Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli jana
tarehe 15 Agosti, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Mbunge na
aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mhe. Ichiro Aisawa Ikulu
Jijini Dar es Salaam.
Katika
Mazungumzo hayo Mhe. Ichiro Aisawa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa
uongozi mzuri, kupambana na rushwa na msukumo mkubwa anaoutoa katika
maendeleo, juhudi ambazo zinasaidia kuimarisha uchumi na kuboresha
huduma za kijamii.
Mhe.
Ichiro Aisawa ambaye ametembelea baadhi ya miradi inayojengwa hapa
nchini na kampuni za Japan ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara za juu
(Flyover) wa TAZARA na Mradi wa kuzalishaji umeme kwa gesi wa Kinyerezi
amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa kampuni hizo zitafanya kazi nzuri
na zitakamilisha kazi kama ilivyopangwa.
Pia
Mhe. Ichiro Aisawa amesema baada ya kuona changamoto ya foleni katika
Jiji la Dar es Salaam amebaini kuwa nchi yake bado inahitaji kuendelea
kushirikiana na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya Jiji la Dar es
Salaam na ameahidi kufikisha ujumbe huo kwa Waziri Mkuu wa Japan Mhe.
Shinzo Abe.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Ichiro Aisawa kwa kuja
Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa ambao
Japan inautoa katika maendeleo, na itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano
na ushirikiano wake na Japan katika masuala mbalimbali.
Mhe.
Rais Magufuli ameishukuru Japan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza
miradi mikubwa ya ujenzi Jijini Dar es Salaam ikiwemo upanuzi wa
barabara ya Mwenge – Morocco utakaoiwezesha barabara hiyo kuwa na zaidi
ya njia nane, ujenzi wa barabara ya TAZARA, ujenzi wa Daraja la Gerezani
njia nne, na barabara ya Bendera tatu hadi Kamata.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Ichiro Aisawa ambaye ni mwakilishi wa
wabunge wa Japan wanaoshughulikia masuala ya Afrika kuwahamasisha
wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Japan kuja kuwekeza hapa nchini na
ameahidi kuwa Serikali itahakikisha uwekezaji wao unalindwa kama
itakavyofanya kwa kampuni ya kutengeneza rangi ya Kansai Plascon ambayo
awali ilijulikana kama Sadolin, na kampuni inayozalisha Betri za
Panasonic hapa nchini, ili uwekezaji huo ulete manufaa hapa nchini.
“Naomba
unifikishie ujumbe kwa Waziri Mkuu Shinzo Abe kuwa Tanzania inamshukuru
kwa ushirikiano huu mkubwa, tunamkaribisha sana Tanzania na kwa kuwa
Serikali yetu imehamia Dodoma tutafurahi sana kama Japan itaweka alamu
ya urafiki wetu kwa kutujengea barabara za Dodoma mjini, iwe ni flyover
au kilometa 20 za barabara, sawa tu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment