Monday, 7 December 2015

#YALIYOJIRI>>>Ada Elekezi shule Binafsi: Wamiliki wa Shule Waiijia Juu Serikali.Fahamu zaidi hapa.

Taharuki imetanda kwa wamiliki wa shule nchini baada ya kupokea waraka unaowakataza kuongeza ada kwa shule zisizo za serikali katika mwaka wa masomo unaoanza mwezi ujao.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa Desemba 3, mwaka huu na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Sifuni Mchome, shule zinatakiwa kutoongeza ada mwaka wa masomo 2016 hadi zitakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu.

Tangazo hilo pia lilieleza kuwa kwa shule ambazo zimeongeza ada bila kupata kibali cha Wizara, kamwe hazitatambuliwa kwani ni batili na kwamba zimefutwa kwavile hazina nguvu kisheria.

Kadhalika, tangazo hilo lilieleza kuwa ada zote kwa shule zisizo za serikali zitabaki kama zilivyoidhishwa na kamishna ambapo waraka wa Elimu Na. 4 wa mwaka 2008 umeelekeza ada zinazotozwa shule za msingi na sekondari pamoja na zisizo za serikali.
 
Ada iliyowekwa kwa shule za kutwa zisizo za serikali ni Sh. 150,000 na shule za bweni Sh. 380,000 kwa mwaka kila mwanafunzi.

Wamiliki wa Shule Waivaa Serikali
Mkuu wa Shule ya Mtakatifu Florence ya Mikocheni, Willison Mwabwuke, alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo kutoka kwa serikali.

Alisema wao hutumia gharama kubwa kuendesha shule hiyo ikiwamo kuwalipa mishahara walimu na kununua vitendea kazi.
 
Alisema hutoza ada Sh. 2,055,000 kwa wanafunzi wa kutwa na Sh. 2,970,000 kwa wanafunzi wa bweni.

“Tunagharamia usafiri, chakula, ulinzi, maji na usafi pia tunawalipa walimu mishahara mikubwa, sidhani kama serikali watakuwa wanatutendea haki,” alisema Mwabwuke.

Alisema serikali inatakiwa kuboresha huduma katika shule za umma na siyo kuzibana shule binafsi.
 
Aliongeza kuwa ni mapema kwa serikali kuanzisha utaratibu huo.

Naye mmiliki wa Shule za Green Acres, Julian Bujugo, alisema suala hilo haliwezekani kwa sababu wahusika waliopanga kiwango hicho hawakuangalia gharama wanazozitumia shule binafsi.

Alisema shule binafsi zina magari ambayo yanatumika kuwabeba wanafunzi kutoka majumbani hadi shuleni.

Alisema kama serikali inataka kuanzisha utaratibu huo, ni dhahiri watahamia katika hospitali kwa kuwa nako zinamilikiwa na watu binafsi na kuwapangia bei.

“Hili suala sisi wamiliki wa shule binafsi tunalipinga moja kwa moja na serikali inatakiwa kufanya utafiti kwanza kabla haijaanza kutekeleza,”alisema Bujugo.

Alisema shule za Green Acres hutoza Sh. 400,000 kwa wanafunzi wa kutwa na Sh. 550,000 kwa wanafunzi wa bweni.

Alisema endapo serikali wakiendelea kusisitiza kuwapo kwa bei hizo, Green Acres hawataweza kuendelea kutoa elimu.

Alisema walimu katika shule zake wanalipwa kuanzia Sh. 700,000 hadi Sh. milioni moja kwa mwalimu wa daraja la juu na Sh. 450,000 hadi Sh. 500,000 kwa walimu wa daraja la chini.

Mkuu wa Shule ya Sahara iliyopo Mabibo, Pili Odinga, alisema ni vyema serikali ikatoa mchanganuo wa gharama hizo walizozielekeza kwa wamiliki wa shule binafsi.

Alisema Shule ya Sahara inajiendesha na haipati ruzuku kutoka serikalini.

Alisema ada ya mwanafunzi kwa shule ya msingi ni Sh. milioni moja kwa kutwa na Sh. milioni 2.2 kwa wanafunzi wa bweni kwa mwaka na kwamba ina walimu 15 wanaolipwa mishahara.

Kwa upande wake, mmiliki wa shule ya sekondari na Chuo cha Ufundi Mong’are, Joseph Mong’are alisema suala hilo haliwezekani na litakuwa gumu kutekelezwa.

Alisema kwa mfano, darasa moja lenye wanafunzi 40 kila mwanafunzi akilipa Sh. 150,000, itakuwa Sh. milioni sita kwa mwaka.

Alisema Sh. milioni sita ikigawanywa kwa miezi 12 ya kuwapa mishahara walimu itapatikana Sh. 500,000, ambayo haitaajiri walimu wala kujenga majengo, vitendea kazi, maktaba, maabara, vitabu havitanunuliwa.

Serikali Yakanusha
Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Oliva Kato, alisema serikali haijatoa waraka wa ada elekezi yoyote kwa shule zisizo za serikali kama ilivyoripotiwa, badala yake imetoa tangazo la katazo la kuongeza ada kwa mwaka masomo 2016 kwa shule hizo.

Alisema hadi sasa hakuna waraka uliotolewa na serikali ukizitaka shule hizo kutoza ada elekezi, badala yake limetoka tangazo linalozitaka kutotoza ada mpya bila kuwasiliana na Kamishna wa Elimu.

“Hakuna ada elekezi yoyote iliyotolewa na serikali kwa mwaka wa masomo 2016 limetolewa tangazo la kuzikataza shule kutotoza ada mpya mpaka zipate maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu,”alisisitiza Kato.

Alisema wamiliki wa shule hizo wamepewa wiki mbili kuwasilisha ada walizotoza mwaka huu na vibali vya kutoza pamoja na zitakazotozwa mwaka ujao wa masomo kwa ajili ya kupatiwa vibali na Kamishna.

Alisema kwa sasa bado wataalam wa wizara wanafanya utafiti za kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kutambua gharama za kumsomesha mwanafunzi katika elimu ya awali, msingi na sekondari.

0 comments:

Post a Comment