Sunday, 27 December 2015

#YALIYOJIRI>>>Mrithi wa Dk Slaa CHADEMA Kujulikana Mwezi Ujao.Fahamu zaidi hapa.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema mchakato wa kumpata katibu mkuu wake utaanza mwezi ujao.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, ndiye mwenye jukumu la kupendekeza jina la Katibu Mkuu na kulipeleka katika Baraza Kuu kupigiwa kura, kisha kupitishwa.

Tangu Agosti 3, Katibu Mkuu wa chama hicho Dk Willibrod Slaa alipumzishwa na Baraza Kuu baada ya kutofautiana na Kamati Kuu baada ya chama hicho kumkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu ndiyo anakaimu nafasi iliyoachwa wazi na Dk Slaa.

Mchakato wa kumpata Katibu Mkuu umeanza kuibua hali ya sintofahamu, huku majina mbalimbali ya vigogo wa chama hicho yakitajwa, likiwemo la Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ambaye hivi karibuni alitangaza rasmi kujiunga na Chadema.

Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema Ibara ya 6.3.5 inasema; (b) nafasi wazi za uongozi walioteuliwa zitazibwa na vikao husika kwa kufanya uteuzi mpya katika muda usiozidi miezi mitatu tangu nafasi kuwa wazi, (c) muda wa uongozi wa muda kwa mujibu wa kifungu 6.3.5 (b) hautazidi mwaka mmoja (d) bila kujali sharti la kifungu 6.3.5 (c) hakutafanyika uchaguzi rasmi wa kuziba nafasi kama kumebakia miezi sita tu au chini ya hapo kabla ya uchaguzi mkuu wa kawaida wa Chama unaofuata kufanyika.

Akizungumzia mchakato huo, Mwalimu alisema Baraza Kuu litakutana mapema Januari mwakani, kujadili masuala mbalimbali, likiwamo la kumpata Katibu Mkuu.

“Si kama chama kimekaa muda mrefu bila Katibu Mkuu. Yupo anayekaimu na kinachofanyika sasa ni kumpata Katibu kamili.”

“Baraza Kuu lilikutana litajadili suala hilo kwa kina na kuja na mapendekezo mbalimbali,” alisema Mwalimu na kusisitiza kuwa kila jambo litafanyika kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

Alisema uongozi wa muda ndani ya chama hicho hauwezi kuzidi mwaka mmoja na nafasi ya kuteuliwa muda wa kukaa wazi hauzidi miezi mitatu kabla ya kuteuliwa kiongozi mwingine.

0 comments:

Post a Comment