Sunday 9 August 2015

#YALIYOJIRI>>>Tamko la Wizara kuhusu mgogoro wa madereva na Serikali.

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA KAZI NA AJIRA

TAARIFA KWA UMMA

TAMKO LA SERIKALI KUHUSU HATUA ZILIZOCHUKULIWA KUSHUGHULIKIA MGOGORO WA MADEREVA

1.0 Tarehe 9/4/2015 ulifanyika mgomo wa madereva nchini uliohusu malalamiko na kero mbali mbali za madereva. Katika kuzipatia ufumbuzi kero hizi, tarehe 2/5/2015 Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliunda Kamati ya Kudumu ya Kutatua Matatizo katika Sekta ya Usafirishaji yenye Wajumbe kutoka Serikalini, Umoja wa Madereva na Vyama vya Madereva, pamoja na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji. Kutokana na vikao vilivyofanywa na Kamati hiyo iliundwa Kamati Ndongo ya kushughulikia haki na maslahi ya madereva.

2.0 Kufuatia vikao vya Kamati ya Kudumu na Kamati Ndogo vilivyofanyika tarehe 12/5/2015, 19/5/2015, 21/5/2015 18/6/2015, 19/6/2015 na 23/6/2015, tunapenda kutoa taarifu kwa wadau wote wa sekta hii ya usafirishaji pamoja na wananchi wote kwa ujumla kwamba hadi sasa hatua zifuatazo zimeshakwisha kutekelezwa:

2.1 Serikali kwa kushirikiana na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Viongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji nchini imeboresha Mkataba wa Ajira wa Madereva. Mkataba ulioboreshwa uliidhinishwa na wadau katika kikao kilichofanyika tarehe 23/6/2015 na ilikubalika kwamba Mkataba huo uanze kutumika tarehe 1/7/2015. Aidha, ilikubalika kwamba hatua za kutekeleza Mkataba huo iwe ni katika kipindi cha miezi mitatu hadi tarehe 30/9/2015 ili kuwapa nafasi waajiri na madereva kuhuisha mikataba yao ya zamani na kutumia mipya na madereva watakaoajiriwa kuanzia tarehe 1/7/2015 waendelee kutumia mikataba mipya.

2.2 Kwa kuzingatia hoja ya kuimarisha umoja wa madereva, Serikali imewezesha kuundwa kwa vyama vya wafanyakazi vya madereva viwili ambavyo ni Chama cha Wafanyakazi Madereva wa Malori Tanzania (CHAMAWATA) kilichosajiliwa tarehe 28/5/2015 na Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU) kilichosajiliwa tarehe 25/6/2015. Uwepo wa Vyama hivyo utawawezesha Madereva kushiriki ipasavyo katika majadiliano ya pamoja na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kwa lengo la kuboresha maslahi na haki za madereva.

2.3 Serikali kupitia Wizara ya Kazi na Ajira imeendelea kutoa elimu ya sheria za kazi kwa Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi vya Madereva, Viongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji,na baadhi ya Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kama ilivyoelekezwa na Kamati ya Kudumu. Vikao vya uelimishaji vilifanyika tarehe 19/5/2015, 18/6/2015 na 23/7/2015. Elimu ya sheria za kazi itaendelea kutolewa kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirushaji nchi nzima kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa sheria, kanuni, na taratibu za kazi.

2.4 Ili kudhibiti tatizo la kughushi mikataba ya ajira linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, ilikubalika kuwepo na nakala tatu za mkataba kwa ajili ya mwajiri, dereva na SUMATRA. Aidha, katika utoaji wa leseni mpya kwa vyombo vya usafirishaji, SUMATRA itoe leseni baada ya wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kuwasilisha nakala ya mkataba wa ajira wa dereva ulioboreshwa.

3.0 Aidha, katika kikao cha kutoa elimu ya sheria za kazi kilichofanyika tarehe 7/8/2015. Serikali na viongozi wa Vyama vya wafanyakazi vya madereva pamoja na viongozi wa umoja wa wamiliki wa vyombo vya usafirishaji walikubaliana kwamba kikao kingine cha Kamati ya Kudumu ya Waziri Mkuu kifanyika siku ya Alhamisi tarehe 13/8/2015.

4.0
Hitimisho: Serikali inapenda kutoa wito kwa Wamiliki wa vyombo vya usafirishaji, viongozi wa vyama vya wafanyakazi vya madereva pamoja na madereva wote nchini kutekeleza makubaliano yaliyokwishafikiwa hadi sasa. Aidha, Serikali pamoja na Taasisi zake itaendelea kutoa elimu pamoja na kufuatilia makubalianao yaliyofikiwa na hatua za kisheria zitachulikwa dhidi ya wale watakaokiuka utekelezaji wa makubaliano hayo.

IMETOLEWA NA
KATIBU MKUU
WIZARA YA KAZI NA AJIRA

8/08/2015.










0 comments:

Post a Comment