WINGA aliyekipiga Mbeya City msimu uliopita, Mrisho Ngassa, amerejea
kwenye klabu yake ya zamani ya Yanga na leo amejumuishwa kwenye kikosi
hicho kilichocheza na Tusker kwenye michuano ya Super Cup, katika Uwanja
wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Ngassa, ambaye mkataba wake na Mbeya City umemalizika baada ya msimu wa
Ligi Kuu Tanzania Bara, ameonekana akifanya mazoezi na kikosi cha klabu
hiyo ya Jangwani katika Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es
Salaam.
Taarifa ambazo BINGWA imezinasa jana kwenye mazoezi hayo, ni kwamba
Ngassa ameagizwa kujiweka fiti ili kuangaliwa uwezekano wa kusajiliwa
kwa ajili ya msimu ujao.
“Ngassa ameomba kurejea Yanga na benchi la ufundi kupitia uongozi
limempa masharti ya kuhakikisha anajifua na kurejesha kiwango chake ili
waangalie uwezekano wa kumpa mkataba,” kilisema chanzo hicho.
Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema michuano hiyo haimzuii
mchezaji kutoka timu nyingine kushiriki, bali kikubwa ni kufuata kanuni
zao walizoweka.
“Kwa sasa Ngassa yupo na timu yetu akifanya mazoezi na ikibidi anaweza
kutumika pia katika michuano hiyo, suala la kumsajili itategemeana na
mapendekezo ya kocha, akimhitaji tutampa mkataba,” alisema Mkwasa.
Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, amesema anachofahamu yeye kuhusu
Ngassa ni kwamba amekwenda Yanga kwa ajili ya kufanya mazoezi ili
ajiweke fiti na wapo wengine wengi.
“Siyo Ngassa pekee anayefanya mazoezi na Yanga, wapo wachezaji wengi
ambao huwezi kuwazuia wala kuwauliza wamefuata nini, kwani kazi yangu ni
kufundisha, jukumu la kuuliza nani yupo kwa sababu gani ni la uongozi
wa juu,” alisema.
Mbali na Ngassa, wachezaji wengine waliojiunga na kikosi hicho kwenye
mazoezi ya kujiandaa na michuano hiyo ya Super Cup ni Babu Ally wa
Kagera Sugar, Zahora Pazi (Mbeya City), Haruna Chanongo aliyecheza
Mtibwa Sugar msimu uliopita, Emmanuel Kichiba na mshambuliaji mmoja wa
Ghana.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment