Friday, 12 May 2017

TUHUMA za Mateso Dhidi ya Wafanyakazi wa Ndani Oman, Mtanzania Afunguka Makubwa.

Wafanyakazi wa majumbani walioko Oman wanatoka kila mahala duniani. Wafilipino peke yao ni wengi mara nyingi sana kuliko Watanzania na huwasikii ila wachache sana kulalamika. Lakini idadi ya walalamikaji kutoka Tanzania ndiyo iliyo kubwa kabisa ingawa jumla yao ni ndogo sana Oman.

Wapendwa waungwana na wapenda ukweli. Siku hizi za karibuni kumekuwako na upotoshwaji mkubwa wa habari za wafanyakazi wa ndani nchini Oman. Jamani waungwana, Waswahili husema kunya anye kuku akinya bata huambiwa kaharisha. Hizo habari za mayaya Oman ni za fitina na uchochezi uliokithiri na hazitamsaidia mtu yoyote, maana sisi ndio wahitaji zaidi wa hizo ajira nje ya nchi yetu.

Nchi za GCC zimekuwa na utaratibu wa miaka mingi kuajiri wafanyakazi kutoka nchi za Asia. Kwa kuzingatia msemo “mfae nduguyo kwanza” ndipo Waomani wakawa pia na utaratibu wa kuwaajiri wafanyakazi kutoka Afrika Mashariki, kwa kuwa kuna historia ya muda mrefu na ya kidugu baina yao. Sasa imekuwa balaa kila kukicha ni matusi yasiyokuwa na maana ila kutapakaza fitina na chuki kwenye mitandao ya kijamii na hata baadhi ya vyombo vya habari kama vile magazeti na televisheni.

Bora nitangulize kusema kitu kimoja ambacho mtu yeyote mwenye akili zake timamu na kupenda kusikia ukweli hawezi kukikataa, nacho ni kuwa hakuna nchi yoyote duniani ambayo haina watu wema na pia watu waovu. Mambo ni kuzidiana tu. Wala hakuna nchi yenye matajiri wenye kuajiri wafanya kazi pasitokee wenye kudhulumu na wenye kudhulumiwa. Kwa vile nazijua vizuri nchi mbili hizi — Tanzania na Oman — naweza pia kusema kwa uhakika kuwa baina ya Tanzania na Oman, utakuta kuwa dhulma wanazotendewa wafanyakazi wa majumbani Tanzania ni kubwa zaidi ukilinganisha na Oman.

Hapa Tanzania wapo wafanyakazi wanaoteseka kila siku na jamaa zao wenyewe kwa mshahara wa shilingi 20,000 au 40,000 kwa mwezi. Sio hilo tu la mshahara, bali hata siku za mapumziko za Jumamosi na Jumapili au zile sikukuu za kitaifa, hawapewi. Haya ni ya ukweli kabisa na wala sio siri. Ukitaka kumtoa mtu kijiti jichoni mwake, kwanza jiangalie kama jicho lako halina boriti.

Hapa Tanzania wafanyakazi wana kila mateso lakini wanavumilia tu. Ukifuatilia kwa makini utagundua kuwa haya ya uchochezi uliojaa fitina unatokana na kundi fulani ambalo hawapendelei pawe na masikilizano mema baina ya Waarabu na Waafrika. Na lengo lao hasa hata si Waarabu. Ukipeleleza kwa makini utagundua kuwa wanachokichukia kweli ni dini waliyoileta Waarabu, nayo ni Uislamu.

Katika siku za hivi karibuni kuna sauti zinatumwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa WhatsApp na Instagram, zikidai kuwa kuna wafanyakazi wa majumbani nchini Oman wanateswa vibaya hadi kusema kuwa wanauawa kwa makusudi na wengine wanapangiwa njama za kuuliwa ili wawe mihanga kwa majini ya Kiomani. Mojawapo ni sauti ya mama mtu mzima ambaye dhahiri kabisa inaonekana kuwa alitumwa kusudi kutukana dini ya Kiislamu.

Hilo ndilo lengo lao hasa, maana hakuwa na haja ya kutaja maneno kama vile kuwa watu wanasali sala tano kila siku halafu wanatesa watu. Hiyo haikuhusu kabisa. Ikiwa sala tano zinawaudhi basi wataumia sana. Mimi binafsi nimeishi na Mlokole wa Kanisa la Efatah, (mlokole) ni wale wanaojiita wasafi kwa jina la Yesu, huyo mama kila mwezi au wiki tatu hubadilisha mfanyakazi au wanaacha kazi kwa mateso yake. Sasa jee huyu mlokole anashinda kanisani kusali mpaka ndoa zinavunjika, hivyo tumuweke kundi gani? Mbona hawasemi “wanasali siku nzima na makelele mtaani na ni hao hao wanatesa wafanyakazi!” Jamani tuishi kwa kusema ukweli kuwa fitina za uzushi ni mbaya na haupiti muda huwarudia mwenyewe.

