Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa onyo kwa Wabunge Halima
Mdee (Kawe) na Mwita Waitara (Ukonga) kwa kushindwa kufika mahakamani
kusikiliza kesi inayowakabili dhidi ya kumjeruhi Katibu Tawala wa jiji,
Theresia Mbando.
Kesi
hiyo imepangwa kusikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi na leo
kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa maelezo ya awali dhidi ya washtakiwa.
Upande
wa Jamhuri ukiongozwa na Esterlia Wilson alidai kuwa kesi hiyo
ilipangwa kusikilizwa maelezo ya awali lakini washtakiwa Mdee na Waitara
hawapo mahakamani.
Utetezi ulidai kuwa Mdee ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa amesafiri kwenda nchini Canada na Waitara ni mgonjwa.
Hakimu
alisema sababu zilizotolewa na upande wa utetezi hazina mashiko
kisheria kwa kuwa wameshindwa kuwasilisha vielelezo vya kuithibitishia
mahakama kwanini washtakiwa wameshindwa kufika kusikiliza kesi yao.
“Kama
kweli mshtakiwa Waitara ni mgonjwa upande wa utetezi mlipaswa
kuwasikilisha vyeti mahakamani na kuhusu mshtakiwa Mdee aliyesafiri kwa
safari zake binafsi kwenda Canada, siyo sahihi tunapaswa tuheshimu hizi
taratibu ili kila kitu kifanyike kwa haki ya pande zote” alisema Hakimu Shahidi.
Mbali
na Mdee na Waitara, wengine ni, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Saed Kubenea
, Diwani wa Kata ya Tabata Kimanga, Manase Njema , Diwani wa Kata ya
Kimara, Ephrein Kinyafu na mfanyabiashara Rafii Juma.
Wengine
waliounganishwa katika kesi hiyo ni, Diwani wa Kata ya Segerea Edwin
Mwakatobe (31) na Mkazi wa Tabata Edwin Mwaipaja (40).
Katika
kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Februari 27, mwaka huu katika Ukumbi wa
Karimjee, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam walimjeruhi Theresa
Mbando na kumsababishia maumivu mwilini mwake.
Washtakiwa
hao walikana mashtaka hayo kwa nyakati tofauti na upande wa Jamhuri
ulidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, uliomba tarehe nyingine ya
kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Hakimu alisema kesi hiyo itasikilizwa maelezo ya awali Julai 27, mwaka huu, dhamana ya washtakiwa inaendelea.
0 comments:
Post a Comment