Monday, 7 September 2015

Breaking News>>TANESCO imetangaza maeneo mengi Nchini yataingia gizani kwa siku saba kuanzia leo.Fahamu zaidi hapa.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kuwatangazia wateja wake walioungwa kwenye gridi ya taifa kote nchini kuwa majaribio ya Mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi 1 megawati 150 yanaendelea vizuri na sasa tupo kwenye hatua za mwisho za kuwasha mtambo huo.
Habari njema ni kwamba, gesi kutoka Mtwara imesukumwa na tayari imeshafika Kinyerezi Dar es Salaam. -Kazi ya kuunga bomba kubwa la gesi hiyo kwenye mitambo ya kufua umeme kwa gesi iliyopo Ubungo, itafanyika kuanzia Septemba 07 hadi Septemba 14, 2015.

Kazi hiyo italazimu kuzima mitambo ya kufua umeme kwa gesi iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam na hivyo kuathiri upatikanaji wa umeme kwa baadhi ya mikoa iliyoungwa kwenye gridi ya taifa.

Tunatarajia baada ya kazi hiyo kukamilika, umeme utaanza kurejea kwenye hali ya kawaida.

Uongozi unaendelea kuomba radhi wateja wake kwa usumbufu wowote uliojitokeza na utakaojitokeza.-

Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano TANESCO Makao Maku

BAADA ya kufika kwa gesi asilia jijini Dar es Salaam ikitokea Mtwara, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), itaingiza gesi hiyo katika mitambo yote ya umeme nchini, hivyo kuanzia leo kutakuwa na ukosefu wa umeme katika mikoa yote inayotumia Gridi ya Taifa.

Hatua hiyo inatokana na kuzimwa mitambo yote ya umeme katika kituo kikubwa cha kuzalisha umeme cha Ubungo, Dar es Salaam kwa nia ya kuingiza gesi asilia katika mitambo huo. Imeelezwa kuwa tatizo hilo la umeme, litadumu kwa wiki nzima ambao umeme utakatika kwa saa kadhaa usiku na mchana, lakini hali itakuwa mbaya zaidi kwa siku ya leo.

Akizungumza katika kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi One jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema mitambo yote ya umeme itazimwa ili kuingiza gesi asilia kuanza kuzalisha umeme katika kituo hicho kikubwa.

“Wiki hii umeme utakatika sana kutokana na kuunganishwa gesi kutoka Mtwara kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kuanzia kesho mitambo yote itazimwa,” alisema Mramba. Alisema kwa saa za mchana na usiku ndani ya wiki hii itakuwa mikoa yote inayotumia Gridi ya Taifa itakosa umeme.

Alisema baada ya majaribio ya kupitisha gesi asilia kukamilika sasa wanaingiza kwenye mitambo hiyo ili kuanza kuzalisha megawati 150 za umeme huku mitambo ya megawati 200 iliyokuwa haifanyi kazi kutokana na gesi kutotosha nayo itaanza kufanya kazi.

Alisema baada ya kuunganisha bomba hilo na umeme kuanza kuzalishwa mwishoni mwa wiki Watanzania watakuwa na uhakika wa umeme pamoja na bei ya umeme ya uhakika kwa muda mrefu.

“Kutokana na kuwa na gesi ya uhakika naamini mdhibiti ataangalia na bei inaweza kupungua ingawa siyo kesho au mapema,” alisema bosi huyo wa Tanesco.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Dk James Mataragio alisema kwa sasa mitambo ya Kinyerezi imejaa gesi na wameishaingiza gesi yenye mgandamizo wa tatu na inatakiwa kufika mgandamizo 50 hadi 51 ili kuzalisha umeme.

Alisema kwa muda wa wiki watakuwa wamefikisha mgandamizo huo kwa kuingiza polepole baada ya kufanya majaribio na kuona kuna uwezo wa kuingiza mgandamizo 90.

“Kuanzia kesho (leo) mpaka baada ya wiki mbili tutakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kwa gesi kwa kufikia mgandamizo huo wa 50,” alisisitiza na kuongeza kuwa uzalishaji huo, Serikali itaokoa dola bilioni moja zilizokuwa zikitumika kwa uzalishaji umeme wa mafuta.

Mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam ulikamilika Julai mwaka huu.

Awali gazeti mtandao la FikraPevu.com Agosti 22, 2015, liliripoti taarifa hii baada ya kupokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa watumiaji wa nishati hii.
 
SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco), limesema suala la kukatika mara kwa mara kwa umeme unatokea nchini hakutokani na kuwepo kwa mgawo wa nishati hiyo, bali kunasababishwa na hatua ya Shirika hilo kuanza majaribio ya uzalishaji umeme katika Mradi wa Kinyerezi namba moja wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150 kwa kutumia gesi asilia unaoingizwa kwenye Gridi ya Taifa, FikraPevu
imejulishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchismi Mramba, amesema shirika hilo lipo kwenye hatua za mwisho za majaribio ya kuwasha mitambo hiyo ya gesi asilia kupitia mitambo hiyo ya Kinyerezi namba moja.

Kwa mujibu wa Mramba katika mitambo minne iliyopo katika mradi huo, mitambo miwili hadi sasa imekwishakuanza kazi ya kuzalisha umeme, huku mingine miwili ikitarajiwa kuwashwa ndani ya muda wa wiki tatu zijazo, kwa maana ya Septemba, mwaka huu.

Mramba ameiambia FikraPevu kuwa wakati wa kufanya majaribio hayo, inawalazimu Tanesco kuzima mitambo iliyoko kwenye baadhi ya vituo vya kusambazia umeme, hali inayosababisha baadhi ya maeneo nchini kukosa umeme kwa takribani saa tatu hadi tano kwa siku.
Mwonekano wa kituo cha kuzalisha umeme wa gesi Kinyerezi
 Mradi huo wa Kinyelezi namba moja, umeanza kupokea gesi asilia inayotoka Mtwara kupitia mabomba ya gesi, kwa kuungana na mabomba mengine ya gesi kutoka Songosogo. Mradi huo kwa sasa una uwezo wa kuzalisha megawati 150 za umeme unaoingizwa moja kwa moja katika Gridi ya Taifa.

Aidha, mradi huo unaojumuisha ujenzi wa njia za umeme za msongo wa 220Kv kutoka Kinyerezi hadi Kimara pamoja na njia ya kutoka Kinyerezi hadi Gongolamboto yenye msongo wa 132Kv. Utekelezaji wa mradi huo ulianza Januari, 2013, na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Agosti, 2015.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, ameihakikishia FikraPevu kwamba hali ya umeme itaimarika zaidi nchini mara baada ya mradi huo wa Kinyerezi kukamilika rasmi mapema mwezi ujao.

Bei ya umeme kushuka

Waziri huyo, amewapa matumaini Watanzania akisema baada ya mitambo yote minne ya mradi huo kuwashwa na kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, bei ya umeme nchini kwa uniti moja itashuka ikilinganishwa na bei ya sasa kwa kuwa umeme unaozalishwa kwa kutumia gesi asilia utakuwa na gharama nafuu katika uzalishaji wake, ikilinganishwa na uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta.
Kituo cha kuzalisha umeme wa gesi cha Kinyerezi namba moja
   Kutokana na hali hiyo, Simbachamwene alisema wizara yake imeanza mchakato wa kukutana na Mamalaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ili kuangalia namna ya kuweza kupunguza bei hiyo ya umeme ili kuwaletea nafuu wananchi.

Kabla ya ufafanuzi huo wa Tanesco kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya watumiaji umeme nchini, wakilalamikia hali hiyo ya Tanesco kukata umeme wake hovyo, wakati mwingine bila kuwataarifu wateja wake.

Siku chache zilizopita gazeti hili mtandao la FikraPevu liliripoti taarifa iliyohusu kero ya kukatika umeme ambako kulielezwa

kuwachosha wakazi wa mikoa mingi nchini na kuwafanya kulilalamikia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuwa kitendo hicho cha kukata umeme nyakati za asubuhi, mchana na usiku kimesababisha kuibuka kwa kasi ya kuungua vifaa vinavyotumia nishati hiyo.

0 comments:

Post a Comment