi na daladala. Pia mazingira ya Stendi Kuu yaboreshwe, vyoo
vya kulipia pia vijengwe katikati ya mji,” amesisitiza.
Waziri
Mkuu ameuagiza uongozi wa Wakala wa majengo (TBA) waorodheshe majengo
yote ya Serikali na taasisi zake yanayotumika kwa sasa na yasiyotumika,
“Nataka muyawekee utaratibu maalum wa matumizi yake ili tupate kujua
yanayoweza kutumika kwa muda kwa baadhi ya wizara na taasisi zake. Hii
ni pamoja na jengo jipya la Mkuu wa Mkoa, linaloendelea kujengwa.”
Amewataka
wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kujenga nyumba za kuishi za
kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watu watumishi na
wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa kuishi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMANNE, JULAI 26, 2016.
0 comments:
Post a Comment