Wednesday, 27 July 2016

#YALIYOJIRI HIVI PUNDE>>>>CHADEMA yatoa tamko kali kuhusu kuminywa kwa Demokrasia nchini.Watangaza kuanza operesheni ''Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA)''.Fahamu zaidi hapa.

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) MAAZIMIO YA KIKAO CHA KAMATI KUU ILIYOFANYIKA HOTELI YA BAHARI BEACH LEDGER PLAZA, 23-26 JULAI, 2016

1.0 UTANGULIZI
Kamati Kuu ya dharura ya Chama iliketi kuanzia tarehe 23-26 Julai, 2016 Jijini Dar Es Salaam na ilikuwa na ajenda moja mahsusi ambayo ni kujadili hali ya siasa na uchumi wa Taifa tangu serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani mwezi Novemba, 2015.

Mwenendo wa serikali hii ya CCM ya awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli, ni dhahiri kuwa umeamua kuiweka demokrasia kizuizini na kuleta utawala wa Kidikteta katika nchi yetu.

  1. MATUKIO MAHSUSI YA UKANDAMIZAJI WA HAKI NA DEMOKRASIA
NCHINI
  1. Kupiga Marufuku Mikutano ya Vyama vya Siasa: Serikali kupitia Waziri Mkuu na hatimaye Rais na jeshi la Polisi walitangaza kwa nyakati tofauti kwamba ni marufuku kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa mpaka mwaka 2020 ili kuipa Serikali nafasi ya kufanya kazi. Huu ni uvunjaji wa Ibara ya 20 (1) ya Katiba. Aidha, katazo la mikutano ya siasa linakiuka Sheria namba 5 ya Vyama vya siasa ya mwaka 1992 kifungu cha 11 ambayo imetoa haki kwa vyama vya siasa kufanya kazi ya siasa.
2.2 Kupiga Marufuku Urushwaji wa moja kwa moja (live coverage) wa Mijadala ya Bunge: Katazo hilo ni kinyume na Katiba ibara ya 18 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatoa uhuru wa maoni na uhuru wa kupata habari kwa kila mwananchi.

2.3 Kudhibiti Wabunge wa Upinzani Bungeni: Serikali imejificha nyuma ya kiti cha Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb) ili kuwadhibiti Wabunge wa Upinzani Bungeni kwa lengo la kuwanyamazisha wasiikosoe Serikali.

Ikumbukwe kwamba Dkt. Tulia akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa ni mtumishi wa umma asiyepaswa kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa; lakini ghafla anaonekana akigombea nafasi ya Naibu Spika kupitia CCM. Hivyo yupo Naibu Spika ambaye ni mteule wa Rais. Swali: Anawajibika kwa nani kati ya Bunge na Rais?
 
Kuingilia Mhimili wa Mahakama: Serikali ya CCM kupitia Rais, kwa nyakati tofauti imeonekana kujaribu kuingilia uhuru wa Mahakama jambo ambalo ni hatari kwa utoaji wa haki nchini. Katika hotuba yake, wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria duniani Rais alinukuliwa akisema kwamba Mahakama iwahukumu harakaharaka watu waliokwepa kodi halafu atatumia asilimia fulani ya fedha ambazo zitakuwa zimepatikana kutokana na faini za wale walioshindwa kesi kuwapa Mahakama.
Muswada wa Sheria ya Haki ya kupata habari –Serikali imepeleka Bungeni Muswada wa Sheria ya Haki ya kupata habari. Sheria hii imeweka adhabu kubwa sana kwa waandishi kama vile kifungo cha miaka 15 na kisichozidi miaka 20 kwa mujibu wa kifungu cha 6(6)

Kupuuza Utawala wa Sheria: Tarehe 24 Juni, 2016 wakati wa uzinduzi wa siku ya usalama wa raia, Rais Magufuli alinukuliwa akiwaruhusu polisi kuwaua majambazi bila kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Aidha aliuagiza uongozi wa Jeshi la Polisi kuwapandisha vyeo watakaowauwa majambazi. 
Serikali hii inatishia ukuaji wa uchumi
Tangu serikali ilipoingia madarakani hali ya ukuaji wa uchumi na hata uwekezaji wa mitaji imekuwa ikiporomoka kwa kasi kubwa sana nchini mwetu na hata baadhi ya wawekezaji wanaondoa mitaji yao kutokana na serikali hii kukosa mwelekeo unaoeleweka wa Kiuchumi.
 
Serikali za mitaa kunyanganywa mapato na serikali kuu.
Baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 tulifanikiwa kushinda maeneo ya Majiji ya DSM, Mbeya,Arusha na Miji mikubwa ya Iringa, Moshi,Bukoba,Babati,Tunduma na mingineyo ya maeneo ya mijini ambayo kwa kiasi kikubwa wanategemea sana kuendesha Halimashauri hizo kwa kutumia kodi ya Majengo Kodi ya Majengo inachangia kati ya 30% hadi 60% ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Miji.

2.9 Diplomasia na mahusiano ya kimataifa

Hivi karibuni serikali imetoa maelekezo kupitia mawasiliano yake na Mabalozi (Note Verbale) kuelekeza kuwa kabla ya Mabalozi au maofisa wa Ubalozi kukutana na asasi zisizo za kiserikali au vyama vya siasa ni lazima kwanza waombe kibali cha serikali kupitia Wizara ya Mambo Nje.

Utaratibu huu unaminya uhuru wa mabalozi na wanadiplomasia mbalimbali kufanya kazi zao nchini na ni utaratibu ambao unakiuka utamaduni uliokuwepo awali na pia unakiuka masharti ya Mkataba wa Vienna kuhusu mahusiano ya Kibalozi Duniani.

2.10 Uteuzi wa Wakurugenzi wa Halimashauri

Uteuzi wa Rais wa Wakurugenzi wa Halimashauri na Makatibu Tawala wa Wilaya haukuzingatia sheria za utumishi wa umma na badala yake umezingatia kigezo cha Ukada zaidi badala ya weledi na historia katika utumishi wa umma kama ambavyo sheria zinataka, zaidi ya wakurugenzi 80 na Makatibu tawala zaidi ya 40 waligombea kura za maoni ndani ya CCM 2015.

2.11 ZANZIBAR

Kwa sababu ya hasira ya kukataliwa kwa CCM, vikosi vya ulinzi na hasa Jeshi la Polisi vimekuwa vikishiriki katika vitendo kadhaa vya ukiukwaji wa haki za raia huko Zanzibar ambapo kwa zaidi ya miezi miwili sasa, wamekuwa wakipita katika vijiji na kuwapiga, kuwatesa, kuwakamata, kuwatishia na hata kuharibu mali za wananchi na mifugo yao

Tunawataka wananchi wa Unguja na Pemba waendelee kuikataa Serikali haramu iliyopo madarakani huko Zanzibar kwa njia za amani .

3.0 MAAZIMIO YA KAMATI KUU

Baada ya majadiliano Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo;
Septemba 1, siku ya mikutano ya hadhara nchi nzima
Kamati kuu imeagiza ngazi zote za chama kuanzia ngazi ya msingi, Kata, Majimbo, Wilaya, Mikoa, Kanda, Mabaraza na Taifa kukaa vikao vyake vya kikatiba na imeelekeza ajenda ya vikao hivyo kuwa ni kujadili hali ya siasa, hali ya uchumi na maandalizi ya mikutano ya hadhara ya tarehe 01 Septemba, 2016 nchi nzima.
 
Wanasheria wa Chama kuchukua hatua
Kamati Kuu imewataka wanasheria wa chama kukaa na kuyatazama mambo yote ambayo yametokea na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuyatafutia suluhisho la kisheria.
 
OPERESHENI UKUTA
UMOJA WA KUPAMBANA NA UDIKTETA TANZANIA (UKUTA)

UTANGULIZI

Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika utangulizi kuna maneno yameandikwa na ambayo yamekaziwa na sheria namba 15 ya mwaka 1984 ibara ya 3 na sheria namba 1 ya mwaka 2005 ibara ya 3. Katika utangulizi huo wa katiba yetu imeandikwa kama ifuatayavyo;

“KWA KUWA Sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani” “NA KWA KUWA misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia, ambayo Serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi na pia yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu:”

“KWA HIYO, BASI, KATIBA HII IMETUNGWA NA BUNGE MAALUM LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA kwa niaba ya Wananchi kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya Demokrasia ujamaa na isiyokuwa na Dini”

Aidha kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzana ibara ya 3 (1) inasema kuwa “Jamhuri ya Muungano ni Nchi ya Kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”

Ni wazi sasa kuwa kuna tishio kubwa dhidi ya ukuaji wa Demokrasia hapa Nchini mwetu kutoka kwa viongozi wa serikali hii ya awamu ya tano kukandamiza Demokrasia na madhara ya kukandamizwa kwa demokrasia yameshaanza kulitafuna taifa letu.

Ni dhahiri kuwa kama raia wema tuna wajibu na haki ya kuilinda na kuitetea Katiba ya Nchi na kuhakikisha kuwa haivunji na yeyote na misingi ya Kidemokrasia ambayo ilijengwa kwa miongo mingi inaendelea kuimarika, kulelewa na kukuzwa mara dufu.

3. 4 KWANINI UKUTA NI MUHIMU !

Wakati wa Ufashisti wa Adolf Hitler huko Ujerumani unaanza kuchipua kabla ya kukomaa alianza kuchukua hatua mbalimbali za kuwanyamazisha Wajerumani kwa njia mbalimbali ili aweze kutawala kwa mkono wa Chuma.

Alikuwepo Mchungaji mmoja anayejulikana kwa jina la Martin Niemoller na ambaye alikuwa akimsemea Hitler kwa kila hatua ambazo alikuwa anachukua dhidi ya makundi mengine katika jamii ya wajerumani bila kujua kuwa lilikuwa ni suala la muda tu kabla hata yeye hajafikiwa na mkono wa Chuma wa Hitler.

Mchungaji huyu ni maarufu sana kwa msemo wake ambao aliutoa alipofikiwa na mkono wa Hitler ambao ulimpelekea kuishia jela kwa miaka 7 na wakati huo hapakuwa na

mtetezi wa kumsemea, alisema hivi;

First they came for the Socialists, and I did not speak out— Because I was not a Socialist. Then they came for the Trade Unionists, and I did not speak out— Because I was not a Trade Unionist. Then they came for the Jews, and I did not
speak out— Because I was not a Jew. Then they came for me—and there was no one left to speak for me.

3.5 HALI TANZANIA IKOJE?

Tangu utawala wa awamu ya Tano ulipoingia madarakani mwezi Novemba, 2015 umechukua hatua mbalimbali za kubinya Demokrasia na kuua dhana ya utawala bora kwa njia mbalimbali.

