SERIKALI imetoa ufafanuzi juu ya marekebisho ya Sheria ya Mikopo,
Misaada na Dhamana na kubainisha kuwa masharti ya mikopo ya nje,
yaliyowekwa dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), yanatokana
na masharti ya wadau wanaotoa mikopo hiyo.
Aidha, imebainisha kuwa kupitia marekebisho hayo ya Sheria ya Mikopo,
Misaada na Dhamana yanayopendekeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania (SMT) kufaulisha mkopo kwa SMZ, yana nia njema na yamelenga
kuwahakikishia wahisani hao kuwa masharti yao yanafuatwa.
Ufafanuzi huo wa serikali umekuja baada ya kuibuka mjadala mkali bungeni
kutoka kwa baadhi ya wabunge, wanaotaka marekebisho ya sheria hiyo
yabadilishwe kwa kuwa yanainyima uhuru Zanzibar kukopa yenyewe kadri ya
uwezo wake.
Hoja hizo ziliibuka baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju
kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba
4 wa Mwaka 2016 bungeni mjini Dodoma jana.
Akitoa ufafanuzi huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
alitaja baadhi ya wadau wanaoikopesha SMT ambao ni Benki ya Dunia, Benki
ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Saudi Fund, kuwa katika moja ya sehemu
ya makubaliano ya primary loans wanahitaji kuona kuna utaratibu wa
wanaonufaika kuwajibika katika malipo.
“Haya si masharti ya SMT ni masharti ya wanaotukopesha, mkiyafungia
mtaweka vikwazo kwa hawa wanaotukopesha kwa masharti nafuu,” alisisitiza
Dk Mpango.
Alisema lengo la muswada huo, ni kuweka kisheria sasa kwamba fedha
zinazokopeshwa na SMT kwa SMZ zinawasilishwa kwa masharti yaliyopo na
zinalipwa kama ilivyopangwa lakini pia kuhakikishia wahisani hao kuwa
masharti waliyoweka ya ukopeshaji yanafuatwa.
Alisema madai kwamba SMZ imekuwa ikikandamizwa na kunyimwa fursa ya
kujipatia mkopo si ya kweli, kwani hata katika sheria hiyo ya Mikopo,
Misaada na Dhamana vipo vifungu vinavyotoa mamlaka ya serikali hiyo
kupokea fedha bila kupitia mgongo wa SMT.
“Leo nimeangalia deni la nje kuanzia mwaka 1993 mpaka mwaka jana, fedha
zilizokopwa na SMT kwa ajili ya SMZ zilifikia dola milioni 772.39 sawa
na asilimia 2.59 ya deni lote la taifa letu,” alieleza Dk Mpango.
Masaju wakati akihitimisha mjadala huo, alimuunga mkono Dk Mpango kuhusu
suala hilo la kufaulisha mkopo kwa SMZ na kubainisha hata pale
itakapotokea tatizo lolote katika mikopo hiyo inayokopeshwa tena kwa
Zanzibar atakayewajibika si Zanzibar bali ni Serikali ya Tanzania.
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) aliwataka wale wote
wanaopinga marekebisho ya sheria hiyo ya mikopo, misaada na dhamana,
kuwasilisha hoja za nini kifanyike na si kubakia kulalamika hali ambayo
hailisaidii Bunge wala serikali.
Alisema kwa upande wake kutokana na uzoefu wake, haoni tatizo lolote
katika marekebisho ya sheria hiyo kutokana na ukweli kuwa yamefanyika
kwa sababu ya matakwa ya wakopeshaji na wala hayana nia yoyote ovu kama
inavyodhaniwa na baadhi ya wabunge.
“Muswada huu ni muswada mzuri, uzuri wa sheria yoyote ni pale unapoanza
kuitumia ndio utaona. Kazi ya bunge ni kutunga sheria, tunapaswa tuwe
watulivu na kujenga hoja ili kutengeneza sheria nzuri,” alisisitiza
Chenge aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aliongeza kuwa, “Namheshimu sana Lissu (Waziri Kivuli wa Kambi ya
Upinzani Bungeni Tundu Lissu) amesema mengine mazuri, lakini kwa hili
angesaidia sasa nini tufanye, kulalamika hakusaidii Bunge wala mtu”.
