Mbunge
wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni mtoto wa rais mstaafu,
Dkt. Jakaya Kikwete ameeleza uhusiano uliopo kati ya baba yake na Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa bado ni maswahiba.
Ridhiwani
ametoa ufafanuzi huo kutokana na imani iliyojengeka kuwa kuna uhasama
kati ya Dkt. Kikwete na Lowassa ambao awali walikuwa maswahiba wakubwa
kabla ya siasa kuingiza doa kwenye uhusiano huo.
Uhasama
huo uliaminika kuwepo na kuongezeka hasa baada ya Dkt. Kikwete kuongoza
kamati ya maadili ya CCM iliyoliondoa jina la Lowassa katika orodha ya
waliokuwa wakiwania nafasi ya kugombea urais, hali iliyopelekea
mwanasiasa huyo kuhamia Chadema na kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza
wikendi hii na mtangazaji wa Clouds FM, Millard Ayo baada ya kuenea
mitandaoni picha inayomuonesha akisalimiana na kuteta na Lowassa,
Ridhiwani alieleza kuwa hakuna uhasama kati ya baba yake na mwanasiasa
huyo mkongwe kama wengi wanavyoamini.
Aliongeza kuwa amewahi kuwashuhudia wakizungumza na kuwasiliana kama kawaida kwa njia ya simu mara kadhaa.
“Kwanza
hakuna ugomvi kati ya watu hawa wawili. Unajua watu wanashindwa kuelewa
kwamba hakuna urafiki katika masuala ya kazi. Kwa mfano suala lile la
kumtafuta rais, jambo la kutafuta rais sio jambo la Jakaya peke yake,” alisema Ridhiwani.
“Ukweli wa mambo ni kwamba Bwana Lowassa na bwana Kikwete ni watu wanaosaidiana katika mambo mengi sana,” aliongeza.
Katika
hatua nyingine, Ridhiwani alieleza kuwa baba yake alipoona picha yake
na Lowassa wakisalimiana baada ya kukutana Jumamosi iliyopita Uwanja wa
Taifa kwenye mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga alimpigia simu
kutoka Ethiopia na kumtaka kuendelea na hali hiyo kwani siasa sio vita.
“Kwa
mfano hata jana jioni alinipigia simu, of course alikuwa yuko Ethiopia,
akaniambia ‘bwana nimeona kwenye picha uko na bwana Edward [Lowassa]
ilikuwa wapi hapo?’, nikamwambia nimekutana nae uwanja wa Taifa tulikuwa
tunaangalia mpira,” “[Akasema] ‘aah naye alikuja kuangalia mpira’
nikasema ndio. Akasema ‘okay hayo ndio mambo mnayotakiwa kufanya,
msifike sehemu mkaona kama siasa ni vita’.
“Kwahiyo
ndio maana mimi baada ya kuongea naye akaniambia siasa sio vita, na
mimi niliposhika simu yangu Instagram yangu nikaandika kwamba
‘tunaendelea kujifunza…. Lakini basically najifunza kutoka kwa maneno ya
mzee wangu ambaye ameniambia kwamba ‘siasa sio vita na kwamba na ninyi
katika umri wenu inabidi muendelee kujifunza’ kwahiyo hata mimi comment
yangu kwenye Instagram, actually sababu yake kubwa ni hiyo,” alifafanua.
Ridhiwani
alieleza kuwa alimuona Lowassa baada ya kipindi kirefu kupita hivyo
aliamua kumfuata na kumsalimia ambapo pamoja na mambo mengine, Lowassa
alimuuliza alipo Dkt. Kikwete na akampa salamu zake amfikishie na
familia kwa ujumla.
Lowassa
alilazimika kujiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu mwaka 2008 katika Serikali
ya Awamu ya Nne iliyokuwa inaongozwa na Dkt. Kikwete kutokana na sakata
la Richmond.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment