Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amepiga marufuku
wauzaji holela wa samaki na mboga mitaani badala yake wapeleke katika
masoko maalumu.
Aidha ameliagiza jeshi la polisi na halmashauri zote mkoani humu kuwakamata wafanyabiashara watakaokiuka agizo hilo.
Makonda alitoa kauli hiyo jana, wakati alipotembelea Soko la
Kimataifa la Samaki la Feri na kuzungumza na wafanyabiashara wa soko
hilo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika Wilaya ya
Ilala.
Wafanyabiashara hao walieleza kuwa, moja ya changamoto
zinazowakabili ni pamoja na kuzagaa kwa wafanyabiashara huria wa samaki
hususani katika vituo vya mabasi ya daladala na pembezoni mwa barabara
mkoani humo.
Walidai kuwa, hali hiyo inahatarisha uhai wa soko hilo kwani watu
wengi hawafiki kununua samaki katika soko hilo, badala yake huishia
kununua katika vituo vya mabasi na mitaani.
Mfanyabiashara Said Ally alimueleza mkuu huyo wa mkoa kuwa, masoko
huria ya mitaani yanaendelea kushamiri huku viongozi wa halmashauri na
wananchi wakikaa kimya.
“Mkuu wa mkoa tusaidie sasa hivi kila kona kuna wauza samaki
hasa katika vituo vya mabasi jambo linalosababisha feri tunakosa wateja
wanaishia mtaani, soko litakufa kwa sababu watu hawaji tena tofauti na
awali,” alisema Ngasa.
Mbali na hayo wafanyabiashara hao waliomba kuboreshwa kwa
miundombinu ya soko hilo ambayo imechakaa licha ya soko kuwa la
kimtaifa.
Kutokana na malalamiko hayo, Makonda alipiga marufuku biashara ya
samaki na mboga mitaani na kumuagiza Kamanda wa Operesheni, Kanda Maalum
ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya kuwashughulikia wafanyabiashara wote
watakao kiuka agizo hilo kuanzia sasa.
“Ni marufuku kufanya biashara ya samaki na mboga katika maeneo
ambayo sio rasmi wafanyabiashara wapeleke katika maeneo yaliyotengwa kwa
ajili ya kufanyia biashara hizo,” alisema Makonda.
Download Application ya Hebron Malele Blog Kwenye Simu yako Kusoma Habari Zetu Kwa Urahisi
Bonyeza Hapa CLICK HERE
0 comments:
Post a Comment