Wakati
Mwenyekiti wa CUF aliyefutiwa uanachama, Profesa Ibrahim Lipumba
akitangaza masharti kwa Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad ya kuingia
kwenye ofisi za chama hicho Buguruni, Dar es Salaam Chadema imetangaza
kutoshirikiana naye.
Akizungumza
kwenye makao makuu ya Chadema jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe aliwataka viongozi wa chama chake, kutotoa ushirikiano kwa Profesa
Lipumba, badala yake wampuuze na wamwone kuwa msaliti wa harakati za
kudai haki.
Wakati
akisema hayo, Profesa Lipumba akiwa katika Ofisi Kuu za CUF, alitoa
masharti kwa Seif kama anataka kufika ofisini hapo, kuwa lazima akiri
kumtambua na kumkubali kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho.
Mbowe
katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema Lipumba, Msajili wa
Vyama vya Siasa na taasisi ya utafiti ya Twaweza, ni mawakala wa
Serikali wa kuzia harakati za kupigania demokrasia nchini.
Alisema
harakati za kuzuia wapinzani kupigania haki, hazifanywi moja kwa moja
na Serikali, bali na wakala wao ambao wanakuja kwa sampuli mbalimbali.
“Kamati
Maalumu ya Kamati Kuu inatambua mgogoro ndani ya CUF, hivyo chama chetu
hakimtambui Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF wala Mwenyekiti
Mwenza wa Ukawa.
“Kamati
inalaani uamuzi wa Jaji Francis Mutungi wa kuivuruga CUF kwa kujaribu
kumrudisha madarakani Lipumba ambaye alijiuzulu katika mazingira
yanayoashiria kununuliwa na CCM, kwa lengo la kusaliti Ukawa kwenye
uchaguzi mkuu wa mwaka jana,” alituhumu.
Kuhusu
Jaji Mutungi, Mbowe alimtangaza kama adui wa demokrasia na vyama vingi
na kudai kuwa pamoja na kuwa Jaji, hana weledi wa kusimamia vyama vya
siasa.
Alitumia
nafasi hiyo kubainisha kuwa chama hicho hakina sababu hata moja ya
kumheshimu mtu kama Jaji Mutungi ambaye alisema anaonekana kutumika na
CCM.
“Mtu
ambaye tunamwona msomi, ambaye hapewi mamlaka yoyote ya kisheria ya
kuamua ndani ya vyama vya siasa, badala ya kusaidia vyama kumaliza
migogoro, amekuwa akichangia migogoro.
“Anaona vyama vinaminywa na Serikali anakaa kimya, lakini kila akizungumza anavikandamiza zaidi, huyu mtu ni adui mkubwa sana,” alisema.
Alimhakikishia
Jaji Mutungi kuwa mbinu zake za kudhoofisha vyama vya upinzani
hazitafanikiwa, kwani hakuwa Msajili wa kwanza, na kwamba matendo hayo
hayatafifisha vyama hivyo.
Kuhusu
Twaweza, alidai kuwa imekuwa ikilipwa na Serikali itangaze mambo
mbalimbali siku moja kabla ya Ukuta kwa kutoa takwimu alizoziita za
kipumbavu na kwamba wamekubali kujitwisha uendawazimu.
“Hawa
ni mawakala wa Serikali na wanajulikana. Ni Mtanzania mwendawazimu
pekee ambaye utamwambia kwamba hali ya nchi, Serikali inakubalika kwa
asilimia 96, lazima uwe mwendawazimu na utafiti huo hauwezi kulisaidia
Taifa,” alisema.
Wakati
Chadema ikitoa kauli hiyo, hali ya kisiasa ndani ya CUF ilizidi kuwa
mbaya kutokana na pande mbili zinazosigana kutunishiana misuli.
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari waliofika Ofisi Kuu zaCUF jana, Profesa
Lipumba alisema alipata taarifa kwamba Maalim Seif angefika ofisini hapo
juzi, hivyo alimsubiri ampangie kazi.
