Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma imeanza rasmi kutekeleza Ahadi ya Uadilifu kwa watumishi wa Umma nchini .
Akiongea
na vyombo vya habari leo, Katibu Mkuu Hab Mkwizu amesema utekelezaji
huo umeanza rasmi Desemba, 2015 ambapo kila Mtumishi wa Umma ataweka
saini ya kiapo kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na mazingira ya
taasisi husika.
“Utaratibu
wa Utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa Watumishi wa Umma umetolewa
kupitia waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na. 2 wa mwaka 2015 kuhusu
utekelezaji wa Ahadi ya Uadilifu kwa viongozi, Watumishi wa Umma na
sekta binafsi wa tarehe 1 Agosti, 2015.” alisema Mkwizu.
Mkwizu
aliongezea kwa kusema, uanzishwaji wa Ahadi na Uadilifu ni muendelezo
wa uundwaji wa vyombo vya kusimamia maadili baada ya ongezeko kubwa la
ubadhirifu, utoro sehemu za kazi na kushuka kwa nidhamu katika kipindi
cha miaka ya themanini na tisini.
Alivitaja
vyombo vingine ambavyo vilianzishwa kusimamia ahadi na uadilifu kuwa ni
Sekretariate ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Tume ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Mkwizu
alivitaja vipengele ambavyo mtoa ahadi anatakiwa kuvitamka ni, kuwa
mzalendo wa nchi yake na kutii Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania, kuhudumia Umma na watumishi wenzake kwa heshima, kutimiza
wajibu wa kutoa huduma bora kwa umma, kutoa huduma bora kwa usawa kwa
watu wote na kutofanya ubaguzi wa dini, siasa, kabila, udugu, ukanda,
jinsia, urafiki au hali ya mtu.
Vipengele
vingine ni kutumia rasilimali za Umma kwa manufaa ya Umma, kutotoa siri
za Serikali au mteja kwa watu wasiohusika isipokuwa kwa maslahi ya
Umma, kufanya kazi kwa nidhamu ya hali ya juu, kutoomba kushawishi,
kutoa wala kupokea rushwa na kutotumia madaraka kwa manufaa binafsi ya
ndugu, rafiki au jamaa.
Aidha,
Mkwizu ametoa wito kwa waajiri wote kuhakikisha kuwa utekelezaji wa
Ahadi na Uadilifu unakamilika ifikapo tarehe 31/12/2015 na kuwasilisha
Ofisi ya Rais – UTUMISHI kabla ya tarehe 25/02/2016 na utekelezaji wake
kuwa kila ifikapo Juni 30 ya kila mwaka.
Fomu za Ahadi ya Uadilifu zinapatikana katika tovuti ya Ofisi ya Rais – UTUMISHI yenye anwani www.utumishi.go.tz.
0 comments:
Post a Comment