Monday, 20 February 2017

Mwanamke Aishia Mikononi mwa Polisi Baada Ya Kukutwa Akifukua Maiti ya Mwanaye, Aliamini Atafufuka Baada ya Siku 3.Fahamu zaidi hapa.

Mwanamke aliyekuwa akiamini kuwa mtoto wake angefufuka siku ya tatu baada ya kufariki dunia Februari 15, jana alizua kizaazaa baada ya kufukua kaburi na kutoa maiti hiyo, hali iliyosababisha wananchi wafanye vurugu na kuichoma nyumba yake.

Mtoto huyo, Baraka Mwafongo (22), aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu, alizikwa siku iliyofuata lakini maiti yake ilifukuliwa usiku wa kuamkia jana na kuwekwa katika pagala ikiwa imevishwa suti kumsubiri mchungaji aifufue.

Mwanamke huyo, Ruth Segeleti (52), anayeishi Mtaa wa Shigamba, Mbalizi, hakutaka kuzika maiti ya mwanawe akieleza kuwa mtoto wake angefufuka baada ya siku tatu, kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari.

Alisema polisi waliona kuwa huenda hana uwezo ndipo walipomsaidia kuzika, lakini usiku wa kuamkia jana alipata vijana wawili waliomsaidia kufukua kaburi na kuchukua maiti hiyo ambayo waliipeleka kwenye pagala na kuiweka ikiwa imevishwa suti.

Baada ya wakazi kubaini kaburi la mtoto huyo limefukuliwa, kundi la watu lilijitokeza makaburini na kusababisha polisi kufyatua mabonu ya machozi

Wananchi waligundua kuwa kaburi lilikuwa wazi majira ya saa 3:00 asubuhi baada ya majirani kumuona mwanamke ambaye walijua alikuwa na msiba wa mtoto wake Jumamosi akiwa na jembe mkononi na furushi la nguo akitokea makaburini.


“Nilipomsemesha, hakutaka kunijibu,” alisema mkazi wa mtaa huo, Mariam Mwakisepile ambaye ni jirani wa mwanamke huyo. 

“Nililazimika kuwaarifu majirani wengine ambao walikwenda makaburini ambako walikuta kaburi la Baraka likiwa limefukuliwa.”

 Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Christina Nyopelo alisema walipiga simu kituo cha polisi cha Mbalizi na kuwaarifu.

“Baada ya muda mfupi polisi waliwasili na wakiwa makaburini waliona sanduku ndani ya kaburi, lakini mwili haukuwapo,” alisema Nyopelo.

 “Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliamua kukagua maeneo ya makaburi na hatimaye walifanikiwa kuukuta mwili ukiwa umelazwa kwenye banda lililopo karibu na eneo hilo.” 

Habari hizo zilisambaa na kukusanya kundi la watu kutoka mji wa Mbalizi na kusababisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Alisema baadaye polisi walikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo na kumkamata, pia waliupeleka mwili wa Baraka, Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya kuuhifadhi.

Kamanda Kidavashari alisema mtuhumiwa alipelekwa Kituo cha Polisi Mbalizi kuhojiwa.

Umati wa watu pia ulijazana Mtaa wa Shigamba na kusababisha polisi walipue mabomu ya machozi ili kuwatawanya watu.

Jitihada hizo zilizaa matunda kwa muda mfupi, lakini ilipofika saa 8:00 mchana watu wasiofahamika waliichoma moto nyumba ya mwanamke huyo.

Katika kukabiliana na tukio hilo, polisi waliwatawanya wananchi kwa kupiga baadhi ya watu waliokutwa eneo la tukio. Kamanda Kidavashari alisema polisi wanawasaka watu waliohusika kuchoma moto nyumba ya mwanamke huyo.

Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment