Thursday, 29 September 2016

#YALIYOJIRI>>>>Pato La Taifa Lakua Kwa Asilimia 7.9.Fahamu zaidi hapa.

Na Veronica Kazimoto

Pato la Taifa limekua kwa jumla ya thamani ya Shilingi trilioni 11.7 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2016 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 10.9 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema ukuaji wa pato la Taifa umetokana na shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, misitu na uvuvi ambapo shughuli  hizo zimekuwa  kwa asilimia 3.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 1.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

Kwa upande wa shughuli za uchumi za viwanda na ujenzi, Dkt. Chuwa alisema kumekua  na ongezeko la asilimia 20.5 katika kipindi hicho ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 11.2 mwaka 2015 katika shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto.

Aidha shughuli za uzalishaji bidhaa na viwanda zimeongeza kwa asilimia 9.1 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2016 ukilinganisha na kasi ya asilimia 5.2 ya mwaka 2015.

Shughuli za uchukuzi na uhifadhi, Dkt. Chuwa amesema kuwa shughuli hizo zimekua kwa kiwango cha asilimia 30.6 zikisababishwa  na usafirishaji wa abiria kwa njia ya reli na barabara ikiwa ni pamoja na usafiri wa UDART.

Vilevile, shughuli za fedha na bima zimeongezeka kwa kasi ya asilimia 12.5 ikilinganishwa na asilimia 10.0 iliyopatikana katika kipindi kama hicho mwaka 2015.

Dkt. Chuwa amefafanua kuwa  huduma za elimu zimekua kwa kasi ya asilimia 8.0 katika robo hiyo ya mwaka ikilinganishwa na aslimia 7.4 ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2015 ambapo ukuaji wa shughuli hii imetokana na ongezeko la wanafunzi waliodahiliwa mwaka 2016.

Kwa upande wa Nchi za Afrika Mashariki ambazo zimeshachambua na kutoa Pato la Taifa katika kipindi kinachoishia Juni 2016 ni Rwanda ambapo Pato halisi la Nchi ya Rwanda katika kipindi cha Aprili – Juni 2016 limeendelea kukua kwa asilimia 5.4 ikilinganisha na asilimia 7.2 ya miezi kama hiyo mwaka 2015.

Takwimu za Pato la Taifa kwa robo mwaka hupimwa kwa kutumia thamani ya bidhaa na huduma zilizozalishwa nchini katika vipindi vya miezi mitatu mitatu ambavyo ni Januari – Machi, Aprili – Juni, Julai – Septemba na Oktoba – Desemba ambapo hujumuisha shughuli zote za kiuchumi, na hutumika katika kutathmini, kupanga mipango na kutayarisha sera za kiuchumi.
MWISHO.

0 comments:

Post a Comment