Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein Ikulu Jijini Dar es salaam.
Akizungumza
na vyombo vya habari mara baada ya mazungumzo hayo, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema lengo
la mazungumzo hayo ilikuwa ni kumpa taarifa Rais Magufuli juu ya hali ya
mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea huko Tanzania Zanzibar baada ya
uchaguzi Mkuu.
Rais
Shein amesema mazungumzo juu ya hali ya Zanzibar yanaendelea chini ya
kamati maalum ambayo yeye ndiye mwenyekiti na wengine wakiwa ni Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa awamu ya pili
wa Jamhuri ya Muungo wa Tanzania Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu
wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid
Karume na Rais Mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar Dkt. Salmin Amour.
Amesema
tayari kamati hiyo imeanza mazungumzo tangu tarehe 09 Novemba, 2015 na
kwamba mazungumzo hayo yamelenga kujadili hatma ya Zanzibar baada ya
uchaguzi Mkuu.
Rais Shein amebainisha kuwa mazungumzo hayo bado yanaendelea.
"Kwa
hiyo nimekuja kumpa taarifa Mheshimiwa Rais Magufuli kuhusu maendeleo
ya mazungumzo yetu ili aweze kujua kinachoendelea akiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake, na sisi ni
jukumu letu kumpa taarifa hiyo" Alisema Rais Shein.
Aidha Rais Shein ameongeza kuwa mazungumzo hayo yatakapokamilika wananchi watajulishwa.
0 comments:
Post a Comment