Tuesday, 11 October 2016

#MICHEZO>>>YANGA IMEVURUGWA, NAFASI YA UBINGWA INAKWENDA INAPOTEA TARATIBU TENA MAPEMA KABISA.FAHAMU ZAIDI HAPA.

Ukiangalia haraka haraka unaweza kuona kama kila kitu kinakwenda kawaida kabisa. Lakini kikosi cha Yanga, kinakwenda kinapotea nafasi ya kubeba ubingwa.

Taratibu, Yanga inakwenda inapoteza mwelekeo kutokana na mgogoro ambao unaonekana kuzidi kuibana na kuubana uongozi wake.

Wanachama wa Yanga waliafikiana kwa pamoja kuikodisha timu na nembo yao kwa miaka 10 kwa kampuni ya Yanga Yetu Ltd.

Mchakato ukafanyika kwa zaidi ya mwezi mmoja na baada ya hapo kupitia wadhamini wakasaini mkataba huo ili ukodishwaji uanze.

Wakati hayo yakiwa yamekamilika, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) likaibuka na kusema halitambui na kutaka utaratibu ufuatwe kwa madai limepata malalamiko.

BMT ilikuwa imelala, wakati mchakato ukiendelea baada ya Wanayanga kukubali, kila kitu kilifanyika hadharani lakini hawakusimama na kusema.

Hao waliopeleka malalamiko, ilikuwa lini? Vipi BMT ilikaa kimya muda wote hadi isubiri mkataba usainiwe ndiyo iseme?

Lakini TFF ambayo pia ilikuwemo na imekaa kimya, imeibuka leo na kusema kama ilivyotamka BMT. Huenda TFF imeona sasa baada ya kusikia BMT imetamka.

Jiulize pia, TFF walikuwa wapi, vitu viliendelea na kama Yanga walikutana haikuwa halali, hawakusema lolote na ukimya wao ni ishara ya hakukuwa na tatizo.

Vipi TFF inasema sasa, haikusema kabla ya BMT kusema? Hapa utagundua kuna tatizo.

Mgogoro huu unaweza kuonekana kama ni mdogo, lakini kwa unavyokwenda hakuna ubishi unakwenda kuiangusha Yanga kama timu na mwisho inapunguza zaidi nafasi yake ya kuwa bingwa tena au kufanya vizuri.

Huenda wanaotaka Yanga kutoingia kwenye mabadiliko hayo kwa visingizio kibao, wakashindwa kwa kuwa wanachama wenyewe wa Yanga zaidi ya asilimia 95 wanataka nafasi hiyo ya mabadiliko.

Lakini hadi inafikia wamekubaliana au wamewashinda wanaotaka kuwazuia, tayari watakuwa wamepoteza nguvu ya usimamizi au mwendo kwenye Ligi Kuu Bara.

Kama wapinzani wao Simba au Azam FC wakiwa makini, basi Yanga wataisoma namba na watalazimika kusubiri mwakani ili mambo yaende sawa.

Kingine ambacho kinawaangusha Yanga, ni suala la wao wenyewe kujichanganya kutokana na taarifa kwamba wanataka kumuacha Kocha Hans Pluijm.

Kumekuwa na taarifa walizungumza na kocha Mzambia. Uongozi ulifanya kazi ya kukanusha, lakini bado haiwezi ikawa imesaidia sana wakati wana mchezo mgumu kesho dhidi ya Mtibwa Sugar.

Yanga wanalazimika kufanya kazi ya ziada kutenganisha timu na haya yanayotokea. Ingawa kuna ugumu lakini wachezaji wanatakiwa kujengwa kisaikolojia zaidi ili warejee katika mwendo sahihi.

0 comments:

Post a Comment