Friday, 17 July 2015

#YALIYOJIRI>>>Fomu za Ubunge, Udiwani sasa zauzwa shilingi milioni 5.




FOMU ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali nchini likiwemo Jimbo la Songea Mjini, mkoani Ruvuma na Babati mkoani Manyara, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imepandishwa kutoka kiwango cha Sh 100,000 kilichowekwa na chama hicho Taifa hadi kufikia Sh 5,000,000 kwa kila anayetaka kugombea nafasi hiyo katika jimbo.

Aidha, katika maeneo mbalimbali nchini, fomu za nafasi za madiwani zinazotakiwa kulipiwa sh. 10,000 hivi sasa wanaotaka kuteuliwa na chama hicho wanalipia kati ya shilingi 10,000 na 30,000.

Habari zaidi kutoka ndani ya CCM zinaeleza kuwa, fomu ya ubunge katika maeneo yote nchini zinatakiwa kulipiwa Sh. 100,000 na fomu ya udiwani ni Sh. 10,000 hali ambayo ni tofauti katika majimbo na kata hizo nchini.

Taarifa kutoka wilayani Babati mkoani Manyara, zinaeleza kuwa CCM inatoza wanachama wake kati ya shilingi milioni 2 na milioni 5 kwa watu wanaotaka kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.

Kuchukua fomu ya ubunge Jimbo la Dk Nchimbi sasa ni Sh. milioni 3.1 badala ya 100,000

Uchunguzi wa FikraPevu katika Jimbo la Songea mkoani Ruvuma imebaini kuwa fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika Jimbo la Songea Mjini, mkoani Ruvuma, kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imepanda kutoka kiwango cha Sh 100,000 kilichowekwa na chama hicho Taifa hadi kufikia Sh 3,100,000 kwa kila anayetaka kugombea nafasi hiyo katika jimbo hilo.

Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Juma Mperi, amethibitisha chama chake wilayani humo kuweka kiwango hicho cha gharama cha Sh milioni 3.1 kwa ajili ya kuchukulia fomu.

Kwa mujibu wa Mperi, kiasi hicho cha fedha, kinajumuisha gharama ya kuchukua fomu ambayo ni Sh 100,000 kama ilivyotangazwa na CCM Taifa, lakini kwa yeyote anayetaka kugombea jimbo hilo atalazimika kutoa kiasi kingine cha Sh 3,000,000 kwa ajili kulipia gharama za uchaguzi.

Ingawa Katibu huyo wa CCM hakuweza kufafanua gharama hizo za uchaguzi ni zipi, inaeleweka kwamba gharama hizo zinahusiana na mchakato wa kura za maoni, ambapo wajumbe wote wa mkutano mkuu wa jimbo hutakiwa kugharamiwa na chama katika jimbo husika, zikiwemo gharama za usafiri kutoka majumbani kwao hadi kwenye kituo cha kupigia kura za maoni kama zoezi hilo litafanyika katika kituo kimoja.
  • Kumbukumbu zinaonyesha kwamba siku chache zilizopita Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walitangaza kuwa fomu kwa wagombea urais zitatolewa kwa Sh1 milioni, ubunge Sh250,000 na udiwani Sh50,000.
  • Kwa upande wa Chama cha NCCR-Mageuzi kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu-Bara, John Nyambabe kimesema mgombea wa urais, atalazimika kulipa Sh1 milioni kwa nafasi hiyo na gharama za fomu za ubunge ni Sh50,000 na udiwani Sh20,000 huku kikieleza kuwa fedha zitakazopatikana kwa gharama za fomu zitatumika kusaidia shughuli za chama.
  • Ofisa Uchaguzi wa CUF, Lugoni Abdulrahaman,amesema mgombea urais atalazimika kulipia fomu Sh 500, 000 na tayari wabunge wamesharejesha fomu na kura za maoni zilianza Mei 20, 2015 ambapo wagombea hao walichukua fomu kwa Sh50,000, huku za udiwani zikiwa ni Sh20,000.
  • Chanzo ni 
  •                       (http://www.wavuti.com/)

0 comments:

Post a Comment