De Gea, Van Gaal hapakaliki
*Terry tumbo joto, Chelsea wamtaka Varane
*Wenger anaendelea kutafuta mshambuliaji
Uhusiano
wa kipa wa Manchester United, David de Gea na kocha wake, Louis van
Gaal unaelezewa kuharibika ka kiasi kikubwa kutokana na kocha huyo
kumtupa nje ya kikosi chake.
De Gea ametazama mechi zote
za tatu za United akiwa jukwaani na hakupewa hata nafasi ya kuwa na
wachezaji wa akiba, maelezo yanayotolewa na kocha yakiwa kwamba hawezi
kujituma kwa sababu anafikiria mambo ya Real Madrid.
Wakati
Mhispania huyo akitaka kurudi kwao anakotakiwa na Real, United wanasema
kwamba hawatamuuza mchezaji huyo licha ya kubakisha msimu mmoja tu
kiasi kwamba anaweza kuondoka kama mchezaji huru kiangazi kijacho.
De
Gea anaona kwamba hali ilivyo klabuni hapo itakuwa ngumu kufanya kazi
na kocha huyo ambaye alimwekea maneno mdomoni kwamba alisema hataki
kucheza mechi mbili za kwanza ilhali alikuwa na kiu ya kurejea langoni.
Chanzo
cha habari kilicho karibu na De Gea kimenukuliwa kikisema: “David
haelewani tena kabisa na Van Gaal – uhusiano wake na kipa wa makocha,
Frans Hoek ndio umetibuka kabisa.” Van Gaal alidai kwamba De Gea
alimwambia kocha huyo wa makipa kwamba hakuwa na shauku ya kucheza,
ndipo wakaamua kumpumzisha na nafasi yake kuchukuliwa na Sergio Romero.
Pia
Victor Valdes aliyesajiliwa akiwa mchezaji huru naye ni kana kwamba
ametupiwa virago na hutazama mechi akiwa jukwaani, baada ya kumchefua
Van Gaal kwa kukataa kufanya mazoezi na kikosi cha pili. Alimwambia
anaweza kuondoka, na anasubiri timu ya kumnunua, lakini ana mkataba
mnono hapo, hivyo anakaa bure.
Zipo habari kwamba Pedro
Rodriguez aliyekuwa ajiunge na Man United kutoka Barcelona alibadilisha
mawazo baada ya kushauriwa ama abaki Camp Nou au aende klabu nyingine ya
Ligi Kuu ya England, kwani Van Gaal angeweza kumharibia maisha kutokana
na hasira na ukali wake.
Kipa wa zamani wa Manchester
United, Edwin van der Sar, ambaye sasa ni mmoja wa wakurugenzi wa Ajax
ya Uholanzi anasema anafahamu fika sintofahamu iliyoibuka baina ya kocha
na mchezaji huyo na alikuwa na haya ya kusema kumhusu:
“Ni
wazi kwamba kuna mengine mengi zaidi yanaendelea chini chini; kuna kitu
kati ya Louis na De Gea. “Nina wasiwasi kwamba De Gea atakuwa na
kipindi kigumu sana cha miezi 10 ijayo. Nikiwa mwajiriwa na kipa wa
zamani wa klabu hiyo, nahisi ni kitu cha kuogofya kuona makipa wazuri
watatu – De Gea, Anders Lindegaard na Victor Valdes – wakiwa jukwaani
wakiangalia mpira wa Man United.
“Huyo Sergio Romero
alikuwa mchezaji huru ambaye hajacheza mechi ya ligi kiushindani hasa
katika miaka miwili, lakini ndiye anapewa nafasi ya kwanza. Jina la
Cillessen linatajwa kama mtu wa kuchukua nafasi ya De Gea, lakini nikiwa
mkurugenzi hapa Ajax, najitahidi kuhakikisha kwamba mchezaji wetu bora
zaidi anabaki.”
Nahodha wa Chelsea, John Terry, 34, anahofia hatima yake ndani ya
klabu hiyo, baada ya kusikia tetesi kwamba kocha Jose Mourinho
anafikiria kumsajili beki wa kati wa Real Madrid, Raphael Varane, 22.
Mourinho
alimwondosha Terrywakati wa mapumziko kwenye kikosi chake
kilichofungwa na Manchester City 3-0, badala yake akamwingiza Kourt
Zouma, na juzi alimtaja kuwa mmoja wa wachezaji sita waandamizi
waliochemsha msimu huu.
Chelsea wameshapeleka dau mara
tatu Everton kwa ajili ya kumsajili beki wa kati, John Stones, lakini
pia wametuma barua Real Madrid kuhoji uwezekano wa kumsajili Varane
kiangazi hiki. Varane amekuwa kipaumbele cha Mourinho lakini Madrid
hawaelekei kumuachia.
Terry amekuwa akijifua zaidi,
akiamini kwamba anaweza bado kuwika kama msimu uliopita, ambapo alicheza
dakika zote za mechi zote za ligi kuu. Makocha waliomtangulia Mourinho,
Rafa Benitez na Andre Villas-Boas walikuwa wakimtupa benchi Terry.
Karim Benzema, inasemekana yuko njiani kwenda Arsenal. |
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema uchache wa washambuliaji
mahiri wenye viwango vikubwa kimataifa na klabu zenye wachezaji wa aina
hiyo kutotaka kuwauza kunawafanya Arsenal kushindwa kusajili jina kubwa
hadi sasa.
Hata hivyo, amesema uwapo wa vipaji vingi, hasa
katika klabu za Barcelona na Real Madrid kiasi cha kutoa ushindani wa
namba kwa wachezaji kunaweza kuwanufaisha Arsenal, kama ilivyotokea kwa
kuwapata Alexis Sanchez kutoka Barca na Mesut Ozil kutoka Real, na sasa
wote wana umri wa miaka 26.
Pamekuwapo habari kwamba
Arsenal wanataka kumsajili mshambuliaji wa kati wa Real Madrid, Mfaransa
Karim Benzema, ambapo baadhi walidai dili lingekamilika wiki iliyopita,
wengine wakisema huenda mwanzoni mwa wiki hii, lakini hadi sasa ni
kimya.
Zilikuwapo taarifa pia kwamba Arsenal walikuwa
wakiulizia uwezekano wa kumpata Edinson Cavani wa Paris Saint-Germain
(PSG) au hata mshambuliaji mwenzake, Zlatan Ibrahimovic aliyesema
angeushangaza ulimwengu juu ya klabu atakayohamia.
Alipata
kukaribia kucheza Arsenal miaka kadhaa iliyopita, akafanya nao mazoezi
akiwa tayari ameshapewa jezi, lakini akatimka baada ya Wenger kumtaka
aingie kwenye majaribio halisi kama angefaa, Ibrahimovic akasema yeye si
mtu wa maonesho bali alikuwa ameenda kucheza moja kwa moja.
Mkongwe
wa Arsenal, Ray Parlour ameunga mkono majaribio ya kuwasajili Benzema
na Cavani, japokuwa jitihada zikifanyika uwezekano kwa Arsenal ni kupata
mmoja wao tu.
Toa maoni yako hapa.
0 comments:
Post a Comment