SASA Yanga kumekucha. Baada ya kumaliza pilikapilika za kushangilia
ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa klabu hiyo inataka kuanza kazi
ya kuunda kikosi kipya kwa ajili ya msimu ujao.
Kamati ya Utendaji wa Yanga imeunda kabineti ya watu watano na
kuwakabidhi Sh bilioni 2 kwa ajili ya kufanya mazungumzo na nyota wao
wanaomaliza mikataba mipya na kufanya usajili ili kuongeza nguvu kwenye
kikosi chao.
Mwenyekiti wa kabineti hiyo ni Hussein Nyika, makamu wake ni Mustapha
Ulungo, huku wajumbe wakiwa ni Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa na
kocha wa klabu hiyo, George Lwandamina.
Moja ya majukumu yatakayowakabili ni kuhakikisha wananasa saini za
wachezaji wanaotajwa kuwaniwa na klabu hiyo, ambao ni Salmin Hoza,
Yusuph Ndikumana, Mbaraka Yusuph, Jamal Mwambeleko, Michael Gradiel,
Raphael Daudi, Mrisho Ngassa, Youth Rostard, Said Ndemla, Ibrahim Ajib
na Jonas Mkude.
Ili kupata nafasi ya kuwasajili wachezaji hao, klabu hiyo imepanga
kuacha nyota wao 15, ambao hawakuwa na nafasi katika kikosi hicho na
kusuka upya timu kwa ajili ya msimu ujao.
“Kamati imeazimia kusajili wachezaji wengi vijana ambao wana uwezo na
wenye ubora wa kucheza Yanga na kuwaacha wachezaji 15 ambao walikuwa
hawana nafasi ya kucheza, wamedhamiria kujenga timu imara yenye hadhi na
mashindano ya kimataifa, ndiyo maana wametenga fungu hilo la fedha,”
alisema mjumbe huyo.
Aliongeza kuwa, mbali na kufanya usajili huo wa nguvu, lakini kamati
hiyo leo inatarajia kuanza mazungumzo na wachezaji Deus Kaseke, Donald
Ngoma, Amis Tambwe, Haji Mwinyi, Thaban Kamusoko, Vincent Bossou na
wengine ambao mikataba yao ya kuichezea timu hiyo imemalizika hivi
karibuni na kupendekezwa na Kocha Lwandamina kuendelea kuwa nao.
Mmoja wa wajumbe wa kabineti hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake,
alisema: “Kesho (leo) Jumatatu tutaanza kazi ya kuzungumza na wachezaji
wote ambao walimalizia mikataba yao, ambao wamependekezwa kubaki na
kocha Lwandamina, baada ya hapo itakuja zamu ya wachezaji wapya ambao
watakuwa wameorodheshwa kwenye ripoti ya kocha wetu.”
Kwa upande wake Mkwasa, alisema Yanga ni timu kubwa na wamejipanga
kufanya usajili wa nguvu wenye tija utakaowezesha kutetea ubingwa wao
msimu ujao.
“Tumejipanga kila eneo ili kufanya usajili wa nguvu wenye tija ambao
utazingatia vigezo vyote na mimi ndio nitaongoza jahazi hilo,” alisema
Mkwasa.
Katika mipango yao ya usajili, Yanga wanadai kuwa na mpango na kuanza na
beki wa kushoto wa Azam, Gadiel Michael, ili kucheza pamoja na Haji
Mwinyi kwenye klabu hiyo.
Naye kiungo wa zamani wa timu hiyo, Athumani Idd ‘Chuji’, ameomba
kurejea tena kundini kuvaa viatu vya Justine Zullu ‘Mkata Umeme’ na
kusema uwezo wa kuitumikia timu hiyo ya Jangwani bado anao kama akipewa
nafasi katika eneo la kiungo mkabaji.
“Nimeiangalia Yanga msimu uliomalizika, nimegundua bado ninao uwezo
mkubwa wa kuichezea timu hiyo pamoja na umri wangu wa miaka 29, bila
shaka ninaweza kulitibu tatizo la kiungo mkabaji ambalo limekuwa
likiwasumbua Yanga kwa muda mrefu,” alisema ‘Pass Master’ huyo, Chuji.
Akizungumza kuhusiana na ombi hilo la Chuji kutaka kurejea tena Yanga,
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Paulo Malume, alisema
amelisikia suala hilo na atalipeleka mahali husika kwa ajili ya
kulitolea maamuzi, lakini yeye hawezi kusema lolote.
“Nimelisikia suala la mchezaji huyo, kwa kifupi nitalipeleka mahala
husika tuone nini watasema, kila mtu anamfahamu Chuji alikuwa ni
mchezaji wetu, lakini muda mrefu umepita tangu aondoke, hivyo ngoja
tuone watasemaje,” alisema Malume.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment