Thursday, 3 December 2015

#Hivi Punde>>>>Rais Dkt. Magufuli atoa siku saba kwa wafanyabiashara wakwepa kodi.Fahamu zaidi hapa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt.John  Pombe  Magufuli amewapa siku saba kuanzia tarehe 03/12/2015 wafanyabiashara wote ambao waliingiza mizigo yao bila kulipa kodi wakalipe kwani baada ya hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria
 
Hayo  yamesemwa leo Ikulu  jijini Dar es Salaam na Mheshimiwa Rais katika mkutano wake na wadau wa sekta binafsi  alipoamua kufanya mazungumzo nao pamoja na kuwasikiliza maoni  yao ikiwa ni sehemu ya ahadi zake katika kipindi cha kampeni za kuomba kura za kiti cha Urais,lengo likiwa ni kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Rais  aliendelea kusema kuwa katika kipindi hichi cha miaka mitano amedhamiria kuijenga nchi na watu wasimuelewe vibaya kwa maamuzi anayofanya kwani ni kwania njema ya kuleta maendeleo na siyo ujeuri.

“Tutaangalia namna ya kupunguza utitiri wa ushuru katika bidhaa mbalimbali,mfano katika kipindi cha kampeni niligundua katika Mkoa wa Kagera na Kilimanjaro wanakolima zao la Kahawa,wamekuwa wakitozwa tozo  26 kwa zao hilo na hiyo imechangia kusababisha wafanyabiashara wa zao hilo kufanya biashara haramu ya kupeleka zao hilo kwa magendo kuuza  katika nchi jirani”,alisema Mheshiwa Rais Dkt. Magufuli.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Dkt.Magufuli amewaahidi wadau wasekta binafsi ushirikiano mkubwa kwani anatambua mchango wao katika kukuza uchumi na pia amewataka wadau hao kuwa wazalendo na kuliacha kukwepa kulipa kodi ili tuweze kujenga taifa lenye maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli  ameendelea kusema kuwa kama kutakuwa na mfayabiashara yeyote  atakayetaka kuwekeza  na akakwamishwa na  mtu aliyechini ya uteuzi wake  basi mtu huyo ataondoka kwani sasa ni wakati wa wadau wa sekta binafsi kuanza kuanzisha viwanda mbalimbali vitakavyo toa ajira.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli amewapa mawazo ya kibiashara wadau wa sekta binafsi kuanzisha kampuni ya kutenganisha udongo unaotoka kwenye machimbo ya madini,kuanzisha viwanda vya samaki pembezoni mwa bahari pamoja na kutengeneza samani zitokanazo  na mazao ya misitu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw.Regnald Mengi amesema kuwa wako tayari kumpa ushirikiano mkubwa  Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha uchumi watanzania unakuwa kwa haraka na pia amemuomba mheshimiwa rais kuendelea kukemea masuala ya rushwa  pamoja kusaidia kupunguza utitiri wa kodi.
 Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Reginald Mengi akiongea katika mkutano huo na kumuahidi Rais Dkt. Magufuli ushirikiano katika kutekeleza yale anayodhamiria kwenye serikali yake ikiwemo kusimamia ulipaji kodi kwa dhumuni la kuiinua Tanzania kiuchumi
 Baadhi ya Wadau wa Sekta Binafsi wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa mkutano huo Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Bw. Reginald Mengi akimpongeza  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipomaliza kutoa hotuba kwa wajumbe wa Sekta Binafsi nchini Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimueleza Jambo Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Reginald Mengi wakati wa Mkutano na Wadau wa Sekta Binafsi nchini Ikulu leo Jijini Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment