SIMBA imesikia kilio cha mashabiki wake ambao wamekuwa wakiukosoa
udhaifu uliopo kwenye kikosi chao na sasa uongozi wa timu hiyo umeamua
kufanya kweli, kwa kupanga mikakati ya usajili kimya kimya, ili
kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Huku Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiendelea ukingoni, Simba
imeanza kukitathmini kikosi chake kuelekea msimu ujao wa Ligi na
michuano ya kimataifa kama watapata nafasi hiyo.
Habari za uhakika kutoka kwa mmoja ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Simba, zimelieleza kwamba, kwa sasa wanahitaji kujaza wachezaji wa
kimataifa katika nafasi tatu muhimu, ambazo ni straika, beki wa kulia na
kati.
Nafasi ya straika mpaka sasa wana uhakika wa kumsainisha straika wao wa
zamani, Mganda Emmanuel Okwi, kuchukua nafasi ya Frederick Blagnon
anayetemwa, huku utata ukibaki kwa beki Mcongo Janvier Bukungu.
Kwa mujibu wa mjumbe huyo, Bukungu ameibua mvutano baina ya viongozi,
kwani kuna wanaotaka abaki, wengine wakitaka aachwe ili atafutwe beki wa
kulia shupavu atakayeweza kuhimili michuano ya kimataifa.
Mwingine anayetajwa kutupiwa virago ni beki Method Mwanjali, ambaye umri
mkubwa na majeraha ya mara kwa mara vinatajwa kutolishawishi benchi la
ufundi kumbakisha kikosini.
Straika wa kimataifa Mrundi, Laudit Mavugo, amebakizwa kundini kutokana
na mchango wake mkubwa, huku Mganda Jjuuko Murshid naye akisalia kwa
vile bado ana mkataba na Simba.
Aidha, kipa Daniel Agyei amefanikiwa kufanya kile kinachotakiwa langoni,
kwani ameonyesha uimara wa kutosha tangu ajiunge na timu hiyo katika
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Alisema hata hivyo, kikosi hicho kinaweza kikapanguliwa zaidi kama
watapata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, kwani timu hiyo ya
sasa haiwezi kuhimili michuano ya kimataifa.
“Viongozi wengi wanasikilizia kwanza, kama Simba itapata nafasi ya
kucheza michuano ya kimataifa, kikosi kitafumuliwa, utashangaa watabaki
wachezaji wachache sana,” alisema mjumbe huyo.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi>>>>Bonyeza Hapa
Follow me instagram>>>Bonyeza Hapa
Facebook page like hapa>>>Bonyeza Hapa
Jiunge na group la whatsapp>>>Bonyeza Hapa
0 comments:
Post a Comment