Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza
viongozi wote wa Serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za Kilele cha
Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba, 2016
katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale
ambao walishalipwa fedha ya posho na safari kwa ajili hiyo wazirejeshe.
Taarifa
iliyotolewa leo tarehe 12 Oktoba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli
ametoa maagizo hayo ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya
tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi
katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Viongozi
waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na
Wakuu wote wa Mikoa, Wakuu wote wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa Mamlaka
za Serikali za Mitaa, Mameya na Wenyeviti wote wa Halmashauri za Majiji,
Manispaa, Miji na Wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao
wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani
1,500.
Kwa
kuwa sherehe za Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na
Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki dunia miaka 17
iliyopita, agizo hilo limewataka Viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kubaki
katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi
siku hiyo.
Aidha,
Rais Magufuli ameagiza Wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika
shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao,
zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha Mbio za
Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa
utaratibu utakaoelekezwa na Mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.
Hata
hivyo Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa
Uhuru kwa Taifa, Viongozi wote wa Serikali ya Mkoa wa Simiyu na Wilaya
zake pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na
kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe
14 Oktoba, 2016.
Mgeni
Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Oktoba, 2016
0 comments:
Post a Comment