SEMWANZA
Simba
tayari imekamilika katika mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi
Kuu Bara baada ya beki wa kati wa timu hiyo, Emmanuel Semwanza kurejea
kikosini katika kambi ya timu hiyo huko mkoani Morogoro.
Semwanza
aliyesajiliwa hivi karibuni akitokea Mwadui FC ya Shinyanga, alikuwa
mchezaji pekee wa timu hiyo ambaye hajajiunga na timu hiyo kutokana na
kufiwa na mama yake mzazi na hivyo kupata udhuru wa kuhudhuria mazishi
mkoani Mbeya.
Akizungumza
na Championi Jumatano, meneja wa timu hiyo, Abbas Ally, amesema kuwa
Semwanza amejiunga na kikosi hicho rasmi juzi baada ya kuwa nje ya
kikosi kwa takriban siku tano, hivyo sasa kikosi hicho kipo kamili
katika maandalizi yao chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog.
“Kambi
inaendelea vizuri, hakuna tatizo lolote zaidi amerejea Semwanza ambaye
yeye alikuwa nje ya kikosi kutokana na msiba, hivyo sasa kikosi
kimekamilika katika kuendelea na programu za mwalimu za kujiandaa na
msimu mpya wa ligi,” alisema Abbas.
Mpaka
mwisho wa wiki hii Simba itakuwa imetimiza wiki nne katika kambi hiyo
ikiendelea kujifua na kuwajaribu wachezaji wa kigeni waliopo kikosini
humo na kama wakifuzu waingie kandarasi za kuitumikia timu hiyo msimu
ujao, lengo likiwa ni kurekebisha makosa ya kutoshiriki michuano ya
kimataifa kwa misimu minne mfululizo.
0 comments:
Post a Comment