Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimejipanga na
kitampatia mawakili wa chama Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe katika hatua
yake ya kumfungulia kesi ya kikatiba na ya madai Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda.
Februari
8 mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitaja majina
65 kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwamo
Mbowe na kuwataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa
ajili ya kuhojiwa.
Lakini
siku moja baadaye Mbowe aliitisha mkutano na waandishi wa habari akiwa
mjini Dodoma ambapo alieleza kutofika polisi kwa wito wa Makonda akisema
hana mamlaka hiyo isipokuwa pale tu taratibu za kisheria
zitakapofuatwa.
Mbowe
ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni aliweka bayana nia
yake ya kumfungulia mashtaka ya madai Makonda kwa kumkashifu na
kumchafulia jina.
Akitoa
maazimio ya kikao cha kamati ndogo ya Kamati Kuu ya Chadema jijini Dar
es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdalah Safari
alisema kamati hiyo inaunga mkono hatua ya Mbowe kumfungulia kesi ya
kikatiba Makonda.
“Katika
hili tumejipanga kweli kweli…tutaungana na Mbowe katika kesi hii na
tutampatia mawakili wa chama akiwamo mimi na tuko wengi,”alisema.
Profesa
Safari aliwataka wote ambao walitajwa na wanaamini kuwa walionewa
kujihusisha na biashara au utumiaji wa dawa za kulevya wafungue mashauri
mahakamani.
“Tunatoa
wito kwa wale wengine wote ambao walitajwa na wanaamini kuwa walionewa,
kuchafuliwa majina na au kudhalilishwa wafungue mashauri mahakamani,
kwani hii ndio njia pekee ya kuzuia wengine wasifanyiwe uonevu kama huu
siku zijazo,”alisema Profesa Safari.
Pamoja
na mambo mengine, Profesa Safari alisema tangu kumalizika kwa Uchaguzi
Mkuu 2015 viongozi na wanachama wa Chadema wamekuwa wakikamatwa na
kushtakiwa kwa makosa ya kubambikiziwa kwa kisingizio cha uchochezi.
Alisema mpaka sasa jumla ya wanachama na viongozi 215 wamefunguliwa kesi zaidi ya 78 nchi nzima.
“Kati
ya hao wengi wao wamenyimwa dhamana bila sababu za msingi huku wale
ambao walipatikana na hatia walipewa adhabu za vifungo bila kupewa fursa
ya faini.
“Kutokana
na hilo, hivi sasa tunaandaa orodha kamili itakayoainisha kesi zote za
jinai ambazo ziko mahakamani na kuonyesha aina ya mashtaka na vifungo
vilivyotolewa ambayo itawekwa wazi kwa vyombo vya habari na taasisi za
ndani na nje ya nchi kuthibitisha kuwa kuna mpango wa kuwafunga viongozi
wa upinzani kwa kusudi ili kuwadhoofisha,”alisema Profesa Safari.
Katika
hatua nyingine Profesa Safari aliwaomba marais wastaafu, mawaziri wakuu
wastaafu na majaji wastaafu kuzungumza na Rais John Magufuli kutokana
na yanayoendelea na kwamba wasiogope kwani wao hawatatumbuliwa.
“Marais
wastaafu Ali Hassani Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wanaogopa
nini? Kwanini wasimwambie Rais Magufuli kuwa na wao waliapa kuilinda
Katiba ya nchi hivyo na yeye afanye hivyo.
“Mawaziri
wakuu wako wapi? Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, Dk. Salim Ahmed
Salim huyu amekuwa kimya kabisa na alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa (UN), Majaji wastaafu nao wako kimya. Tunaomba waache uoga
wajitokeze wao hawatatumbuliwa,”alisema Profesa Safari.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment