Mwanahabari nguli Jenerali Ulimwengu, leo anatarajia kuwasilisha
maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akiomba kuungana na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika kesi ya katiba
iliyofunguliwa hivi karibuni.
Ulimwengu anaomba kuunganishwa katika kesi ya katiba namba 1 ya
2017 kama mdai dhidi ya wadaiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam
na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
“Maombi ya kumuunganisha yameandaliwa na kesho(leo) yatakuwa
mahakamani kuomba naye awe mdai. Anaomba kujiunga kwa kuwa mambo
anayopigania Mbowe naye ana maslahi nayo kwa sababu ni mambo muhimu ya
katiba,” alisema mmoja wa jopo la Mawakili kutoka Kurugenzi ya Katiba Sheria na Haki za Binadamu ya Chadema, Peter Kibatala.
Katika kesi hiyo ya katiba, Mbowe anaomba Mahakama Kuu itamke kuwa Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kudhalilisha na kukamata.
Mbowe pia anaomba mahakama itengue vifungu vya 5 &7 vya Sheria
ya Tawala za Mitaa kwa kuwa ni batili na vinakiuka haki ya katiba.
Mbowe alifungua kesi hiyo akidai Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda amekiuka sheria na taratibu katika kushughulikia watuhumiwa
wa biashara ya dawa za kulevya nchini.
Kesi hiyo ya katiba inasikilizwa na majaji watatu, Jaji Sakieti Kihiyo, Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Khaday.
Baada ya kufungua kesi hiyo Mbowe pia aliomba mahakama itoe amri
asikamatwe mpaka maombi yake ya zuio yatakaposikilizwa na kutolewa
uamuzi.
Mahakama ilitoa zuio la muda kwa Jeshi la Polisi kutomkamata Mbowe
hadi maombi yake ya kupinga kukamatwa aliyowasilisha mahakamani
yatakaposikilizwa.
Maombi hayo yalitakiwa kusikilizwa mwishoni mwa wiki lakini upande
wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Gabriel Malata uliwasilisha
pingamizi, ukiomba mahakama iyatupilie mbali kwa sababu hana msingi
katika sheria.
Upande wa mdai ulijibu hoja za kupinga maombi yao na Mahakama
ilisikiliza hoja za pande zote mbili na kupanga kutoa uamuzi wa
pingamizi hilo Machi 2, mwaka huu.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment