Gazeti la Mwananchi la tarehe 23 Septemba, 2016 katika ukurasa wake wa Tano imeandikwa habari yenye kichwa cha habari “Harambee ya Profesa Muhongo yakusanya Sh 40,000 Bukoba”.
Mwandishi
wa Habari hiyo ameandika kuwa ziara aliyoifanya Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika Kata ya Hamugembe, Bukoba wakati
akikagua miundombinu ya umeme, iligeuka kuwa harambee baada ya
waathirika wa tetemeko la ardhi kudai msaada wa chakula na mahema.
Tunapenda
kuuarifu Umma wa Watanzania kuwa, siyo kweli kwamba Profesa Muhongo
aliitisha harambee ya kuchangia maafa hayo kama ilivyoandikwa na
Mwandishi ambaye kwa sababu zake binafsi aliamua kupindisha ukweli na
kueleza kuwa, “ilimlazimu Profesa Muhongo kuitisha mchango wa fedha
kutoka kwa maofisa aliokuwa ameambatana nao na kufanikiwa kupata
shilingi 40,000 na kuwakabidhi wakazi hao”.
Hivyo,
taarifa kuwa Profesa Muhongo aliitisha harambee ya kuchangisha fedha za
kusaidia waathirika wa maafa siyo sahihi kwani Profesa Muhongo hakuomba
wala kuagiza Maofisa alioambatana nao kuchangia fedha kama ambavyo
mwandishi anataka kuwaaminisha wananchi.
Akiwa
katika kata ya Hamugembe mkoani humo ambapo alikwenda kukagua nyumba
ambazo zimekatiwa huduma ya umeme kwa sababu ya kuathiriwa na tetemeko
hilo, baadhi ya wananchi walidai kuwa shida yao ni chakula na malazi, na
mmoja wa wananchi alisema kuwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera
aliyeambatana na Profesa Muhongo, alishafika kata hiyo na kuwasaidia
kiasi cha fedha.
Hata
hivyo, Profesa Muhongo aliwaeleza wananchi hao kuwa, yeye alikwenda
hapo kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kitaalam anayoyasimamia na
kwamba kilio chao kuhusu kucheleweshewa huduma atakifikisha kwenye
Kamati inayoshughulikia Maafa aliyokutana nayo tarehe 22 Septemba, 2016.
Baada
ya wananchi kumtaja Meneja wa TANESCO wa Mkoa Kagera aliyewahi
kuwasaidia wananchi hao fedha kutokana na tetemeko hilo, Meneja huyo
aliamua kuongeza kiasi cha Fedha na kumpa mmoja wa wananchi hao, tofauti
na ilivyoandikwa kwenye gazeti kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye
aliyekabidhi pesa kwa wananchi.
Tunawaasa waandishi wa habari kuzingatia ukweli na usahihi katika uandishi wa habari ili kupeleka habari sahihi kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment