TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI KUHUSU TUKIO LA KUSHAMBULIWA KWA HELKOPTA YA DORIA NA KUUAWA
KWA RUBANI ROGERS GOWER TAREHE 29/01/2016
1.0
UTANGULIZI
Itakumbukwa
kuwa mnamo tarehe 29/01/2016 lilitokea tukio la kuhuzunisha ambapo majangili
walishambulia helikopta iliyokuwa inafanya doria katika maeneo ya Pori la Akiba
Maswa na Ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba. Shambulio hilo lilisababisha kifo cha
Rubani Bw. Rogers Gower raia wa Uingereza na kuharibika vibaya kwa helkopta
hiyo baada ya kuanguka. Aidha, katika tukio hilo Bw. Nick Desta aliyekuwa
pamoja na Bw. Rogers aliweza kunusurika na kukimbizwa Nairobi kwa ajili ya
matibabu zaidi.
Tarehe 30/01/2016 nilitembelea eneo la tukio ili kujionea
hali halisi na kutoa tamko la serikali. Haiyumkini, kutokana na kuguswa na
kadhia hiyo, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John P.
Magufuli alitoa maelekezo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuanza kufanya
msako haraka wa kuhakikisha kuwa wahalifu hao wanakamatwa na kufikishwa kwenye
vyombo vya Sheria. Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Major
Gen. Gaudence Millanzi akifuatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania
(TAWA), Major Gen. Hamisi Semfuko na baadhi ya watendaji wa Wizara walitembelea
eneo hilo tarehe 02 hadi 03/02/2016.
Napenda kuwajulisha kuwa, katika ziara zote mbili
tuliweza kushuhudia namna watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii (Pori la
Akiba Maswa, Kikosi Dhidi Ujangili Bunda, Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mamlaka
ya Hifadhi Ngorongoro) kwa kushirikiana
na vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Taifa na vya Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya
Meatu na Maofisa kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
Viongozi wa FRIEDKIN CONSERVATION FUND,
Bw. Dan Friedkin na Bw. Pratik Patel na watumishi
wengine kwa pamoja walisaidiana sana katika kuendesha msako kwa juhudi kubwa na
weledi wa hali ya juu. Kazi hii ilifanyika usiku na mchana katika mazingira
magumu na hatarishi. Mara kadhaa watendaji hao wamekuwa wanalazimika kuvuka
makorongo na mito yenye maji mengi kwa kuogelea kutokana na mvua zinazoendelea
kunyesha katika maeneo hayo.
Mtakumbuka kuwa taarifa zilizopatikana baada ya tukio
hilo la kusikitisha zilibainisha kuwa majangili waliohusika na tukio hilo
walikuwa watatu (03) na kwamba walikuwa na bunduki mbili aina ya rifle zenye
ukubwa wa mtutu (calibre) wa 303 na .458 mtawalio. Aidha, wakati wa tukio hilo,
majangili hao tayari walikuwa wamefanikiwa kuua tembo mmoja na kutoweka na meno
yake mawili.
2.0 HATUA ZILIZOFIKIWA:
Kama mlivyosikia kwenye taarifa iliyotolewa na Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Simiyu, sote kwa pamoja tunafarijika kuwajulisha kuwa
jitihada zilizofanyika za kuwasaka wahalifu hao ndani ya kipindi cha wiki moja
zimeleta matokeo mazuri ambapo:
· watuhumiwa wote muhimu (key suspects) waliotajwa kuhusika na tukio hilo
wamekamatwa na wote wamekiri kuwepo kwenye tukio. Mmojawapo anatuhumiwa kuhusika
moja kwa moja na kufyatua risasi iliyosababisha kuanguka kwa ndege hiyo na
hatimaye kifo cha rubani.
· bunduki mbili zilizotumika aina ya Rifle Calibre 303 na .458 zinazoshukiwa
kutumika kwenye uhalifu huo zimekamatwa pamoja na risasi 5 za .458 na moja ya
303;
·
meno mawili ya tembo aliyeuawa siku ya tukio yenye uzito wa kilo 31
yamekamatwa;
·
pikipiki moja ambayo inashukiwa kuhusika katika tukio hilo na matukio
mengine ya uhalifu imekamatwa;
· raia wema wanaendelea kutoa taarifa zinazobainisha kuwepo kwa mtandao mkubwa
wa ujangili katika Mkoa wa Simiyu na maeneo ya jirani. Taarifa hizo zimesaidia kupanua
wigo wa operesheni na kuwezesha kuboresha mbinu za mapambano dhidi ujangili.
3.0 MPANGO MAHSUSI WA WIZARA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI UJANGILI NA USAFIRISHAJI HARAMU WA MAZAO YA
WANYAMAPORI NA MISITU
Tukio hili limetoa funzo kubwa kwa nchi yetu na linadhihirisha
kuwa hivi sasa baadhi ya majangili
wamefikia hatua ya kujijengea uthubutu na ujasiri wa kutisha.
Kutokana na mazingira haya, Wizara ya Maliasili na
Utalii imeamua kurejea (review) kwa haraka na kwa upana zaidi mbinu na mikakati
yake ya vita dhidi ujangili wa wanyamapori na mazao ya misitu pamoja na usafirishai
haramu wa mazao ya wanyamapori na misitu kwa kufanya yafuatayo:
1. Kukamilisha haraka uanzishaji wa Kikosi Maalum cha
Kupambana na Uhalifu wa wanyamampori (Wildlife
Crime Unit);
2. Kikosi hiki kitaundwa kwa kushirikisha Taasisi zote za
Wizara (Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania
(TAWA), Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Aidha, kitafanya kazi kwa karibu na
Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Sheria, Mamlaka ya Bandari, Viwanja vya Ndege,
Mamlaka ya Mapato Tanzania, Taasisi za Uhifadhi za ndani na nje ya Nchi na
wadau wengine wa Uhifadhi;
3. Kikosi hiki kitakuwa na jukumu la kuratibu na
kufuatilia utendaji wa vikosi vidogo (Taskforce Coordinating Groups TCGs))
vilivyoundwa kwenye kanda nane za kiikolojia (ecosystem approach) ili kukabili
kwa haraka nyendo zote za ujangili wa wanyamapori, uvunaji na usafirishaji
haramu wa mazao ya wanyamapori na misitu;
4. Kuharakisha ukamilishaji wa kubadilisha muundo wa
utendaji kazi wa Wahifadhi Wanyamapori kutoka mfumo wa Kiraia kuelekea mfumo wa Jeshi Usu (Paramilitary);
5. Kuharakisha usimikaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA) iliyozinduliwa Oktoba 2015 katika jitihada za kuimarisha na
kuboresha uwekezaji binafsi wa Serikali katika maeneo yaliyopo nje na ndani ya
Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorogoro;
6. Kurejesha utaratibu wa kuwa na kada ya walinzi wa
misitu (Forest Rangers) ambao watakuwa na uwezo wa kutumia silaha ambapo pamoja
na kudhibiti uvunaji haramu wa misitu, utapanua wigo wa kukabili ujangili
katika Hifadhi za Misitu;
7. Kuishauri serikali kuangalia upya endapo bado kuna sababu
za msingi kwa wananchi kuendelea kununua na kumiliki bunduki zenye mitutu mikubwa.
Uamuzi huu unatokana na kuongezeka kwa matukio ya kukamatwa kwa silaha hizo
zikiwa zinatumika kwenye vitendo vya uhalifu nje ya mikono ya wamiliki halali;
8. Kuboresha utendaji kazi wa wahifadhi kwa kuwapatia
mafunzo ya mbinu mpya za ukusanyaji habari na ufuatiliaji wa nyendo za majangili
(intelijensia), kukusanya na kutunza kumbukumbu za ushahidi na kuendesha
mashtaka (Inteligence, investigation and prosecution);
9. Kuimarisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa ikiwa ni
pamoja na kuwashirikisha wadau wa uhifadhi katika kuchangia ununuzi/upatikanaji
wa vifaa hivyo ili kukabili kasi ya mbinu mpya zinazotumiwa na majangili na wasafirishaji
haramu wa mazao ya wanyamapori na misitu;
10.
Kwa kuwa katika Operesheni hiyo,
wako Askari wa Wanyamapori wanaotuhumiwa kushiriki katika uhalifu wa kijangili,
askari hao watafikishwa katika Mahakama ya kijeshi ili kukabiliana na mashitaka
ya kijeshi ya kukiuka kiapo na dhamana waliyopewa.
4.0 HITIMISHO
Napenda
kutumia fursa hii kutambua na kuwapongeza
watendaji wote, Uongozi wa Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Meatu. Napenda
kupongeza na kuishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Jeshi la
Polisi, Jeshi la Wananchi, Usalama wa Taifa Shirika la Friedkin
Foundation na wadau wengine wote walioshiriki katika msako
huu hadi kufanikisha na kutimiza azma iliyokusudiwa na Mhe. Rais wa
Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli pamoja na Watanzania wote wenye mapenzi mema na Taifa letu.
Kama nilivyotangulia kueleza, pamoja na mazingira
magumu yaliyojitokeza wakati wa kutekeleza kazi hii, washiriki wote waliweza kuendesha
operesheni hii kwa ari kubwa na weledi wa hali ya juu hadi kukamilisha lengo
kuu ndani ya kipindi kifupi. Aidha,
naomba kuwashukuru wananchi wote ambao kwa namna ya pekee waliweza kutoa
ushirikiano kwa kutoa taarifa muhimu zilizoweza kufanikisha lengo hili.
Pia nawashukuru wadau wote walioweza kutoa michango ya
hali na mali kwa watendaji wa operesheni hii. Michango yao ilikuwa chachu kwa
washiriki wa operesheni kuwajengea mazingira kuendelea kujituma kwa kupunguza
makali ya ugumu wa mazingira wakati wanatekeleza jukumu hili. Aidha, natoa wito kwa wananchi wote waendelee
kuisaidia Wizara katika vita hii kubwa ya kukabili ujangili na usafirishaji
haramu wa rasilimali zetu.
Imetolewa na:
Waziri wa Maliasili na Utalii
09/02/2016
0 comments:
Post a Comment