Hatma
ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema),
ilishindwa kujulikana jana baada ya mawakili wa Serikali kuweka
pingamizi, wakipinga Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kusikiliza maombi ya
dhamana yaliyowasilishwa na mawakili wa mshtakiwa.
Kaimu
Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Jaji Sekela Moshi, alisema kutokana
na pingamizi hiyo, atasikiliza hoja za sheria zilizowasilishwa
mahakamani hapo kabla hajatoa uamuzi wowote juu ya dhamana ya mshtakiwa.
Aliwaelekeza mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja za sheria kabla mahakama haijaendelea na hatua yoyote.
Jaji Moshi alisema atatoa uamuzi kuhusu mvutano huo wa sheria, Novemba 22, mwaka huu
Katika
maombi hayo namba sita ya mwaka 2016, Jamhuri iliwakilishwa na
mawakili, Matenus Marandu na Paul Kadushi wakati Lema anatetewa na jopo
la mawakili sita ambao ni Peter Kibatala, John Mallya, Adam Jabir, Sheck
Mfinanga, Faraji Mangula na Charles Adiel.
Katika
shauri hilo jana, hoja za sheria za pingamizi zilianza kusikilizwa saa
4:54 asubuhi hadi saa 7:25 mchana ambako mawakili wa Serikali na wale wa
upande wa utetezi, walichuana vikali kujenga hoja.
Akiwasilisha
pingamizi hilo, wakili Kadushi, aliiomba mahakama iwaruhusu kuwasilisha
pingamizi moja na kama mahakama ikishindwa kuridhia pingamizi hilo,
wawasilishe pingamizi la pili.
Alidai
maombi hayo yaliyosainiwa na wakili Kibatala yanalenga katika kifungu
cha 372 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachoipa
Mahakama Kuu kufanya mapitio ya mashauri ya kesi za mahakama za chini.
Alidai
hoja ya sheria inasema mabadiliko ya sheria yaliyofanyika mwaka 2002
yaliondosha haki za pande zote katika kesi za jinai kuomba rufaa au
mapitio ya uamuzi mdogo uliofanywa katika mahakama zinazoongozwa na
mahakimu nchini.
“Kwa
mujibu wa kifungu cha 43 (2) cha sheria ya mahakama za mahakimu, maombi
hayo yanakinzana na kifungu hicho kwani uamuzi huo mdogo unaopingwa na
mawakili wa mshtakiwa, haujamaliza shauri la jinai.
“Lakini
pia, uamuzi huo unaobishaniwa na mawakili wa mshtakiwa, uko katika
ukurasa wa 17 hadi 19, hivyo mahakama inafungwa na sheria kusikiliza
rufaa au mapitio katika uamuzi mdogo.
“Kwa
kuwa uamuzi ni mdogo mahakama inakuwa na uamuzi wa kutupilia mbali
maombi haya na kusubiri tuendelee na mwenendo wa kesi. Lakini, kama
mahakama haitavutiwa au kushawishiwa na hoja hii, tunaomba kutoa hoja
ya pili,”alidai wakili Kadushi
Baada
ya hatua hiyo, hoja ya pili iliwasilishwa ikisema maombi ya Lema
hayajakidhi matakwa ya sheria, kifungu cha 359 (1) cha Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka
2,002.
Kwa
mujibu wa wakili Kadushi, kifungu hicho kinaelekeza namna mtu
asiporidhika na uamuzi uliotolewa na mahakama ya chini, anavyotakiwa
kukata rufaa mahakama kuu.
“Msingi
wa sheria umeshawekwa na mahakama kuwa maombi ya kufanya mapitio kamwe
siyo mbadala wa rufaa na uamuzi mwingi umetamka hivyo,” alidai wakili Kadushi.
Katika
maelezo yake, wakili huyo alirejea mashauri mbalimbali ya Mahakama Kuu
na Mahakama ya Rufaa yenye kesi za namna hiyo na kudai kuwa kulikuwa na
haki ya waleta maombi kukata rufaa na haki hiyo ipo mpaka sasa.
Kibatala
ambaye alikuwa akiwawakilisha mawakili wenzake watano, alidai hoja za
sheria zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri hazina
msingi katika sheria na akaiomba mahakama izitupilie mbali.
Aliiambia
mahakama kwamba hakimu aliyeruhusu wakili wa Serikali kusimama kabla
hajafikia mwisho wa uamuzi aliokuwa akiusoma ni ishara kuwa mahakama
hiyo haikuongozwa vizuri jambo ambalo linaifanya Mahakama Kuu iingilie
kati na kutoa maelekezo.
“Hoja
walizoleta Serikali hazijakidhi matakwa ya sheria. Kwanza kabisa,
pingamizi lao halijasema linakuja kwetu au linakwenda kwa mahakama kwa
sababu sisi na Serikali tumeitwa hapa mahakamani na hii ni kama
mwananchi wa kawaida kwenda kwa msajili kulalamika kisha jaji akaziiita
pande zote mahakamani,” alisema Kibatala.
Alisema
wanaishangaa Serikali kuzungumzia kifungu cha 43 ambacho barua ya
maombi yao haijakizungumza na pia mahakama kuitisha majalada na kupitia
yaliyotokea mahakama za chini, inajenga mamlaka na kuruhusu mahakama kuu
kuitisha majalada hayo kupitia mwenendo au uamuzi.
“Kifungu
cha 373 cha sheria hiyo ya makosa ya jinai, kinaelezea jinsi Mahakama
Kuu inavyoweza kupata taarifa ya upungufu wa mwenendo katika mashauri
yanayoendelea mahakama za chini.
“Mfano
mahakama za chini zinaruhusiwa zenyewe kupeleka majalada mahakama kuu
ili kupitia mwenendo au kupata taarifa yoyote au kuomba namna ya
kurekebisha wanapokosea na hata mwanasheria mkuu wa Serikali amewahi
kutumia mfumo huu katika kesi mbalimbali,” alisema Kibatala.
Alisema
mahakama kuu ina mamlaka ya kupokea malalamiko na kuyafanyia kazi na
ina uhuru wa kuitisha majalada na kusikiliza maombi ya upande wowote
kati ya Serikali au utetezi.
Katika
maelezo yake, Kibatala alisema kifungu cha 148 (3) cha Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinasema rufaa inaweza kukatwa kama mtu
amenyimwa dhamana ila uamuzi wa mtu kunyimwa dhamana haukatazi
mshitakiwa kuomba mapitio ya uamuzi huo.
“Mahakama
ilijivua mamlaka ambayo inayo ikiwa ni pamoja na kazi yake ya sheria.
Katika hili, hakimu alikosea kumruhusu wakili wa Serikali kusimama
katikati ya uamuzi.
“Nasema
hivyo kwa sababu kifungu cha 148 (6) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa
ya Jinai kinasema mahakama ikitoa dhamana kwa mshitakiwa ni lazima
ifikie mwisho wa hatua ya uamuzi wake kwa kuweka masharti ya dhamana.
“Lakini
katika suala hili, mahakama iliishia njiani baada ya wakili wa Serikali
kuingilia kati na kueleza kusudio la kukata rufaa.
“Jukumu
letu ni kuiongoza mahakama na siyo kuviziana ili tushinde. Hapa Kadushi
amedai haturuhusiwi kuomba mapitio au rufaa ila akasema tulipaswa
kukata rufaa na siyo kuomba mapitio ya mwenendo wa uamuzi ule.
“Kwa
misingi hiyo, ndiyo maana tunasisitiza kwamba pingamizi la Jamhuri
halina mashiko yoyote ya sheria, tunaomba litupiliwe mbali na mahakama
isikilize maombi yetu,” alisema Wakili Kibatala.
Katika
maombi hayo, Lema kupitia mawakili wake, anaiomba mahakama hiyo ifanye
mapitio ya majalada ya kesi za jinai namba 440 na 441 ya mwaka huu
ambako anakabiliwa na makosa ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John
Magufuli
Mawakili
hao wa Lema wanaomba ombi hilo kwa sababu wakati Hakimu wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha akisoma mwenendo wa uamuzi huo
uliokuwa na kurasa 22 hivi karibuni, alisema mahakama hiyo inamwachia
Lema kwa dhamana kwa masharti atakayopewa na mahakama hiyo.
Hata
hivyo, kabla hajakamilisha uamuzi huo akiwa katika ukurasa wa 21 kati
ya kurasa 22, mawakili wa Serikali walisema Serikali inakusudia kukata
rufaa juu ya uamuzi huo.
Wakati
hayo yakiendelea, jana nje ya mahakama kuu, kulikuwa na ulinzi mkali
wa polisi na askari magereza waliokuwa na silaha za moto.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
Bonyeza Hapa CLICK HERE
0 comments:
Post a Comment