Ujenzi
wa Daraja la Salender litakalounganisha eneo la Coco Beach na eneo Agha
Khan kupitia baharini Jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuanza Mwezi
Juni Mwakani baada ya Serikali ya Tanzania kukamilisha mchakato wa
upatikanaji wa fedha za ujenzi kutoka benki ya Exim ya Korea.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema hayo leo tarehe 22 Septemba, 2016 muda mfupi baada ya kufanya Mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais
Magufuli amesema ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa
kilometa 7 zikiwemo kilometa 1.4 zitakazopita baharini, unatarajiwa
kukamilika mwaka 2020 na daraja hilo litasaidia kupunguza adha ya
msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
"Mchakato
wa kulijenga hili daraja la Salender unaendelea vizuri kwa sababu hivi
sasa kampuni ya Kikorea ambayo inafanya usanifu ipo kwenye hatua za
mwisho na zabuni zinategemewa kutangazwa mwezi wa tatu Mwaka kesho na
zitakwenda haraka, kwa hiyo mambo yakienda vizuri ujenzi unaweza kuanza
mwezi wa sita, bahati nzuri fedha zote zipo na zimeshatolewa na Benki ya
Exim ya Korea" Amesema Rais Magufuli.
Aidha,
Dkt. Magufuli amemshukuru Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete kwa juhudi alizozifanya zilizowezesha kujengwa kwa
hospitali ya Mloganzila kwa ufadhili wa Jamhuri ya Korea na kwamba
hospitali hiyo itakuwa ya kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika
Mashariki.
Amesema
ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa
mwaka huu na kwamba tayari Madaktari na Wataalamu takribani 100
waliopata mafunzo nchini Korea na wenye ujuzi wa namna ya kutumia
teknolojia inayowekwa kwenye hospitali hiyo wapo hapa nchini.
Rais
Magufuli ambaye ameelezea nia ya Serikali ya Tanzania kufungua ofisi za
Ubalozi Mjini Seoul nchini Korea ameongeza kuwa Serikali yake
imedhamiria kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri
uliopo kati ya nchi hizi kwa lengo la kuwaletea manufaa wananchi ikiwemo
kutumia teknolojia na ujuzi wa nchi ya Korea katika ujenzi wa Meli.
Kwa
upande wake, Balozi wa Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young ametoa
salamu za pole kufuatia maafa ya tetemeko la Ardhi yaliyotokea Mkoani
Kagera na mikoa jirani, na ameahidi kuwa Korea itatuma timu ya wataalamu
kuja kuona namna ya kusaidia.
Balozi
Song Geum-Young pia amemhakikishia Rais Magufuli kuwa Korea itaendeleza
na kuimarisha uhusiano wake na Tanzania na kwamba itatoa ushirikiano wa
kutosha kufanikisha miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa hapa nchini
ikiwemo ujenzi wa Daraja la Salender, Meli, Hospitali ya Mloganzila na
mingineyo.
Wakati huo huo,
Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Balozi wa Urusi hapa
nchini Mhe. Yuri Popov ambapo viongozi hao wamekubaliana kuendelea
kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizo huku
wakitilia mkazo katika kukuza biashara na uwekezaji.
Pamoja
na hayo Balozi Yuri Popov amepongeza na kuelezea kufurahishwa na hatua
zinazochukuliwa na Rais Magufuli katika kuimarisha uchumi huku
akibainisha kuwa kwa hatua hizi anaamini ajenda ya kujenga uchumi wa
viwanda itafanikiwa.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea taarifa ya hali ya Maabara ya
Mkemia Mkuu wa Serikali na katika mazungumzo yake na Mkemia Mkuu wa
Serikali Prof. Samwel Manyele, amemtaka kuendelea kuimarisha utendaji
kazi wa maabara hiyo ili kuongeza ufanisi wa majukumu yake ambayo ni
kufanyia uchunguzi vielelezo vya makosa ya Jinai na usimamizi wa sheria
za udhibiti wa kemikali na udhibiti wa vinasaba vya binadamu (DNA).
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
22 Septemba, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na kumkaribisha Balozi wa Urusi hapa nchini Yuri Popov
aliyefika Ikulu kwa ajili ya mazungumzo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akisalimiana na Mkemia Mkuu wa Serikali Profesa Samwel Manyele Ikulu
jijini Dar es Salaam.
PICHA NA IKULU.
<<<<DOWNLOAD APPLICTION KWENYE SIMU YAKO HAPA>>>
0 comments:
Post a Comment