Mamlaka
ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), imeifikisha Ofisi ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Taasisi ya Kudhibiti na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), kutokana na harufu ya rushwa kwenye
ununuzi.
Mwenyekiti
wa Bodi ya PPRA, Dk Matern Lumbaga, alisema hayo jana Dar es Salaam
alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ukaguzi wa Mamlaka hiyo,
kwenye ofisi, taasisi na mashirika ya umma 70 kati ya 506.
Kwa
mujibu wa Dk Lumbaga, katika ukaguzi huo wa kipindi cha mwaka wa fedha
2015/16, taasisi tisa za umma, ikiwamo Ofisi ya Bunge na wizara moja,
zilibainika kuwa na viashiria vya rushwa.
Taasisi
zingine mbali na Bunge ambazo nazo zimepelekwa Takukuru ni Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), Makumbusho ya Taifa, Halmashauri ya Jiji la
Dar es Salaam, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na Wakala wa Umeme
Vijijini (REA).
Zingine
ni Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Darts), Halmashauri
ya Wilaya ya Sikonge na Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
“Lengo
la ukaguzi huo ni kuangalia kama ununuzi ulizingatia matakwa ya Sheria
ya Ununuzi ya mwaka 2011 na mikataba ya ununuzi iliyoingia katika
kipindi hicho.
“Kati
ya taasisi za umma 506, ni taasisi 70 pekee ndizo zilifanyiwa ukaguzi
kati ya Aprili na Septemba, ambapo taasisi 15 zimewekwa kwenye kundi la
wizara, idara na wakala wa Serikali, mamlaka ya Serikali za Mitaa 25 na
mashirika ya umma 30,” alisema.
Alisema
pia mikataba 21,313 yenye thamani ya Sh trilioni 1.05 ilifanyiwa
ukaguzi na kati ya hiyo, 845 ilihusu kazi za ujenzi; 7,179 vifaa na
bidhaa; 103 ushauri wa kitaalamu; 3,083 ununuzi na mikataba na 453
makubaliano maalumu.
Dk
Lumbanga alisema uchambuzi wa matokeo hayo ulionesha kuwa taasisi 22
zilikidhi viwango, 38 kiwango cha kati na 10 kiwango kisichoridhisha
yaani chini ya asilimia
60.
Katika
ukaguzi huo, walibaini malipo tata ya Sh. bilioni 1.32 kutoka kwenye
taasisi nne kwenda kwa wakandarasi kwa kazi ambazo hazijafanyika.
Alitaja taasisi hizo kuwa ni Jiji la Dar es Salaam, Rea, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) na Mfuko wa Pensheni wa LAPF.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dk Laurent Shirima alisema wakati wowote Bodi ya
Wakurugenzi itaita wakuu wa taasisi zilizofanya vibaya, wajieleze kwa
nini wasichukuliwe hatua kutokana na uzembe na kuisababishia Serikali
hasara.
Alisema
pia kwa taasisi zilizopata chini ya asilimia 78, Mamlaka hiyo itaandaa
utaratibu wa kuwapa mafunzo ya uelewa wa matumizi ya Sheria ya Ununuzi
na kanuni zake.
“Ingekuwa rahisi kubaini upungufu iwapo taasisi zote zingewasilisha taarifa zao PPRA kwa wakati,” alisema.
0 comments:
Post a Comment