Alisema sheria hiyo imetungwa kulingana na matakwa ya Katiba kwani kwa
mujibu wa katiba hiyo mikopo ya nje na dhamana inayotolewa na serikali
sheria zake haziwezi kutungwa nje ya Katiba hiyo.
“Kupitia muswada huu inapendekezwa angalau ifanyike utaratibu
utakaowezesha SMZ kupata mikopo ya nje kupitia mgongo wa SMT. Huu ni
utaratibu wa watoa mikopo, haya yanayozungumzwa hapa hayaendani na
wanachokitaka watoa mikopo hiyo,” alisema.
Katika muswada huo, ambao una sheria sita zilizofanyiwa marekebisho,
kwenye marekebisho ya sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana Sura ya 134,
inapendekeza masharti mapya ya mikopo kuhusu serikali ya Muungano na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Marekebisho hayo yamependekeza serikali hizo kuingia katika utaratibu wa
on-lending (serikali ya muungano ndiyo inayokopa na baadaye kuikopesha
SMZ baada ya serikali hiyo kukidhi mahitaji na masharti ya kupewa
mkopo).
Kwa mujibu wa Masaju, marekebisho ya sheria hiyo yanapendekeza kabla ya
SMT haijakopa kwa niaba ya SMZ, lazima ijiridhishe kuwa mkopo huo
unaweza kulipwa.
“Lengo la marekebisho haya ni kuweka utaratibu wa kisheria utakaowezesha
serikali ya Tanzania kukidhi masharti ya baadhi ya wakopeshaji
wanaohitaji masharti hayo na pia kuhakikisha mikopo inalipwa kwa mujibu
wa makubaliano ya mkopo,” alisema.
Hata hivyo, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Katiba na Sheria kuhusu muswada huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Mohammed Mchengerwa, alisema kamati hiyo inaishauri serikali katika
suala hilo la ukopaji itoe uhuru mkubwa wa kukopa kwa Zanzibar kadri ya
uwezo wake.
Naye Lissu wakati akiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu muswada
huo, alisema ni wakati sasa wa serikali ya Tanzania kuipatia uhuru
Zanzibar ili nayo iwe na uwezo wa kukopa yenyewe kwa maslahi ya wananchi
wa Zanzibar.
Pamoja na yao, baadhi ya wabunge wa CUF na CCM walirushiana maneno
makali walipokuwa wakichangia muswada huo, hatua iliyompa wakati mgumu
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Najma Murtaza Giga.
Mwenyekiti huyo alilazimika kuwatuliza wabunge hao na kuwaomba
waheshimiane na kuvumiliana wakati mjadala huo ukiendelea, kwani wakati
mmoja wao akiwasilisha hoja inayopinga upande mwingine, walikuwa
wakirushiana maneno bila kuheshimu kiti.
Wakati akichangia mjadala huo, mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamadi
(CUF), aliitaka serikali kuangalia kwa makini marekebisho ya sheria hiyo
kwani badala ya kutoa unafuu kwa upande wa Zanzibar, yanazidi kuinyima
haki serikali hiyo ya SMZ.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) alisema marekebisho ya sheria
hiyo, hajalenga kukandamiza upande wowote, isipokuwa imeweka kinga na
kuongeza masharti kwa wakopaji ili kudhibiti taasisi zinazokopa kiholela
bila kuwa na uwezo wa kulipa.
Masaju alisema marekebisho hayo ya sheria ya mikopo ya elimu ya juu,
yanapendekeza bodi ya mikopo kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosomea kozi
za Stashahada (Diploma) na sifa za kupata mkopo huo zitachapishwa kwenye
gazeti la serikali.
Download Application ya Hebron Male Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment