Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema atampiga marufuku Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kufanya mikutano ya kisiasa Tanzania Bara kama hatamtambua kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.
Lipumba alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na viongozi wa CUF kwenye mkutano wa ndani mkoani Geita.
Ziara
ya Lipumba imefanyika wakati Maalim Seif akiwa amesambaza barua kwa
viongozi wa CUF wa wilaya zote nchini akiwataka wasishirikiane na
Profesa Lipumba huku akionya atakayekaidi atachukuliwa hatua.
“Kama
Maalim Seif hatambui kuwa mimi ni mwenyekiti wake, huku mimi
nikimtambua kuwa Katibu Mkuu wangu, basi naye tutamzuia kufanya mikutano
ya kisiasa Tanzania Bara,” alisema Lipumba.
Profesa
Lipumba alisema hana tatizo na wananchi wa Zanzibar wala kiongozi wa
upinzani atakayetetea watu hao na kuongeza kuwa yeye amekuwa mstari wa
mbele kutetea Wazanzibari.
“Mimi
natambua kuwa ndiye mwenyekiti halali wa chama hiki na mwenye mamlaka
ya kumwondoa mwenyekiti au katibu ni mkutano mkuu wa chama na lazima
theluthi moja ya wajumbe watoke Bara na theluthi nyingine Zanzibar,
lakini mkutano huo haukufanyika wala muhtasari haupo,” alisema Profesa Lipumba.
Alieleza kwamba kwa sasa yeye na wana CUF wengine wamejipanga kukijenga chama hicho.
Mwenyekiti huyo pia alizungumzia suala la Muungano akisema ni muhimu kwa usalama wa nchi na Taifa kwa ujumla.
Alisema
ili kulinda Muungano kuna mahitaji muhimu ya kuwa na vyama vyenye nguvu
vitakavyokuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wananchi wa pande
hizo mbili.
Lipumba
alisema amefika wilayani hapa akitoka Urambo kwenye msiba wa Spika wa
Bunge la Tisa, marehemu Samuel Sitta ambapo pia aliongea na baadhi ya
viongozi wa chama hicho.
“Tumeifika
Kahama kuzungumza na viongozi wa hapa na wa wilaya jirani, dunia ina
changamoto kubwa katika masuala ya demokrasia na kujenga utawala bora
kwa baadhi ya viongozi,” alisema Lipumba.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
Bonyeza Hapa CLICK HERE
0 comments:
Post a Comment