Alisema
kama Seif angefika, kabla ya kufanya kazi na Mwenyekiti jambo la kwanza
ingekuwa ni kumtambua kwa nafasi hiyo ambayo alivuliwa na kikao kisicho
halali.
“Ni
lazima akija hapa afanye kazi na Mwenyekiti na walinzi wetu
wanamfahamu, wasingemfanya chochote kwa kuwa ni kiongozi wao pia,” alisema na kuongeza:
‘’Huwezi
kuja ofisi za chama, halafu ukasema humtambui Mwenyekiti, analijua hilo
kwamba akija hapa ni lazima afanye hivyo, kwani anajua kikao kilichokaa
Zanzibar ni cha ujanjaujanja.’’
Profesa
Lipumba alisema ndiye kiongozi wa walinzi wote wa chama, hivyo wana
haki ya kumlinda wanavyotaka wao kwa maslahi ya chama.
Alisema
Maalim Seif anatakiwa kujiamini na kufika kwenye ofisi hiyo ili afanye
kazi na Mwenyekiti wake za kujenga chama na hakuna kikundi kilichokuwa
kimeandaliwa kufanya vurugu au kugombana na kiongozi huyo.
“Anaweza
akaja lakini hawezi kusema kuwa kuna kikundi, hawa ni walinzi
wanaomlinda tangu anagombea nafasi hiyo mwaka 2014, hatuna kikundi ni
Blue Guard na anapaswa kuwaheshimu na si kuwaita kikundi,’’ alisema Lipumba.
Alisema
hakuwa na taarifa rasmi ya ugeni wa Maalim Seif, bali alisikia kwenye
vyombo vya habari, kwamba atakuja na wabunge pamoja na wajumbe kutoka
Zanzibar, hivyo alikuwa anasubiri ujio wake kwa kuwa ana ofisi yake.
‘’Maalim
Seif ana ofisi hapa, yeye kuja ni jambo la kawaida, ila tangu nimeanza
kufanya shughuli za chama sijamwona ofisini, hana haja ya kutangaza
anaweza akaja ofisini kwa Mwenyekiti wake, apate miongozo ya kazi,’’ alisema.
Kuhusu
ujio wa wabunge na wajumbe wa Baraza Kuu alisema atawajulisha muda wa
kukutana, kwa kuwa hajawaita hawapaswi kufika katika ofisi hiyo kama
kikundi.
Habari
za ndani kutoka ofisi hizo, zilidai kuwa Lipumba alilala ndani ya ofisi
hizo usiku wa kuamkia jana pamoja kundi la wafuasi wake waliokuwa
wakihofia kwamba upande wa Maalim Seif ungefika usiku kuchukua ofisi
yao.
Mmoja
wa wafuasi wa Lipumba ambaye alikuwa katika ofisi hizo jana, alidai
baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo walikesha hapo kwa lengo la kumlinda
kwani alikuwa anafanya kazi zake.
‘’Lipumba
hakubaki ofisini kwa kuogopa kundi la Maalim Seif ila alikuwa akifanya
kazi zake kwa kuwa ni muda mrefu tangu ajiuzulu hakuwa ofisini hivyo
kazi zimezidi,’’ alisema.
Hata
hivyo, Lipumba alikana kulala ofisini bali alifika saa 1:45
asubuhi.Katika ofisi hizo magari ya Polisi yalikuwa hayakauki kuanzia
saa moja asubuhi huku Lipumba akieleza kwamba hakuomba msaada wala
ulinzi wowote wa Polisi, kwa kuwa alikuwa ofisini.
Juu ya taarifa kwamba Maalim Seif aliomba ulinzi Polisi, wamsindikize alisema ni jambo la ajabu.
‘’Ikiwa
kuna ukweli katika hilo nastaajabu, unaomba ulinzi kwenda ofisini
kwako, ina maana walinzi alionao wa Serikali na wana chama hawatoshi?’’ Alihoji Lipumba.
0 comments:
Post a Comment