Kuna na mwengine ambaye anasema ni Mkenya anayedai kuwa alitaka kuuliwa na waliomuajiri Oman ili akawe kafara kwa mizimu ya Oman. Naye huyu ni mzushi mkubwa na unauona uzushi wake mara moja ukiwa si mtepetevu wa akili na unaweza kupima anayoyasema. Hebu hapa tutumie akili zetu kuchambua aliyoyasema:

Kwanza, anatuambia anakijua Kiarabu vizuri sana bila ya kututolea ushahidi. Lakini, tumkubalie kwa hili.

Pili, eti amewasikia waajiri wake wakipanga njama za kumuuwa ili kumtoa muhanga na akawasikia vizuri; hivyo kweli waajiri hao wapange njama zao mbele yake naye anawasikia!?

Tatu, eti ameingia chumbani kwake na akafungua ‘air condition’ na kupanga mito kama kuwa yeye amelala na kutoroka asije akauliwa na kutolewa muhanga! Tunajuaje kama huu ni uwongo? Jawabu: Waarabu hawakuwa na mila ya kumtoa binadamu muhanga hata katika siku hizo za ujahiliya kabla ya Uislamu, itakuwa leo!? Hii ni mila yao wenyewe baadhi ya Waafrika na anataka kuipandikiza kwa Waarabu! Tafuteni uzushi mwingine, huu hautafaa.

Nne, eti ametaka ubalozi wa Kenya kumsaidia na hawakumsaidia. Wakatae kumsaidia kwa sababu gani? Anasema haya ili tukitaka kuujua ukweli kutokana na Ubalozi tusiweze kuupata. Kwa nini? Kwa sababu anayoyasema si ya kweli kwani kesi zote zinazofikishwa balozini kokote duniani husajiliwa na hatua huchukuliwa na ubalozi. Huyu mzushi sura zake tumeshaziona, sasa na atuoneshe paspoti yake na mihuri ya kuingia na kutoka Oman na viza yake ya kufanya kazi Oman kama mkweli, tutaifuatilia kesi yake.

Tano, kwa vile waajiri wameshafikwa na mengi kutokana na waajiriwa, kuna walioibiwa dhahabu za kina mama, makarani waliofyeka pesa benki na kadhalika na kadhalika, ndio maana waajiri hao huchukua paspoti na kuziweka wao na kumpa mfanyakazi anapotaka kusafiri kihalali; mfanyakazi huwa na kadi tu. Sasa huyo mzushi, paspoti ya kusafiria aliipata wapi? Tiketi alimlipia nani?

Sita, hapana shaka, hata angelikuwanayo paspoti, hapana shaka ilichukua muda kabla ya kuweza kusafiri, hivyo siku ya pili asubuhi waajiri wake walipokuwa hawamuoni, unafikiri nini wangefanya awali? Si wangelipiga ripoti polisi kuwa mtumishi wao haonekani! Unafikiri polisi hufanya nini? Si hupeleka habari katika kila kituo cha usafiri. Na wakishapiga ripoti na popote atakapotaka kuondokea lazima wangelimzuia na wangelimuhoji na kama ana kesi ya kuwashitaki waajiri wake, basi kesi ingelifunguliwa na waajiri kushtakiwa. Sasa huyu mzushi ameondoka vipi Oman!

Nimekuandikieni haya kwa muhtasari tu. Mkifikiria vizuri mtagundua kuna hoja nyinginezo zinalifanya porojo hili kuwa la ki-paukwa pakawa. Hivyo basi, mkipanga njama zenu wazushi wa fitina tumieni akili, kama mnazo!

Mwishoni nasema kuwa wafanyakazi wa majumbani walioko Oman wanatoka kila mahala duniani. Idadi ya Wafilipino peke yake ni kubwa kwa mara nyingi sana kuliko ya Watanzania na huwasikii ila wachache sana kulalamika. Lakini idadi ya walalamikaji kutoka Tanzania ndiyo iliyo kubwa kabisa ingawa jumla yao ni ndogo sana Oman. Waomani hawana shida ya wafanyakazi. Wala hawatapungukiwa wala kuharibikiwa iwapo wafanyakazi kutoka Tanzania watazuiliwa kwenda kufanya kazi Oman. Sasa kazi kwetu. Kusuka au kunyoa.
Download  Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa

                            Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
                       Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
                       Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa

0 comments:

Post a Comment