Hatimaye
vigogo watatu wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) akiwemo kamishna wa
forodha na ushuru wa mamlaka hiyo, Tiagi Masamaki wameachiwa kwa
dhamana na mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, baada ya kutimiza masharti
ya dhamana yaliyotolewa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam.
Washtakiwa
hao wamedhaminiwa kwa sh. Bilioni 6.6, na hati za mali zisizohamishika
zilizowasilishwa katika mahakama ya Kisutu ambapo dhamana ya vigogo hao
imetolewa na hakimu mkuu mfawidhi wa mahakama ya Kisutu, baada ya
washtakiwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa na jaji wa mahakama
kuu Winfrida Koroso.
Jaji
Koroso alisema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana kila mwombaji
alitakiwa aweke mahakamani sh. Bilioni 2.1 au hati za mali
isiyohamishika zenye thamani hiyo na wadhamini wawili watakaosaini
dhamana ya sh. Milioni 20.
Baada
ya hati hizo kuwasilishwa mahakamani hapo, hakimu alikubaliana na hati
hizo na kuwapatia washtakiwa dhamana, lakini wakili wa serikali
Christopher Msigwa aliomba mahakama hati hizo zikafanyiwe uhakiki kwa
sababu zingine anamashaka nazo.
Aidha wakili Msigwa amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na itatajwa Desemba 30 mwaka huu.
Washtakiwa
ambao hawajaomba dhamana na wamerudishwa rumande na mahakama kuu ni
msimamizi mkuu wa ICD-Azam, Eliachi Mrema, mchambuzi mwandamizi wa
masuala ya biashara TRA, Khamis Omary, Haroun Mpande wa kitengo cha
mawasiliano ya kompyuta ICT - TRA, meneja uendeshaji usalama na ulinzi
wa Azam ICD, Raymond Louis na meneja Azam ICD, Ashraf Khan.
Desemba
3, mwaka huu, Masamaki na wenzake walipandishwa kizimbani katika
mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama ya
kudanganya na kuisababishia serikali hasara ya sh. Bilioni 12.7 kutokana
na makontena 329 kukwepa kodi.
0 comments:
Post a Comment