MCHAMBUZI wa masuala ya siasa amemshauri aliyekuwa Waziri wa Nishati na
Madini mpaka katikati ya wiki iliyopita, Profesa Sospeter Muhongo kuacha
siasa na kurudi chuoni kufundisha elimu ya giologia baada ya kupata
'ajali' mbili za kisiasa ndani ya miaka miwili.
Profesa Muhongo alifukuzwa kazi na Rais John Magufuli Jumatano, ikiwa ni
miezi 28 kamili tangu ajiuzulu nafasi hiyo Januari 24, 2015 chini ya
Rais wa nne, Jakaya Kikwete.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Mhadhiri mwandamizi wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana alisema baada
ya miaka mitano ya ubunge wake ni vyema Prof. Muhongo akarudi kufundisha
ambako atatoa uzoefu wa kuwa kiongozi serikalini na mwanasiasa.
"Hatima ya kisiasa amejijengea vizuri kwa kuwa wapiga kura wake
wamemuelewa na wana imani naye ndiyo maana walimchagua," alisema
mchambuzi Prof. Bana. "Ataendelea kuwa mbunge mzuri wa jimbolake."
"Lakini kwa misukosuko hii asipokuwa na roho ngumu anaweza kukata tamaa."
Prof. Bana ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya siasa, alisema kiongozi huyo
bado ana nafasi ya kurudi kufundisha vyuoni kwa kuwa ni msomi mzuri wa
miamba na madini na kwamba ameshajizolea umaarufu kwenye medali za siasa
na kufahamika, ikiwamo uwezo wake kitaaluma.
"Kama mwaka 2020 Rais John Magufuli atapewa ridhaa ya kuendelea
kuongoza, Profesa Muhongo hawezi kurudi tena kwenye uwaziri," alisema
Prof. Bana hivyo, akitafakari ni vizuri akarudi chuoni kutoa uzoefu wake
wa serikalini na kuendelea na umahiri wake wa miamba na madini na
kuachana na siasa.
"Siasa na madaraka ya uwaziri ameshaonja, machungu yake ameyaonja, abaki
kuwa mshauri... aachane na siasa za leo ambazo ni ngumu sana.
"Kwa wasomi tumezoea kusema baibui ni baibui, lakini kwenye siasa ni tofauti."
Prof. Bana alisema ni wazi hata hivyo kuwa wakati anaingia kwenye siasa,
Prof. Muhongo alitegemea mambo hayo kwa kuwa siasa hazina adui wala
rafiki wa kudumu.
"Aliingia kwenye siasa na kuaminiwa kwa kiasi kikubwa, akapewa nafasi
kubwa serikalini kama ilivyokuwa kwa Profesa Anna Tibaijuka.
"Usomi ndiyo uzoefu wake wa muda mrefu, lakini kama tujuavyo siasa za
nchi changa kama yetu unakuwa na madaraka ambayo wengi wanayapigania.
Nirahisi kukuangusha kwa namna yoyote."
Kwa upande wake Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema hatima ya
Prof. Muhongo kisiasa itajukana baada ya kutolewa kwa ripoti ya
uchunguzi wa kamati huru kwenye mchanga wa madini.
Alisema kwa sasa ni vigumu kuthibitisha kumhukumu mbunge huyo kwa kuwa
changamoto ya kutonufaika kwa Tanzania katika madini yake ilisababishwa
na mawaziri waliomtangulia wizarani hapo na kitendo cha serikali
kuwasilisha bungeni miswada ya sheria za madini na nishati kwa hati za
dharura na kupitishwa haraka bila wabunge kupata muda mwingi wa
kuijadili.
"Kifo cha Prof. Muhongo kisiasa ni pale tu ikiundwa kamati huru ya
kuchungumza mchanga wa madini na kubaini alihusika katika uzembe
uliolisababishia taifa hasa ya matrilioni ya shilingi," alisema.
"Kwa sasa ni vigumu kumhukumu kwa sababu makosa yalifanywa na mawaziri
waliomtangulia na serikali ya CCM iliyotengeneza sheria za madini
zinazonufaisha wawekezaji."
WAPIGA KURA
Mhadhiri mwingine wa siasa UDSM, Dk. Bashiru Ally alisema bado Prof.
Muhongo ana nafasi ya kwenye ulimwengu wa siasa kwa kuwa wenye kuamua
hatima yake kisiasa ni wapiga kura wa jimbo la Musoma Vijijini.
Alisema kiongozi huyo amewajibishwa kwa uwaziri na siyo ubunge hivyo ataendelea kuwatumikia wananchi wake ambao wana imani naye.
Alisema mkataba wake na wananchi unaisha baada ya miaka mitano na hatima
yake kisiasa iko mikononi mwa wapigakura wake kwa muda wa sasa na miaka
ijayo kama atapenda kuendelea kuwatumikia.
Alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia hatima ya Prof. Muhongo
kisiasa, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema
mwanasiasa mwenzake huyo bado ana nafasi ya kurejea kwenye Baraza la
Mawaziri na hata kuwa kiongozi mkubwa nchini.
"Prof. Muhongo bado ana nafasi ya kusaidia nchi kama mbunge na anaweza
kurudi kwenye Baraza la Mawaziri au hata nafasi kubwa zaidi ya hiyo.
Mungu tu ndiye anajua mbeleni pakoje," alisema Zitto ambaye pia ni
Mbunge wa Kigoma Mjini.
Nipashe pia ilimtafuta Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza, ambaye
alisema Prof. Muhongo bado anayo nafasi ya kuitumikia nchi akiwa
mbunge.
Alisema kuwa katika uchaguzi mkuu uliopita, mwanachama mwenzake huyo aliomba ubunge na si uwaziri.
"Lakini baada ya kupata uwaziri, Rais aliona anafaa kumpangia kazi
nyingine zaidi, akaamua kumpa ili amsaidie lakini sasa Rais ameona kazi
hiyo aliyompa, ameshindwa kuifanya na ameamua kumuondoa," alisema.
Alisema kuondolewa kwenye uwaziri siyo mwisho wa safari yake kisiasa na
haimuondolei ubunge wake kwa kuwa wapo wengi waliokuwa kwenye uwaziri na
sasa wapo kama wabunge wa kawaida.
"Wapo wengi walikuwa kwenye uwaziri wakaondolewa kama Ezekiel Maige,
Prof. Anna Tibaijuka na Andrew Chenge, na wengine wengi tu lakini
wakagombea ubunge bila shida yoyote na wamepata," alisema.
Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba (CCM), alisema wananchi wa Jimbo
la Musomo Vijijini walimpa ubunge Prof. Muhongo ili awatumikie na siyo
uwaziri, hivyo anaweza kugombea na akarejea tena bungeni katika uchaguzi
ujao wa mwaka 2020.
Naye Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile (CCM), alisema Prof.
Muhongo bado anayo nafasi ya kurejea tena kwenye Baraza la Mawaziri kwa
kuwa mchango wa utaalamu wake ni muhimu kwa taifa.
Alisema ubobezi wa Prof. Muhongo katika jiolojia ni muhimu si tu kwa
Tanzania, bali duniani, hivyo mchango wake bado unahitajika katika
maendeleo ya nchi.
"Sidhani kama huu ndiyo mwisho wa Prof. Muhongo kisiasa. Kumbuka katika
uchaguzi uliopita, aliomba ubunge na si uwaziri," alisema na kufafanua
zaidi:
"Nafikiri sasa atakuwa na wakati mzuri zaidi wa kuwatumikia wananchi wa
jimbo lake. Anaweza kugombea tena uchaguzi ujao na kurejea bungeni kisha
kupewa nafasi nyingine ya kuitumikia serikali akiwa waziri.
"Ally Hassan Mwinyi alijuzulu uwaziri wa kutokana na vifo vya wafungwa
na hivi karibuni tumeshuhudia mmoja wa mawaziri wa Ubelgiji akijiuzulu
kutokana na shambulizo la kigaidi, Huko ni kuwajibika kutokana na
changamoto iliyotikea.
"Prof. Muhongo bado anayo nafasi ya kuwania ubunge, kurejeshwa kwenye
Baraza la Mawaziri na hata nafasi nyingine kubwa serikalini."
TEGETA ESCROW
Kutumbuliwa kwa Muhongo kunakuja miaka miwili na miezi minne kamili
tangu ajiuzulu nafasi hiyo kufuatia kashfa ya uchotwaji wa mabilioni
katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Januari 24, 2015.
Prof. Muhongo alimuandikia barua ya kujiuzulu Rais wa nne, Jakaya
Kikwete akieleza nia yake ya kujiuzulu baada ya kujadiliwa na kuazimiwa
bungeni, kwa sababu “nataka nchi isonge mbele”.
Dalili kwamba Prof. Muhongo angeondoka na matokeo ya uchunguzi wa kamati
iliyoongozwa na Profesa Mruma zilikuja mapema Ikulu siku hiyo baada ya
Rais Magufuli kumtaka ajipime.
“Ninampenda sana Profesa Muhongo, lakini pia ni rafiki yangu, lakini
kwenye hili ajifikirie! Aji-asses (ajitathimini) na bila kuchelewa
nilitaka aachie madaraka,” alisema Rais Magufuli akionekana mwenye
huzuni.
Muhongo ni Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini kwa tiketi ya CCM, ambaye alichaguliwa mwaka 2015.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa