UTATA umeibuka kuhusiana na biashara ya minofu ya punda nchini baada ya watetezi wa haki za wanyama kudai kuwa viumbe hao watatoweka nchini ndani ya miaka michache ijayo ikiwa kasi ya kuchinjwa kila uchao itaendelea kama ilivyo sasa.
Aidha, imeelezwa kuwa endapo jitihada hazitafanywa katika kusimamia
biashara ya minofu ya wanyama hao, kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka
kwa umaskini katika kaya za maeneo yanayotumia wanyama hao kama chombo
chao cha usafiri.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Ustawi wa Wanyama Tanzania
(Taweso), Dk. Thomas Kahema, ndiye aliyeeleza kuhusu dalili za kutoweka
kwa punda nchini wakati akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya
biashara ya punda wilayani Mpwapwa, mkoa wa Dodoma, jana.
Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Joram
Mghwira, ambaye anashughulikia wanyama, alikiri kuwapo kwa hatari ya
kutoweka kwa punda na jambo hilo kuwaathiri wananchi wanaowatumia
wanyama hao kama chombo cha kazi na usafiri, chanzo cha tishio hilo
kikiwa ni pamoja na kuwapo kwa wizi na uchinjaji holela wa wanyama hao
kwenye viwanda vilivyopo Dodoma na Shinyanga.
UTATA WENYEWE
Akifafanua juu ya kuwapo kwa hofu ya kutoweka kwa punda nchini, Dk.
Kahema alisema kuwa hadi sasa, utafiti uliofanywa na shirika lake
unaonyesha kuwa nchi nzima ina punda takribani 500,000 huku kasi ya
uchinjwaji wa wanyama hao ikifikia wastani wa punda 100 kila uchao.
Alisema takwimu hizo ndizo zinazoongeza hofu ya kutoweka kwa punda na
hivyo akazitaka mamlaka husika kuchukua hatua ya kusimamia sheria kwa
umakini ili kuwaokoa viumbe hao.
Dk. Kahema alisema kushamiri kwa biashara hiyo kila siku, kutasababisha
pia kupungua kwa nguvu kazi ya jamii zenye punda ambao huwasaidia katika
shughuli zao zikiwamo za ubebaji wa mizigo na kazi nyingine mbalimbali.
Alisema mbali na biashara ya kitoweo, pia ngozi za punda zaidi ya 100
wanaochinjwa kila uchao huuzwa katika viwanda vya Wachina vilivyopo
Dodoma na Shinyanga.
Aliongeza kuwa iwapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa sasa, taifa
litakuwa halina mnyama huyo kutokana na ukweli kuwa biashara ya ngozi
yake pia ingali ikishika kasi kubwa China na kwingineko barani Asia.
Alisema hatari zaidi ya kutoweka kwa punda nchini inaongezwa pia na
ukweli kuwa hakuna uwiano mzuri kati ya idadi ya wale wanaochinjwa kila
uchao na kuzaliana kwao.
Kuhusiana na athari za kiuchumi, Dk. Kahema alisema wastani wa bei ya
punda mmoja kwa sasa ni Sh. 200,000, lakini utafiti unaonyesha kuwa
thamani yake kwa ujumla kutokana na mchango wake kwa kaya zenye wanyama
hao ni takribani Sh. milioni 5 kwa mwaka.
“Kwa sasa punda mmoja anauzwa Sh. 200,000 wakati kwa mwaka mnyama huyo
hufanya kazi ya zaidi ya Sh. milioni 5 kwa mkulima iwapo atatumika
kusaidia shughuli za kulima, kuchota maji, kubeba mizigo na kazi
nyingine za kila siku,” alisema Dk. Kahema.
Akizungumzia utata kuhusiana na hatima ya punda nchini, Dk. Mgwira wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, alisema pamoja na serikali kuwapa vibali
wawekezaji kufungua viwanda vya nyama za punda, lakini sheria zinawataka
wawekezaji hao kuwa na mikakati ya inayoonyesha jinsi watakavyoongeza
kuzaliana kwa wanyama hao nchini.
Ofisa mmojawapo wa Kiwanda cha Nyama ya Punda cha Huwa Cheng Company
Limited kilichopo mjini Dodoma, Mohamed Hamis, alisema baada ya
kufungiwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kutozwa
faini kutokana na kasoro za kimazingira, sasa kiwanda hicho
kimefunguliwa na kinaendelea na uzalishaji.
“Hivi sasa kwa siku tunaingiza punda 40 kulingana na kibali tulichopewa…
lakini uwezo wetu ni kuchukua punda 600,”alisema Hamis, na kuongeza
kuwa jana serikali iliwapatia kibali kingine cha kuingiza punda 80 kwa
siku kutokana na wingi wa punda mnadani.
Kuhusu mkakati wa kuufanya uzalishaji uwe endelevu ili punda wasipotee,
Hamisi alisema kuna shamba la punda mkoani Singida na hadi sasa wapo
punda zaidi ya 200 wanaofugwa kukidhi sharti hilo.
Mmoja wa wafanyabiashara wa punda katika Manispaa ya Dodoma, Mussa
Charles, alisema wamekuwa wakiuza punda mmoja kwa Sh. 190,000.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment