Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA vimetangaza rasmi kufikia makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Akitangaza makubaliano hayo mara baada ya kumalizika kwa kikao kirefu kilichokuwa kikijadili mustakabali wa kumpata mgombea urais pamoja na ugawanaji wa majimbo mapya, mwenyekiti mweza wa UKAWA James Mbatia amesema kuwa umoja huo umemteua mgombea ambaye ni chaguo la watanzania.
“Mgombea tutakayemtaja ndiye chaguo la watanzania” Amesema Mbatia
Mbatia amegoma kutaja jina la mgombea aliyepitishwa na umoja huo kwa madai ya anaandaliwa utambulisho maalum utakaoambatana na shamra shamra.
“Tayari jina tunalo lakini tutaliweka hadharani baada ya siku tano au sita hivi, na tutamtoa kwa kimasomaso”
Katika kikao hicho kilichomalizika majira ya saa 3:30 usku kikihusisha wenyeviti wa vyama hivyo pamoja na kamati ya ufundi ya UKAWA, mwenyekiti mwenza wa UKAWA kutoka chama cha wananchi CUF Prof Ibrahim Lipumba hakuweza kuhudhuria.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka CUF, chama hicho kilimuagiza Naibu Katibu Mkuu wa CUF Magdalena Sakaya kuiwakilisha, lakini baadaye Sakaya aliondoka katika kikao hicho bila maelezo yoyote.
Mkurugenzi wa mawasisliano wa chama hicho bwana Abdul Kamaya alipoulizwa kuhusiana na hilo akasema kuwa hakuna mwakilishi yeyote wa CUF aliyekuwepo kikaoni hapo hadi kikao hicho kikimalizika.
Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed alipoulizwa kuhusiana na kukosekana kwa Prof Lipumba kikaoni hapo amedai kuwa Prof Lipumba ni mgonjwa, na hali yake ya kiafya haimruhusu kuhudhuria kikao hicho.
“Mwenyekiti wetu ni mgonjwa, alikuwa safarini kutoka Kigoma, amerejea lakini hali yake si nzuri, ameshikwa na Malaria kali sana na miguu pia inamsumbua” Amesema Rajab Mbarouk.
Katika hatua nyingine, afisa habari wa CHADEMA Tumaini Makene aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari vyama hivyo vimekamilisha kazi ya kugawana majimbo mapya 26 kazi iliyofanyika leo katika kikao hicho.
Chanzo ITV Habari
0 comments:
Post a Comment