Mmamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imewagomea kulipa kodi bila adhabu baadhi ya
wamiliki wa makontena, ambayo yalitoroshwa kwenye bandari kavu bila
kulipiwa kodi.
Badala
yake, TRA imewapelekea hati ya malipo inayowataka wafanyabiashara hao,
kuhakikisha wanalipa kodi hiyo na adhabu ndani ya siku saba, la sivyo
watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Hatua
hiyo inatokana na baadhi ya wamiliki wa makontena hayo, kuiomba TRA
kuwasamehe kulipa adhabu waliyopewa badala yake waruhusiwe tu kulipa
kodi stahiki ya Serikali.
Jumla ya makontena 349 yalitoroshwa katika bandari kavu bila kulipa kodi na kuikosesha Seri kali mapato ya Sh bilioni 80.
Wafanyabiashara
hao, pia wameomba waruhusiwe kulipa kodi wanayotakiwa kulipa kidogo
kidogo kwa madai kuwa wengine hawana uwezo wa kulipa kiasi hicho cha
fedha kutokana na kutapeliwa na mawakala wao waliowatumia kwenda kulipa
kodi hiyo.
Wakizungumza
na mwandishi, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema agizo la Dk
Magufuli alilotoa Desemba 3, mwaka huu kuwa linawataka walipe kodi hiyo
ndani ya siku saba.
Lakini
wafanyabiashara walisema nyaraka za malipo walizopelekewa na TRA,
zimewataka kulipa kodi na faini kwa pamoja wakati hizo siku saba
alizotoa Dk Magufuli hazijamalizika.
Wafanyabiashara
hao wanadai kuwa walishalipa kodi hiyo kupitia kwa wakala wao, kama
taratibu za TRA zinavyowataka kuwatumia mawakala wa bandarini kulipa
kodi, lakini kwa bahati mbaya wakala huyo hakufikisha kodi hiyo
serikalini.
Walidai kuwa walifuatilia nyaraka za kodi kwa wakala wetu, lakini akawa anawaambia wasubiri.
“Tunaomba
hii adhabu tusamehewe, kwani sio kosa letu ila tuko tayari kulipa kodi
halali ya Serikali, lakini wakala wetu ndiye katuingiza kwenye matatizo
haya na yeye tayari ameshatoroka,” aliongeza mfanyabiashara huyo.
Katika nyaraka za kodi ambazo TRA imewapelekea, kontena moja linatakiwa kulipiwa ushuru wa Sh milioni 40.5 ndani ya siku saba na adhabu ya Sh milioni 28.3. Hivyo jumla wanatakiwa kulipa Sh milioni 68.8 kama ushuru na adhabu.
Akizungumza
na mwandishi kuhusu madai hayo ya wafanyabiashara, Mkurugenzi wa Idara
ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema
adhabu walizoandikiwa wafanyabiashara hizo, wanatakiwa kuzilipa pamoja
na kodi stahiki ndani ya siku saba.
Alisema
wamewawekea adhabu hiyo kutokana na kitendo chao cha kuiibia Serikali
na kwa taratibu za nchi, walitakiwa wawe mahabusu sasa hivi, lakini
wametakiwa kulipa ushuru wa Serikali wakati wakiwa nje; hivyo
wanastahili kulipa kiasi hicho cha fedha kama adhabu ya kukwepa kodi.
“Hawa
walitakiwa kukamatwa na kuwekwa ndani, walitoa kontena nje ya
utaratibu, adhabu hiyo ni ya kutoa makontena bila kulipa kodi,” alisema Kayombo. “Wakishindwa kulipa ndani ya muda huo tutawakamata tena na kuwafikisha mahakamani,” alieleza.
Kayombo
alifafanua kuwa siku saba hizo walizopewa wafanyabiashara hao ni
kusamehewa kutoshitakiwa mahakamani na sio kusamehewa kulipa adhabu
wakati tayari walishakiuka taratibu.
Alisema
wafanyabiashara hao, wachague kulipa ndani ya siku saba wasishitakiwe
au waache ili wakutane na rungu la dola la kufikishwa mahakamani.
Alisema
hadi sasa TRA imeshakusanya Sh bilioni 9.4 kati ya Sh bilioni 80
zinazotakiwa kulipwa kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara hao waliokwepa
kodi.
0 comments:
Post a Comment