TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UTEKELEZAJI WA AGIZO LA MENEJIMENTI YA MAAFA KWA KAMATI ZA MAAFA NGAZI ZA MIKOA, WILAYA, KATA NA VIJIJI
Kufuatia
taarifa ya tahadhari ya uwezekano wa kuwepo kwa mvua za El-Nino
iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Mwezi Agosti 2015, Ofisi ya
Waziri Mkuu ilitoa agizo kwa Mikoa yote nchini kuchukua hatua za
kujiandaa na kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea kutokana na mvua
hizo.
Kamati
za Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ambazo ndizo zenye jukumu
kubwa la kusimamia masuala haya, hazijatekeleza agizo hilo kwa kuainisha
hatua zilizochukuliwa katika Kuzuia/Kupunguza, Kujiandaa, Kukabili na
Kurejesha hali baada ya maafa kutokea. Hivyo;
“Naagiza
wenyeviti wa kamati za maafa katika ngazi husika kwa kushirikiana na
taasisi na idara za serikali zinazohusika waorodheshe watu wote
wanaoishi katika maeneo hatarishi na kuwapa barua za kuwataka kuhama
mara moja katika maeneo hatarishi ili kuepuka athari za maafa.
"Taarifa
za utekelezaji wa agizo hili ziwasilishwe katika Ofisi ya Waziri Mkuu
haraka sana kadri iwezekanavyo” amesema Mhe. Mhagama.
Ili kutekeleza agizo hili ninaziagiza Kamati za maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji ziwajibike kutekeleza mambo yafuatayo;
I.
Kamati zote ambazo hazijatekeleza maagizo yaliyotolewa na viongozi
katika kushughulikia maafa zitoe maelezo ya kwanini hazijatekeleza
maagizo hayo kwa mamlaka husika.
II.Endapo
kutatokea maafa mahali popote katika nchi yetu kwa sasa, kamati za
maafa zitawajibika kuelezea sababu za kutokea kwa maafa hayo ni nini
katika maeneo yao na kuainisha hatua zilizochukuliwa na kamati hizo za
kukabili hali hiyo iliyojitokeza. Lakini taarifa hizo pamoja na
kuwasilishwa kwenye mamlaka husika pia ziwasilishwe kwenye vyombo vya
habari.
III.Kamati
zote za maafa katika ngazi zote, zitoe maelezo na mipango waliyonayo
juu ya kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu janga ambalo
linasababisha maafa katika nchi yetu.
IV. Kamati
zote za maafa katika ngazi zote, zishirikishe wadau wa maafa (Wananchi,
Taasisi na Sekta binafsi) katika mipango yao yote ya kukabili maafa ya
menejimenti ya maafa.
V.Kamati
zote za maafa ziendelee kuratibu na kutoa taarifa juu ya misaada yote
ya maafa inayotolewa na Serikali pamoja na wadau katika kusaidia
waathirika wa maafa pale yanapotokea.
VI.Kamati
hizo za maafa katika ngazi zote zinatakiwa, kuchukua /kumchukulia hatua
mtendaji na mhusika mwingine yeyote ambaye hatatimiza wajibu wake na
kutotekeleza maagizo yanayotolewa na viongozi nchini katika kukabili
maafa mahali popote.
“Serikali
inawaomba wadau wote wa maafa ushirikiano wa hali ya juu katika jambo
hili muhimu katika nchi yetu ili kuweza kuokoa watanzania wengi ambao
wanaweza kukumbwa na maafa kwa namna moja ana nyingine”, amesisitiza Mhagama
Aidha,
Sheria Na. 7 ya Mwaka 2015 ya Menejimenti ya Maafa inamtaka kila mdau
kutekeleza wajibu wake katika suala zima la menejimenti ya maafa ikiwa
pamoja na Kuzuia, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali baada ya maafa
kutokea.
“Napenda
kuchukua fursa hii kuzikumbusha Kamati za maafa katika ngazi za Mikoa,
Wilaya,Kata na Vijiji kuhakikisha kuwa zinatimiza wajibu wao katika
suala zima la kushughulikia maafa kwa mujibu wa sheria” amesema Mhe. Mhagama.
Hivi
sasa sehemu mbalimbali za nchi yetu zimekuwa zikipata mvua nyingi
ambazo zimesababisha maafa na baadhi ya sehemu zinakabiliwa na ukame.
Taarifa
nyingi zilizopokelewa zinaonesha baadhi ya maeneo ya nchi yetu yamekuwa
yakipata mvua nyingi ambazo zimesababisha maafa bila Kamati za Maafa za
Mikoa, Wilaya,Kata na Vijiji kuainisha hatua zilizochukuliwa katika
Kuzuia/Kupunguza, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali baada ya maafa
kutokea.
Iwapo
juhudi za ngazi zote pamoja na Mkoa zitashindwa kukabili maafa
yanayotokea katika ngazi za Wilaya, Kata na Vijiji, taarifa na maombi
zitumwe katika ngazi ya Taifa kwa kuzingatia maelekezo/mwongozo wa
uombaji wa misaada na utoaji wa taarifa za maafa uliotolewa na Ofisi ya
Waziri Mkuu.
Imetolewa na
JENISTA J. MHAGAMA (MB)
WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU
SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU
22 DESEMBA 2015
0 comments:
Post a Comment