Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga,(kulia) akizungumza katika hafla hiyo ya kusaini hati ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Filiberto Sebregondi, akisaini Hati
ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya
(EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, naye akisaini Hati hiyo.
Zoezi la kusaini likiendelea.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania, Mhe. Filiberto Sebregondi, wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Hati hiyo ya makubaliano imesainiwa leo, 28-08-2015, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo.
Bi. Mindi Kasiga akiwatambulisha waandishi wa Habari, waliohudhuria hafla hiyo (hawapo pichani).
Katibu Mkuu,Balozi Mulamula akisisitiza jambo, huku Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, wakifuatilia kwa makini mazungumzo hayo.
Umoja
wa Ulaya (EU) utatuma timu ya waangalizi yenye wajumbe 128 nchi nzima
katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
Hayo
yalibainishwa wakati wa uwekaji saini wa Makubaliano ya awali ya
kuruhusu timu hiyo kati ya EU na Serikali ya Tanzania uliofanyika kwenye
Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tarehe 28
Agosti 2015.
Uwekaji
saini huo umefanywa na Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu wa Wizara
ya Mambo ya Nje kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kwa upande wa EU
ulifanywa na Mhe. Filiberto Ceriani Sebregondi, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania.
Akizungumza
baada ya uwekaji saini wa Makubaliano hayo, Balozi Sebregondi alieleza
kuwa EU imekuwa ikituma timu hiyo kwa nchi washirika ambazo zina
historia nzuri ya demokrasia. Aidha, nchi hizo zina dhamira ya dhati ya
kukuza mahusiano na EU kwa kuruhusu waangalizi wafanye majukumu yao
katika hatua zote za uchaguzi kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa uchaguzi
unakuwa wa haki na huru.
Balozi
Sebregondi aliendelea kueleza kuwa timu kama hiyo ambayo wajumbe wake
wanakuwa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya, ilitumwa katika uchaguzi wa
mwaka 2010 ambapo iliutangaza kuwa ni huru na haki. Timu pia ilitoa
ushauri na maelekezo ya namna ya kufanya maboresho katika hatua
mbalimbali za uchaguzi.
Kwa upande wake, Balozi Mulamula aliikaribisha timu hiyo kuja Tanzania
na alisema kuwa jukumu la Wizara yake ni kuratibu na kuhakikisha kuwa
wajumbe wa timu hiyo wanatekeleza majukumu yao kama ilivyokubalika
kwenye Makubaliano ya Kimataifa. Aliongeza kuwa maelezo ya undani wa
shughuli ya timu hiyo wakati wa uchaguzi yatatolewa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, ambao pia watasaini makubaliano ya utekelezaji wa kazi ya timu
hiyo.
Taasisi
zingine za Kimataifa zinazotarajiwa kutuma timu za uangalizi wakati wa
Uchaguzi Mkuu wa 2015 ni pamoja na Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC) na Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).
Toa maoni yako hapa.
0 comments:
Post a Comment