Tuesday, 22 December 2015

Breaking News>>>>Rais Magufuli Amsimamisha Kazi Mkurugenzi wa shirika la reli,Pia Kaivunja Bodi ya RAHCO na bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL).Fahamu zaidi hapa.

Rais wa Jamhuri ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO) Mhandisi Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kufuatia ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais Magufuli amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za serikali ambazo zinahusika katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge"

Amesema pamoja na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Rais Magufuli ameivunja bodi ya RAHCO baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika

Aidha Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Benhadard Tito kutoa ushirikiano kwa vyombo vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa Zabuni hiyo.

Pia ameiagiza Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo endapo itathibitika kuwa zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria.

Katika hatua nyingine Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli amevunja bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) kutokana na kutoridhishwa na jinsi bodi hiyo ilivyoshughulikia ripoti ya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
22 Desemba, 2015

0 comments:

Post a Comment