WAFANYABIASHARA wawili, akiwemo Mohamed Yusufali “Choma”, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka 222 ya kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 14.
Mbali
na Yusufali aliyewahi kutajwa kuwa anajipatia Sh milioni saba kwa
dakika moja kwa njia ya udanganyifu katika mapato ya serikali,
mshitakiwa mwingine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Northern Engineering
Works Limited, Samwel Lema, ambao wanadaiwa kusababisha hasara kwa
kughushi na kukwepa kulipa kodi.
Washitakiwa
walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka kwa zaidi ya
saa tatu na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi,
akisaidiwa na Jackline Nyantori, Diana Lukondo na Wakili kutoka Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.
Mbele
ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri, ilidaiwa, katika tarehe tofauti kati
ya Januari Mosi 2012 na Desemba 31, 2014, washitakiwa hao na wengine
ambao hawajafikishwa mahakamani walipanga njama za kuidanganya Mamlaka
ya Mapato (TRA) na kujipatia Sh 14,052,011,435.
Wakili
Kishenyi akisaidiwa na Nyantori walidai, katika shitaka la tano hadi
103 kuwa, kati ya mwaka 2011 na 2013, jijini Dar es Salaam na Arusha,
washitakiwa hao walighushi stakabadhi za malipo kuonesha Kampuni ya
Northern Engineering Works Ltd imenunua bidhaa mbalimbali.
Ilidaiwa
kuwa stakabadhi hizo zilionesha kuwa kampuni hiyo imenunua bidhaa
mbalimbali kutoka kwenye kampuni tofauti tofauti ikiwemo ya Festive
General Business Ltd, Ever Global General Trading na Jambo Product Ltd,
jambo ambalo si kweli.
Wakili
Diana na Swai waliendelea kudai, katika shitaka la 104 hadi 141, kuwa
kati ya mwaka 2011 na 2015, Lema alighushi hati ya Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) kuonesha kuwa kampuni yake imenunua bidhaa mbalimbali
kutoka kampuni tofauti tofauti ikiwemo ununuzi wa vifaa vya Sh bilioni
1.7.
Wakili
Swai alidai katika shitaka la 142 hadi 219 kuwa, kwa lengo la kufanya
udanganyifu washitakiwa hao walighushi stakabadhi za malipo kuonesha
Kampuni ya Elerai Constructions Ltd, imenunua vifaa mbalimbali kutoka
katika kampuni tofauti tofauti ikiwemo Kampuni ya Blue Arrow Tanzania
Ltd.
Aliendelea
kudai shitaka la 220, linamkabili Lema ambaye anadaiwa kati ya Januari
Mosi, 2012 na Desemba 31, 2015, Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi
anayehusika kushughulikia Kampuni yake ya Northern Engineering Works Ltd
na Elerai Constructions Ltd zilizosajiliwa kama walipa kodi,
aliwasilisha nyaraka za uongo.
Inadaiwa
aliwasilisha nyaraka ambazo ni marejesho ya uongo ya Kodi ya VAT kwa
Kamishna Mkuu wa TRA jambo lililosababisha akwepe kulipa kodi ya Sh
bilioni 14,052,011,435.
Katika
mashitaka ya utakatishaji wa fedha, ilidaiwa kati ya Februari Mosi,
2012 na Februari 25, 2013 jijini Dar es Salaam na Arusha, washitakiwa
hao walijihusisha na kuhamisha Sh milioni 420 zilizotokana na vitendo
vya uhalifu.
Inadaiwa
waliziingiza fedha hizo kwenye akaunti namba 1010000541 inayomilikiwa
na Iqbal Jaferali Jafferjee iliyopo katika Benki ya I&M tawi la
Kariakoo, na kuzitoa huku wakijua zimepatikana kwa njia za uhalifu
ambazo ni kughushi na kukwepa kulipa kodi.
Iliendelea
kudaiwa katika shitaka la 222 kuwa, kati ya Januari Mosi, 2012 na
Desemba 31, 2015, Dar es salaam, kutokana na vitendo vyao vya
kuwasilisha marejesho ya VAT ya uongo kwa Kamishna Mkuu wa TRA
waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya Sh bilioni 14.
Hakimu
Mashauri aliwaeleza washitakiwa hao kuwa, hawaruhusiwi kujibu mashitaka
yao kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu
uchumi isipokuwa Mahakama Kuu.
Baada
ya kusomewa mashitaka, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo
bado unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa, hata hivyo Wakili
Alex Mgongolwa anayeongoza jopo la Mawakili wa Utetezi aliomba
kuwasilisha ombi.
Aliiomba
Mahakama ifute shitaka la utakatishaji wa fedha kwa kuwa lina mapungufu
makubwa ya kisheria ambayo hayawezi kurekebishwa wala kufumbiwa macho
isipokuwa kufutwa.
Alidai
ili shitaka liwe la utakatishaji wa fedha lazima kuwa na dhamira ya
kuficha chanzo cha fedha au lengo la washitakiwa kukwepa adhabu lakini
kama hakuna mambo hayo sheria inatoa mamlaka kwa Mahakama kuyafuta
mashitaka hayo.
Upande
wa Jamhuri uliiomba Mahakama iahirishe kesi hiyo ili wajiandae kujibu
hoja za upande wa utetezi. Hakimu Mashauri alikubali ombi hilo na
kuahirisha kesi hiyo hadi kesho kwa ajili ya kusikiliza majibu ya
Jamhuri.
Washitakiwa
wote walirudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana
dhamana. Mbali na mashitaka hayo, Choma anakabiliwa na kesi nyingine
yenye mashitaka 199 ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6
katika mahakama hiyo.
0 comments:
Post a Comment