MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amemuomba mmiliki wa
Kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na mfanyabiashara Yussuf Manji
kutumia busara kukubali kuuachia ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sadiki alisema
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi katika uamuzi wake imeiamuru
Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni ya Q Consult
kwa ajili ya kampuni hiyo kuendeleza ufukwe huo hata hivyo Manispaa ya
Kinondoni imekata rufaa.
“Kampuni
ya Q Consult kwa busara tu iachane na kesi, ikubali kurudisha ufukwe
huo chini ya mamlaka ya Kinondoni ili iweze kuuendeleza ufukwe huo kwa
manufaa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na sio kwa manufaa ya mtu
mmoja kama anavyotaka mtu huyo,” alisema Sadiki.
Alisema
wananchi wafahamu kuwa ufukwe huo wa Coco haujauzwa, kama watu
wanavyodai na kwamba kesi hiyo iko mahakamani, ambapo Ofisi ya Manispaa
ya Kinondoni kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekata rufaa.
Akielezea
sakata hilo, Sadiki alisema kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na Manji
mwaka 2007 iliingia mkataba na Manispaa ya Kinondoni kuendeleza ufukwe
huo.
Alisema,
hata hivyo, baadaye Manispaa ya hiyo ilivunja mkataba huo baada ya
Kampuni ya Q Consult kushindwa kutimiza masharti, jambo ambalo
liliifanya kampuni hiyo kwenda mahakamani.
Mahakama
Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi iliamuru Manispaa ya Kinondoni,
kutekeleza mkataba wake na kampuni hiyo kwa ajili ya kuendeleza ufukwe
huo.
“Kama
nilivyosema kupitia mwanasheria mkuu wa Serikali tumekata rufaa katika
uamuzi huo kwasababu tunaamini haukuwa sahihi, hata hivyo mwekezaji huyo
namshauri tu anaweza kufanya maamuzi akaachana na kesi hiyo na kuamua
kurudisha ufukwe huo uendelee kutumiwa na Watanzania wote,” alisema Sadiki.
Kwa
kampuni hiyo kushinda kesi hiyo, inamaanisha kuwa mwekezaji huyo endapo
ataendeleza eneo hilo, wananchi hawatakuwa na fursa hiyo tena, kama
wanavyoutumia sasa.
Sadiki
alisema tayari serikali imefanya mazungumzo na moja na benki hapa
nchini kwa ajili ya kupata mkopo, ambao utasaidia kuendeleza eneo hilo
ili liendelee kubaki chini ya Manispaa ya Kinondoni na kutumiwa na watu
wote.
0 comments:
Post a Comment