Yapo makundi ya kijamii ambayo tayari yameshaumizwa au kubinywa na watanzania walio wengi wanakaa kimya kwa sababu wao sio sehemu ya kundi husika ambalo limenyimwa haki au kwa kuwa hajafikiwa moja kwa moja.
  1. 3.6 KWANINI NI MUHIMU KUJENGA UKUTA.
  • Rais alipiga marufuku safari za nje kwa watumishi wa umma- sikusema kwa kuwa mimi sikuwa mtumishi wa umma
  • Rais aliitaka mahakama kuu iwahukumu wafanyabiashara ambao wana kesi za kodi na serikali lazima ishinde-sikusema kwa kuwa sikuwa mfanyabiashara na wala sikuwa na kesi ya kodi
  • Serikali iliingilia Bunge na kupanga kamati za kudumu za Bunge-sikusema kwa kuwa mimi sikuwa mjumbe
  • Serikali ilizuia matangazo ya Bunge live-sikusema kwa kuwa mimi sio Mbunge
  • Wabunge wa Upinzani kunyanyaswa Bungeni na kuonewa –sikusema kwa kuwa mimi sio UKAWA
  • Hotuba za Upinzani kufutwa Bungeni kinyume cha Kanuni za Bunge –sikuwa mpinzani nilikaa kimya Bunge kurejesha fedha zake kwa Rais kinyume cha sheria –sikusema kwa kuwa halinihusu
  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi kurejesha fedha kwa Rais kinyume cha sheria – sikusema kwa kuwa Tume hainihusu
  • Serikali Kuwafukuza na kuwadhalilisha wanafunzi wa UDOM –sikusema kwa kuwa sina ndugu wala mtoto anayesoma UDOM.
  • Mikutano ya kisiasa kupigwa Marufuku –sikusema kwa kuwa mimi sio mwanasiasa
  • Wafanyabiashara kupelekewa bili kubwa za kodi na hata kuzuiliwa kwa Akaunti zao-sikusema kwa kuwa mimi sio mfanyabiashara
  • Uchumi unaporomoka kwenye sekta zote nchini -sikusema kwa kuwa mimi sijawahi kumiliki uchumi
  • Fao la kujitoa limeondolewa kwenye Mifuko ya hifadhi ya jamii, sikusema kwa sababu mimi si mwanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
  • Mashirika na Makampuni kuanza kupunguza wafanyakazi kutokana na kuporomoka kwa uchumi –sikusema kwa kuwa sijapunguzwa kazini
  • Mabalozi na wanadiplomasia kuzuiliwa kukutana na viongozi wa kisiasa bila kibali cha serikali- sikusema kwa kuwa halinihusu
  • Watumishi wa umma kulazimishwa kwenda kinyume na sheria na kanuni za utumishi wa umma wametakiwa kuwa Makada wa CCM –sikusema kwa kuwa mimi sio mtumishi wa umma
  • Ukaguzi wa vyeti vya kidato cha nne na kutumika kama msingi wa kufukuza watu kazi hata kama ni Maprofesa –sikusema kwa kuwa hawajaja kwenye sekta yangu
  • Watumishi wa umma kutumbuliwa majipu bila kufuatwa kwa sheria na kanuni za utumishi wa umma –sikusema kwa kuwa mimi sikutumbuliwa
  • Mawakili kuunganishwa kwenye kesi za wateja wao wanapoenda kuwatetea – sikusema kwa kuwa mimi sio wakili
  • Waalimu kukatwa mishahara iwapo dawati litavunjika kwenye shule yake – sikusema kwa kuwa mimi sio mwalimu
  • Kupotezwa kwa wana CCM ambao watapinga kauli ya Mwenyekiti au kuwa na maoni tofauti-sikusema kwa kuwa mimi sio mjumbe wa vikao vya CCM .
  • Muswada wa sheria ya haki ya kupata habari na adhabu ya kifungo cha miaka 15-20- sikusema kwa kuwa mimi sio mwandishi wa habari
  • Viongozi wa dini kudhalilishwa –sikusema kwa kuwa mimi sio kiongozi wa dini
  • Unyanyasaji na udhalilishaji wa wananchi Zanzibar –sikusema kwa kuwa mimi sio mzanzibari
3.7 TUCHUKUE HATUA!

Kwa kuwa wewe tayari umeshafikiwa hauna budi kujenga UKUTA ili kuzuia wengine wasidhurike na utawala huu.
  1. Kwa kuwa wewe hujafikiwa na ndio maana husemi wenzako wanapofikiwa, njoo tujenge UKUTA ili ukifikiwa awepo wa kusema
  2. Tuungane Tujenge UKUTA ili kuzuia uchumi wetu kuporomoka
  3. Njoo Tujenge UKUTA kuzuia Udikteta huu
  4. Tujenge UKUTA tuilinde Katiba yetu
  5. UKUTA huu ni wa wananchi wote bila kujali dini, kabila, chama cha siasa au rangi
Historia inaonyesha kuwa Duniani pote Hakuna utawala uliwahi kuushinda UKUTA wa wananchi .Na hii ndio Nguvu ya Umma. Kila mmoja achukue hatua popote alipo ya kujenga UKUTA!

Imetolewa na;

…………………….

Freeman A Mbowe

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa

27 Julai, 2016

0 comments:

Post a Comment