Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) limesema lipo tayari kukabiliana na ugaidi nchini na
kwingineko barani Afrika.
Kwa wiki mbili mfululizo, askari wa JWTZ
waliungana na majeshi ya nchi nyingine nane kufanya mafunzo maalumu ya
kukabiliana na ugaidi, biashara ya dawa za kulevya, usafirishaji wa
binadamu na uharamia.
Akitoa tathmini, Mkurugenzi wa Mazoezi hayo,
Brigedia Jenerali Yohana Mabongo alisema yameenda vizuri na askari
wamepata fursa ya kufahamiana na kubadilishana uzoefu.
“Tupo vizuri.
Tunaweza kukabiliana na uhalifu wa kimataifa, ndani na nje ya Tanzania,”
alisema Brigedia Jenerali Mabongo.
Alifafanua kuwa awali askari walikuwa wanafanya kazi kiutamaduni wakiwa na lengo la kulinda mipaka kwa
kutumia silaha nzito, lakini kutokana na kubadilika kwa tishio la
usalama, majeshi mengi duniani yameona kuna haja ya kuwa na mbinu
mbadala.
“Kupambana na gaidi au mtuhumiwa wa dawa za kulevya hakuhitaji
kifaru au mzinga. Majanga yanayoletwa na mapigano au mashambulizi ya
kushtukiza huacha athari nyingi kwa jamii ambazo hustahili msaada.
"Tutayafanya hayo yote hapa nchini au popote Umoja wa Afrika (AU)
utakapoona kuna haja ya kufanya hivyo,” alisema.
Mafunzo hayo
yanayoshirikisha raia kutoka AU, Shirika la Kimataifa la Kuhudumia
Wakimbizi (UNHCR) na Shirika la Msalaba Mwekundu yanafadhiliwa na
Tanzania na Marekani.
Jana, Balozi mdogo wa Marekani nchini, Virginia
Blazer alitembelea Chuo cha Mafunzo ya Kuimarisha Amani Tanzania (TPC)
Kunduchi na kupokea ripoti ya utekelezaji.
Uganda, Djibouti na Ethiopia
ni miongoni mwa nchi zinazoshiriki mafunzo hayo.
Kwa muda mrefu,
Uganda inakabiliana na Joseph Kony anaeendesha mapigano ya kisasi kaskazini
mwa taifa hilo na alipoulizwa juu ya mchango wa mafunzo hayo, Kiongozi
wa askari wa Jeshi la Uganda (UPDF), Kanali Fred Twinamatsiko alisema
jeshi hilo lipo tayari wakati wote, lakini kuna changamoto za
kufanikisha suala hilo.
“Utayari wa kisiasa ndiyo unaokosekana. Mara
nyingi tumempiga Kony na kumuondoa alipokuwapo. Endapo wakubwa watakuwa
tayari, UPDF inamuondoa muda wowote,” alisema.
0 comments:
Post a Comment